Waziri mkuu mstaafu mheshimiwa Edward Ngoyaine Lowasa
anatarajiwa kuwa mgeni maalum katika tamasha la wezesha Upendo redio
linalolenga kukusanya pesa za kitanzania zaidi ya milioni 220 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kuboreshea na kuongeza usikivu wa
matangazo ya redio hiyo litakalofanyika Mei 27 mwaka huu katika
ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
Akizungumzia juu ya tamasha hilo msaidizi wa askofu wa
dayosisi ya mashariki na Pwani (DMP) wa
kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) mchungaji George Fupe
amesema kanisa hilo limemtumia mwaliko mheshimiwa Lowasa kuwa mgeni maalum
katika tamasha hilo kwani yeye ni mmoja wa washarika wa kanisa hilo.
Aidha mchungaji Fupe alisema tayari wameshawatumia baadhi ya
mawaziri,wabunge,wafanyabiashara,watu mashuhuri na viongozi mbalimbali wa
serikali pamoja na wakuu wa dini na madhehebu mbalimbali waweze kushiriki
baraka hizo.
"Tunawakaribisha si kwa sababu wamekuwa na nyasfa
kubwa serikalini bali tumeangalia unyenyekevu wao kwa Mungu na kwa
jamii"alisema mchungaji Fupe.
Aliongeza kuwa kwa taratibu za KKKT askofu wa dayosisi
hiyo na ambaye pia ni askofu mkuu wa kanisa hilo
hapa nchini Dr Alex Malasusa ndiye atakuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo.
Alisema kuwa licha ya upendo redio kumilikiwa na
kanisa hilo na hata kurusha vipindi vya dini pia imekuwa ikitangaza vipindi
vingi vya kijamii kama vile vya ujasiriamali,wanawake na matumaini,
walemavu,vijana,watoto,wazee,upendo mseto na hali halisi ambavyo vimekuwa
msaada kwa jamii.
Tamasha hilo la aina yake litapambwa na vikundi
mbalimbali vya kwaya pamoja na waimbaji
binafsi wa ndani na nje ya nchi
kama vile Faraja Ntaboba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na
Sara Kimani kutoka nchini Kenya.
Wengine ni Jackson bent kutoka jijini Arusha,Jennifa Mgendi kutoka jijini Dar es salaam na kwaya
mbalimbali za KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP).
Upendo redio Fm inayosikika katika masafa
ya FM 107.7 Mhz ilianzishwa mwaka 2004 ikiwa chini ya DMP na inasikika mikoa
saba hapa nchini ambayo ni Dar es salaam,Pwani,Morogoro,Tanga,Zanzibar na
baadhi ya sehemu za mkoa wa Kilimanjaro lengo lake ni kutaka isikie ndani na
nje ya nje.