Katika toleo
lililopita tulianza mada mpya ya “ukiheshimiwa heshimika” ambapo tulichambua
maeneo matatu yaliyojumuisha “Utangulizi”; “Vyanzo vya heshima”; na “Tishio la
kujivunjia heshima baada ya kuheshimiwa”! Leo tutaingia katika sehemu muhimu ya
sababu kubwa ya kibibilia ambayo husababisha wengi wanaofanikiwa na kuheshimiwa
hupoteza heshima zao katika jamii:
Mtazamo wa Yesu
kuhusu kujikinai na kuacha
kuheshimika
Bwana Yesu aliwahi kuongelea tatizo la hali ya
kujikinai baada ya kufanikiwa kiasi cha kudhani mafanikio ni “kibali cha kuishi
milele duniani”! Katika kuweka mkazo kuhusu tabia hii, Yesu alitoa mfano wa mtu
mmoja tajiri aliyeonesha kujikinai kwa utajiri wake na kutamba kuishi duniani
bila ukomo:
“Akawaambia, Angalieni,
jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo
navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa
limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina
pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja
ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote
na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi
ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.
Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho
yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu
ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu. “ (LK. 12:15-21)
Kwa kupitia maandiko haya, unaweza kusoma baadhi ya
kauli za tajiri jinsi alivyojikinai akisema: “….ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka
mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi…” Kumbuka kwamba huyu tajiri
hakuupata utajiri wake kwa njia za ufisadi. Aliupata kwa njia halali kabisaaaa.
Alilima shamba lake “likazaa sana…”
Aidha, mpango wa kujenga ghala za kuhifadhi mali
zake haukuwa jambo baya hata kidogo! Tatizo lake lilikuwa ni kujikinai,
na kujisahau, kwa kufikiri kwamba alifikia kilele cha mafanikio hayo kwa nguvu
zake binafsi na kwamba uhai wake utalindwa na wingi wa mali zake!
Ni upumbavu kuacha
nyuma mali nyingi
uondokapo badala
ya kuzitanguliza uendako
Kutokana na maneno ya Yesu, inaonesha kwamba tabia
ya kukusanya na kijilimbikizia mali nyingi kisha ukaondoka na kuziacha bila
kuzifaidi ni “Upumbavu”! Kwa mujibu wa maneno ya Yesu ni kwamba upumbavu huu
hauishii katika kujilimbikizia peke yake, bali kushindwa kuzitumia mali kwenye
mambo ya ufalme wa Mungu; na matokeo yake mhusika kuondoka duniani ghafla na
mali zake kuchukuliwa na wengine wasiozitaabikia tangu mwanzo:
“….Mpumbavu wewe, usiku huu wa
leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?
Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu..”
Uchunguzi wangu wa kimaandiko katika mada hii,
nimebaini kwamba, kujikinai sio kujisifia utajiri peke yake, wala sio kumsahau
Mungu peke yake, bali ni matumizi ya utajiri wenyewe ambayo Yesu amesema
kwamba “….ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa
Mungu.”
Mambo mawili muhimu hapa. Kwanza, ni tatizo la
kujilimbikizia akiba isiyo na matumizi bali imekaa tu kwenye hifadhi yake.
Pili, kukataa kutumia akiba ya mali katika vipaumbele vya Mwenyezi Mungu
alivyoamuru kwa wale wanaomiliki mali nyingi!
Yesu aliposema “kujitajirisha kwa Mungu” maana yake
halisi kwa tafsiri ya toleo la Biblia ya Kiingereza cha Amplified limesema: “So it is
with the one who continues to lay up and hoard possessions for himself and is
not rich his relation to God…..”
Haya maneno ya “…to lay up and
hoard possessions…” yana maana ya kukusanya
na kujilimbikizia..” Maana yake na ulimbikizaji ambao matumizi yake hayana
mchango wa uhusiano na huduma za kimungu.
Katika uchambuzi huu kuhusu mfano wa Yesu tunajifunza
mambo muhimu yafyatayo:
1. Tishio la mali kuchukuliwa
na wengine
Mtazamo wa kujilimbikizia mali nyingi ili hatimaye
ndipo mkusanyaji apate kuzifaidi hapo baadaye si kitu kipya. Yupo mchaji Mungu
aliyepata kuwa tajiri sana kuliko wengi duniani, ambaye alifanya utafiti kuhusu
hatma ya utajiri ambapo alihitimisha kwa kusema hayo nayo ni ubatili:
"Nami nikaichukia kazi
yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia
yeye atakayenifuata. Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima
au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha
nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonyesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni
ubatili."(MHU. 2:18, 19)
Kuna maneno haya “……kazi yangu yote niliyojisughulisha nayo chini ya jua,…..” “……..sina budi kumwachia yeye atakayenifuata…….”
“…… atatawala juu ya kazi yangu yote
niliyojishughulisha nayo…….” hayo
nayo ni ubatili.”
