Ukomo wa nguvu za
uchawi
katika kuigiza
miujiza ya Musa
“BWANA
akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi,
ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri. Nao wakafanya; Haruni
akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa
chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa
katika nchi yote ya Misri. Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa
uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa
juu ya wanadamu, na juu ya wanyama. Ndipo wale waganga wakamwambia Farao,
Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize;
vile vile kama BWANA alivyonena.” (KUT. 8:16-19)
Maandiko tuliyonukuu hapa juu,
yanadhihirisha jinsi ambavyo hapo mwanzo wachawi wa Farao walijaribu kuigiza
miujiza ya Musa ili kushindana naye. Na ukweli wa macho walionekana kufanikiwa
na kumpa Farao Kiburi. Hali ingeliweza kumchanganya Musa, kuona wachawi nao
wanafanya miujiza ile ile anayoifanya. Lakini Musa hakuteteleka kiimani, badala
yake alimwamini Mungu kujitetea kwa kudhihirisha uweza wake dhidi ya nguvu za
wachawi wa Farao. Hatimaye, tunashuhudia katika
maandiko wachawi walikwama kuigiza “muujiza wa kuleta chawa”. Tunasoma kwamba:
“….Hao waganga nao wakafanya mfano wa
hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze;….” Baada ya
kushindwa ilibidi wakiri waziwazi kwa Farao wakisema kwamba: ”jambo hili ni chanda cha Mungu…”
Kana kwamba hii haikutosha, miujiza
mingine iiliyofuatia ya mapigo ya Musa dhidi ya Farao; hata waganga wake
hawakusalimika. Tunajionea kupitia maandiko kuhusu muujiza wa pigo la majipu
ambapo tunasoma: “Basi wakatwaa majivu ya tanuu na kusimama mbele ya Farao; na Musa
akayarusha juu mbinguni nayo yakawa majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya
wanadamu na juu ya wanyama. Nao wale waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa
kwa sababu ya hayo majipu, kwa maana hao waganga walikuwa na majipu, na Wamisri
wote walikuwa nayo.” (Kut.9:10-11)
Mapambano kati ya
Simoni mchawi
na Filipo aliyejaa
Roho Mtakatifu
Injili iliyohubiriwa
na mitume na wainjilisti wa kanisa la kwanza nayo pia iliambatana na ushindani
dhidi ya nguvu za uchawi. Ili kuupata ushahidi wa haya nisemayo, hebu twende
kwenye kitabu cha Matendo ya Mitume na kuangalia kisa cha mchawi aliyekua
maarufu sana katika jimbo la Wasamaria:
“Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa
akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza
watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu.
Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza
muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo,
akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo,
wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa
alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka. (MDO 8:9-13)
Kwa mujibu wa
maandiko tuliyosoma tunathibitisha kwamba, mchawi Simoni aliwashangaza
Wasamaria kwa muda
mwingi kwa uchawi wake; tena akasifiwa sana kwamba alikuwa na “uweza mkuu wa Mungu”. Na kwa kuwa
hapakuwepo mshindani wake, aliteka usikivu wa watu wote kuanzia mdogo hadi mkubwa. Bila shaka
alifanya utapeli huu kwa miaka mingi.
Lakini wakati muafaka ulifika dhidi ya
Mchawi Simoni kupata changamoto. Tumesoma habari za Mwinjilisti Filipo ambaye
aliingia Samaria na kukuta Simoni akiendelea na mazingaombwe yake. Filipo
hakutaka kushindana na Simoni ana kwa ana kwa kumkemea na kumgombeza kwa
matamko ya matishio ya maneno. Filipo aliamua kuihubiri Injili ya Kristo na
kumruhusu Roho Mtakatifu afanye kazi yake.
Tumeshuhudia jinsi ambavyo Filipo
alitumiwa kufanya miujiza iliyovunja rekodi ya uchawi wa Simoni, na wateja wote
wa Simoni walimwamini Yesu Kristo aliyehubiriwa na Filipo wakafunguliwa katika
vifungo vya pepo na kuponywa magonjwa na kuponywa ulemavu wa viungo vya mwili.
Hatimaye tumeshuhudia mchawi SImoni naye “akibwaga manyanga” yake na
kujisamilisha kwa nguvu za Roho Mtakatifu aliyekuwa naye Filipo.
Paulo alivyoshindana
na mchawi Bar-Yesu
Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa
chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake
Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye
akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno
la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake),
akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani.
Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho,
akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa
haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia,
mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara
kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika
mkono na kumwongoza. Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka,
akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana. (MDO 13:6-12)
Kwa mujibu wa
maandiko haya, tunashuhudia jinsi ambavyo uchawi unaweza kutafsiriwa kuwa ni
huduma ya kinabii. Kwa sababu ya miujiza ya kimazingaombwe inayofanywa na
wachawi/waganga, watu wengine hudanganyika kwa kudhani kuwa hizo ni nguvu za
Mungu, hasa pale ambapo mchawi husika anapoamua kutumia mwavuli wa dini kama
kinga ya kuficha uchawi wake. Lakini, pamoja na hao wachawi, kujificha chini ya
mwavuli wa dini; hawawezi kushindana na utendaji halisi wa nguvu za Roho
Mtakatifu! Tunamwona Paulo akitumia nguvu za Roho Mtakatifu kumdhibiti
Bar-Yesu!
Itaendelea toleo lijalo
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI.