YESU NI JIBU

Jumatatu, 20 Julai 2015

EAGT CITY CENTRE WAITEKA DAR! KWA KUHAMA KUTOKA KATIKA VIWANJA VYA SABASABA KWENDA KWENYE ENEO LAO LILOPO MTONI MTONGANI.

Mamia wajipanga barabarani kustaajabu.
“Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa   masikio; bali sasa jicho langu linakuona.”
 Kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli walipotwaa kila kilicho chao na kuongozwa na wingu la uwepo wa Bwana, kutoka Misri kuelekea Nchi ya ahadi (Kanaani) ndivyo ilivyokuwa Jumapili iliyopita wakati maelfu kwa maelfu ya wana- familia ya Kanisa la EAGT City Centre, chini Mchungaji kiongozi, Florian Josephat Katunzi, walipotwaa vilivyo vyao, na kuandamana  toka eneo la Viwanja vya maonyesho ya Biashara, vya Mwl. Nyerere (Sabasaba)  kuelekea “Nchi ya Ahadi” Mtoni Mtongani Relini, huku mamia ya wana wa jiji la Dar es Salam, bila kujali dini zao wakijipanga bara barani na wengine kuparamia mapaa ya nyumba kustaajabia maandamano hayo ya kihistoria yaliyofunga barabara ya Kilwa kwa muda.

Zoezi la uzinduzi wa kanisa likifanywa na mchungaji kiongozi wa kanisa la EAGT City Center mchungaji Florian Katunzi.













“Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa   masikio; bali sasa jicho langu linakuona.” Maneno hayo yalitamkwa na mchungaji kiongozi wa kansia la EAGT City Centre, Florian Josephat Katunzi, Jumapili iliyopita mara baada ya kukanyaga katika ardhi lilipojengwa Kanisa la kisasa kule Mtoni Mtongani Relini akinukuu maandiko ya Biblia katika kitabu cha Ayubu 42:5.

 Ilikuwa majira ya saa saba mchana wakati anga likiwa angavu, Bendi ya Jeshi la Polisi wakiongoza maandamano kwa wimbo usemao: “Mwambie Farao nimeokoka sitarudi tena misri naelekea kaanani………”
Mbele Mchungaji kiongozi akiwa sambamba na mwimbaji wa nyimbo za Injili Tumsifu Rutufu, aliyevalia majoho kama ya Mussa na kilemba kichwani, sambamba na viongozi wa kanisa hilo walitembea kwa miguu kuelekea mtoni Mtongani, huku maelf ya wana-familia ya EAGT, wakibeba viti vyao  na kufunga kwa muda Barabara ya Kilwa.
Waandamanaji walipofika kwenye daraja la Reli (Mtoni Mtongani, walikunja kona kuelekea upande wa kushoto na kuchora alama ya elo, iliyokuwa kivutio kikubwa, kisha kuingia “Kanaani” eneo lilipojengwa jengo la kisasa, lakini la muda lenye uwezo wa kuhimili watu 3000.

Akikata utepe kukanyaga eneo hilo, Mchungaji Katunzi alisema: “Sasa Bwana ametupa eneo hili kuwa eneo la kumuabudu na kumpa utukufu unaomstahili. Mahali hapa hapatakuwa eneo la wachawi na vinyamkera tena, bali ni mahala pa ushindi na kufunguliwa.” 
Huku akijawa na uwepo wa nguvu za Mungu, Mch. Katunzi aliinua mikono juu na kuwaongoza maelfu kumshukuru Mungu kwa matendo makuu aliyolifanyia kanisa lake, akawabariki wote waliokuwa kwenye maandamano hayo  na kisha kuliombe Taifa, akimsihi Mungu alivushe salama katika matukio muhimu yanayoenda kutokea mwaka huu ikiwa ni pamoja na uchaguzi Mkuu.

Katika hotuba fupi ya kuhitimisha tukio hilo la kiibada, Mch. Katunzi alisema; huu ni mwaka wa uchaguzi na kanisa limeingia kwenye maombi, wagombea wanaotegemea makafara na uchawi hawatachaguliwa kamwe, bali wale wanaomtazama Mungu na kutumainia maombi.
JINSI YA KUFIKA  EAGT CITY CENTRE, MTONI MTONGANI (RELINI)
 Kanisa liko kandoni mwa Daraja la juu la Reli ya TAZARA eneo la Mtoni mtongani,  kama hatua 100 kutoka barabara kuu.
 Unaweza kuwasiliana nasi kwa simu:
0718-267171
0754367826
0784367826

0713803057

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni