Huyu Ndiye Askofu Mkuu
Mteule wa Kanisa la EAGT. Brown Mwakipesile! Ndie Ameshika nafasi ya aliyekuwa
Askofu Mkuu Babu Moses Kulola.
Hatimaye mrithi wa kiti cha
mwanzilishi wa kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT),
Mwanainjili, Dk. Moses Samwel Kulola, aliyemaliza kazi yake na kutwaliwa,
atajulikana amejulikana baada ya wachungaji kutoka kila kona ya nchi watakapokutana
mjini Dodoma, katika mkutano mkuu utakaomchagua Askofu Mkuu wa Pili wa kanisa
hilo la kiroho.
Kiti cha Askofu Mkuu wa EAGT, kimekuwa kikikaimiwa na Makamu Askofu, Asumwisye
Mwaisabila, tangu, Askofu Dk. Kulola alipoimaliza kazi, alhamisi Agosti 29,
mwaka 2013, na kwa mujibu wa katiba ya kanisa hilo, mwaka huu ni wa uchaguzi na
tayari maaandalizi yote yamekamilika.
Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini wa Kanisa la EAGT, Mch. John Henry Mfuko, kuhusu mwelekeo wa
uchaguzi, sifa za anayestahili kukikalia kiti hicho na matarajio ya wana-EAGT,
katika kipindi hiki muhimu.
Mzee huyu aliyetembea na
Askofu Kulola katika safari za Injili wakitaabika nyikani, jangwani na mstuni
katika hali zote alisema:
“Tunaelekea Dodoma kumchagua Askofu wa pili wa kanisa letu. Nitaenda
Dodoma…lazima niende. Uchaguzi wa wakati huu ni tofauti sana kwa kuwa watu
wameomba na tunaendelea kuomba na mkono wa Mungu uko juu yetu.”
Kisha aliongeza: “Si Yesu
alisema ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, bisheni nanyi
mtafunguliwa? Tunakwenda kumpata yule aliyestahili kuliongoza kanisa na si kwa
mazoea, ni yule ambaye ataliongoza kanisa kulingana na hitaji la sasa.”
Alisema; wakati wao Injili
ilienezwa kwa mbinu tofauti na hali ilivyo sasa, wakati huu Kiongozi
anayetakiwa wala si kwa kigezo cha elimu tu, bali ni yule atakayeongoza kwa
vitendo kulipeleka mbele kanisa na si mtawala.
Mzee huyo wa Injili
aliyezaliwa mwaka 1930, alisema kuwa Kiongozi wa anayestahili kuvaa viatu vya
Askofu Kulola ni lazima akidhi malengo ya kikatiba ambayo ni kuhubiri Injili ya
Yesu Kristo.
Pili; awe mtu atakayeliinua
kanisa la EAGT na kuliletea maendeleo ya kiroho na kimwili, badala ya
kujinufaisha yeye mwenyewe.
Tatu, awe mtu anayejitolea kuongoza wengine kwa vitendo akijitolea mapato yake
kuwasaidia wenzake, sio mtawala ni Kiongozi.
Akasisitiza kuwa Askofu Kulola kamwe hakuwa mtawala bali alikuwa Kiongozi wa
watu.
Sifa ya nne; alisema kuwa
ni lazima mtu huyo awe ni yule anayeweza kueneza Injili na kuliinua kanisa la
EAGT mbele ya jamii kwa njia ya habari, kwani hiyo ndiyo inayoweza kuwafikia
mamilioni ya watu kwa dakika chache tu, badala ya watu kujilimbikizia fedha,
wakati watu wanakufa dhambini.
Kiongozi huyo mkongwe
katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake, Temeke, mkabala na Uwanja
wa Taifa, jijini Dar es Salaam, alisema kuwa hitaji la Injili kupitia vyombo
vya habari ni muhimu sana wakati huu ili kukabiliana na wimbi la Imani potofu
ambazo zinaenezwa kwa njia hiyo hiyo ya habari, hivyo kanisa ni lazima litumie
vyombo hivyo kupeleka Injili iliyo sahihi.
Akitoa mfano alisema;
Askofu Sylvester Gamanywa (WAPO MISSINON INTERNATIONAL) alifanya mkutano Mbeya
na kuwafikishia habari mamiloni ya watu kwa muda mfupi sana kupitia vyombo vya
habari na hiyo ndiyo Injili ya sasa.
Alipoulizwa nini mtazamo
wake kuelekea uchaguzi, mwenyekiti huyo wa bodi ya wadhamini (chombo chenye
dhamana ya mali za kanisa) alisema:
“Inaweza kuwashangaza watu
sana kwani Mungu atajitwalia Joshua wa kuliongoza kanisa, anaweza kutoka katika
kundi lisilotegemewa, kutoka watu wa chini tu ambaye amejitoa na anaonekana
kujitolea kulitumikia kusudi la Injili na kuwajali wenzake.”
Alisema Mungu anakanuni
zake, hanaangalii vigezo vya wanadamu kama elimu na mambo mengine, Yeye
hulitazama kusudio lake, alimuita Petro akiwa mvuvi tu na akawa mtumishi wa
Injili.
Alinukuu andiko la Biblia
kwenye kitabu cha Matendo ya mitume 4:13; “Basi walipoona ujasiri wa Petro na
Yohana, na kujua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa wakastaajabu,
wakatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.”
“Kanisa la EAGT, linahitaji
Kiongozi mwenye kuwa na Yesu, kama alivyokuwa Askofu Kulola,”alisema kiongozi
huyo wa kiroho na kufafanua kuwa Kiongozi hupimwa kwa matendo yake. Kiongozi
wetu tunayemtaka ni lazima awe mtu wa kuwarehemu wachungaji wa chini,
awakumbatie na kuwasaidia, si kuwaswaga, huku akijilimbikizia mali tena
zinazotokana na kanisa la EAGT.
“Wewe si umekuja kwangu,
umeona maisha yangu, kanisa langu lipo pale Keko Juu katika ukumbi wa shule,
Mungu akinisaidi nikipata kiwanja kingine nitafurahi kanisa likiwa tofauti na
ukumbi ule nilioutoa kwa ajili ya ibada bure miaka yote.”
“Mimi nimekuwa mdhamini wa
kanisa tangu lilipoanza 1991, vijana wengi tumewapokea wakiwa hawana kitu,
lakini leo ni matajiri wakutupwa, wakati kanisa halina maendeleo kama taasisi.
Mimi ni mzee na kama wanasema mvi ni hekima basi wasikie wana-EAGT.”
Alisema kuwa uchaguzi wa
sasa ni wa tofauti kwa kuwa kwa mara ya kwanza kanisa linafanya uchaguzi bila
ya kuwepo kwa mwanzilishi wake, tangu lilipoanzishwa mwaka 1991.