Aliyeandika haya ni mfalme Sulemani ambaye
alijikusanyia mali na utajiri mwingi kuliko matajiri wote wa ulimwengu
waliowahi kuwepo kabla na baada yake. Ushahidi mwingine wa utafiti wa Mhubiri
unapatikana katika maandiko yafuatayo:
“Maana kuna mtu ambaye kazi
yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu
asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu.”
(MHU. 2:21)
Katika maandiko haya tunakutana na maneno haya.. “….Mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na
maarifa, na kwa ustadi….” “…….naye
atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake…”
Hili jambo lilimchanganya sana Sulemani. Mtu
anakusanya mali nyingi kwa muda mrefu na nguvu nyingi, akisha kufikia kilele
cha ulimbikizaji kabla hajazifaidi anaondoka ghafla, na mtu mwingine
anazichukua bila kuzitaabikia!!
2. Kufananishwa na Mpumbavu
Yesu anamtaja tajiri Yule kuwa “Mpumbavu”!
Ukifuatilia kwa makini Bibilia inamtafsiri “mpumbavu” ni mtu yeyote asiyetambua
uwepo wa Mungu:
“Mpumbavu amesema moyoni,
hakuna Mungu; wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, hakuna atendaye
mema.” (Zab.14:1)
Hivi ndivyo Yule tajiri mkulima alivyoonnesha
upumbavu wake ambapo Yesu aliutafsiri kwamba ni “dhana potofu ya uzima wa mtu
kuwa katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo..”
3. Jinsi ya kuweka akiba yenye
tija ya milele
Haya basi, baada ya kuuthibitisha hasara ya kujilimbikizia
mali na kisha kufa ukaziacha na kuondoka patupu, Yesu alipendekeza njia ya
kunufaika na mali za duniani hata baada ya kuondoka duniani ni kuhakikisha
matumizi ya mali hizo yanatoa kipaumbele kwa mambo ya ufalme wa Mbinguni:
“Msijiwekee hazina duniani,
nondo na kutu viharibupo, na wevi hujunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina
mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala
hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.”
(Mat.6:19-21)
Katika maandiko haya, ukiyatafsiri kwa mtazamo wa
mfano wa tajiri aliyejilimbikizia mali kibinafsi, utagundua maana kama
ifuatavyo: Kwanza, kukusanya mali na kuzitumia kwenye mambo ya ufalme wa Mungu
ndiyo njia pekee ya kulimbikiza mali mahali salama kwa maana kwamba mali
zinakutangulia uendako badala ya kuziacha nyuma yako uondokapo.
Majumuisho kuhusu
kujikinai na kupoteza heshima
Watu wengi hutumia nguvu na muda mwingi katika
kutafuta mafanikio kwa njia mbali mbali. Baada ya kufikia mafanikio na wahusika
kupata kutambuliwa, na kupata umaarufu na heshima kutokana na mafanikio
waliyoyapata, ghafla hubadilika kitabia na kupotesha heshima ile ile waliyokuwa
wameipata kutokana na kazi kubwa waliyokwisha kuifanya.
Moja wapo ya tabia mbaya inayopoteza heshima ni
kujikinai na kudhani kwamba, mafanikio hayo ni juhudi binafsi na Mungu hana
sehemu wala jamii inayowazunguka. Kimsingi hakuna mtu afanikiwaye yeye peke
yake kwa juhudu zake binafsi, pasipo ridhaa ya Mungu, na pasipo mikono ya watu
wengine kuhusika kwa njia moja au nyingine. Hata kama maono, mipango na
mikakati ya utekelezaji imebuniwa na mtu mmoja; bado ufanisi wake lazima
hujumuisha wengi hata kama waliohusika walifanya hivyo kwa malipo.
Aidha, ni upumbavu wa hali ya juu, pale ambapo mtu
afikiapo mafanikio ya kiuchumi, kufikiri kwamba ataishi milele duniani ili
kunufaika kibinafsi na utajiri aliojilimbikizia hapa duniani. Tunao ushahidi wa
maelfu ya watu wengi ambao kwa muda fulani walifanikiwa katika kumiliki uchumi
na kupata umaarufu lakinii ghafla wahusika wakatoweka ghafla kwa maradhi
yaliyooshindikana kutibika japokuwa walikuwa na mali nyingi. Mali zile
hazikuwasaidia kudhibiti na kurefusha maisha yao, wakaondoka pasipo kutaka.
Kana kwamba hii haitoshi, watu wengi
waliojilimbikizia mali nyingi, wanapoondoka ghafla haichukui muda mrefu hata na
mali zile walizohifadhi huangukia mikononi mwa watumiaji wasio na uchungu nazo,
na kisha kutoweka na kubaki historia tu.
Matokeo haya, ya kujikinai na kuishia kupoteza
heshima ni changamoto kwa jamii ya kizazi cha wanaofanikiwa katika karne hii ya
ishirini na moja. Katika toleo lijalo tutapitia kwa kina matumizi mabaya ya
mali na utajiri na athari zake kwa wahusika pamoja na jamii kwa jumla.
Itaendelea toleo lijalo