YESU NI JIBU

Jumamosi, 3 Septemba 2022

INTERNEWS YATAKA USAWA KIJINSIA VYOMBO VYA HABARI

 

Ofisa Mipango Mwandamizi wa Internews, Victoria Rowan akito mada katika mafunzo kwa wanadishi wa habari kuhusu usawa wa kijinsia.

NA MWANDISHI WETU

MHADHIRI Msaidizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) Zuhura Selemani, amesema vyombo vingi vya habari vinaandika na kutangaza habari zinazowahusu wanaume kuliko wanawake jambo ambalo si sawa.

Katika mada yake kwa wanahabari katika mafunzo ya siku moja kuhusu usawa wa kijinsia hususan katika siasa na uongozi pamoja na nafasi ya wanwake katika vyombo vya habari, Zuhura amenukuu utafiti uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) mwaka 2019, akisema ingawa wanawake wengi huhitimu katika vyuo na vyuo vikuu vya uandishi wa habari kuliko wanaume, bado idadi ya wandishi wa habari wanawake katika vyombo vya habari na taasisi nyingine ni ndogo kuliko wanaume.

“Vyombo vingi vya habari pia havina sera kuhusu masuala ya jinsia na vingi kati ya vilivyo na sera hizo, havizitumii,” alisema.

Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na taasisi ya Internews kupitia mradi wa Boresha Habari, Msimamizi wa Vyombo vya Habari wa Internews, Alakok Mayombo, alisema vyombo vya habari vinapaswa kuonesha mfano bora kwa kuandika na kutangaza habari kwa kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kupaza sauti za watu walio katika makundi maalumu wakiwamo wanawake na wenye ulemavu.

Alisema ukosefu wa usawa wa kijinsia bado ni tatizo kubwa katika jamii katika nyanja mbalimbali zikiwamo za siasa, uwakilishi na uongozi sambamba na nafasi katika vyombo vya habari.

“Bado tatizo hili ni kubwa hivyo, lazima wanawake na wanaume washirikiane kuliondoa maana tunataka wote wasonge mbele hata katika shughuli zenye changamoto ili wapate uzoefu na nafasi ya kupanda juu hata katika vyombo vya habari hivyo, lazima hata wanaume waelimishwe na kushirikishwa katika juhudi hizi ili washiriki kuleta mabadiliko badala ya kuwa watazamaji,” alisema Alakok.

Mtaalamu huyo wa habari alisema lengo la kufikia uwiano wa 50 kwa 50 halipaswi kuwa katika siasa pekee, bali pia katika taaluma mbalimbali ikiwamo ya habari kwa kutoa nafasi sawa kwa wanawake na wanaume.

“Sauti za wanawake zisikike na pia, ni vema zioneshe mafanikio na uwezo wao badala ya wanawake kuoneshwa tu kwa matukio mabaya kama ya kubakwa na kupigwa,” alisema.

Katika mada yake iliyosisitiza tofauti baina ya jinsi na jinsia, Ofisa Mipango Mwandamizi wa Internews, Victoria Rowan, alisema ili kufikia usawa wa kijinsia, lazima wanawake na watu wenye ulemavu wapewe nyenzo na kusaidiwa kwa hali na mali ili kufikia uwiano.

“Si tu suala la wote kupata kwa usawa, bali walio pembezoni wapewe nguvu zaidi ili wafikie wenzao katika nyanja mbalimbali kama siasa, uongozi na kiuchumi kwa kuwa hakuna anayezaliwa akiwa kiongozi, bali wote huandaliwa,” alisema Rowan.

Alisema wanawake hawana budi kujengewa uwezo wa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ukiwamo wa kisiasa huku kukiwa na mazingira wezeshi kama usalama, elimu na nguvu za kiuchumi.

Aliwataka wanawake kutojiweka nyuma zinapotokea fursa mbalimbali, bali wajitokeze na kuzichangamkia.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali inayobadilisha maisha ya wanawake vijana na watoto (TIBA), Marcela Lungu, alisema elimu sahihi na endelevu inapaswa kutolewa kwa jamii  ili kufikia usawa wa kijinsia.

Marcela alisema, “Vyombo vya habari vioneshe nguvu ya wanawake katika jamii ili jamii iwaone na kuwapa nafasi maana wapo wanawake wengi wenye uwezo mkubwa wa uongozi, lakini hawapati nafasi.

Akaongeza, “Tatizo hili linachangiwa pia na mtazamo hasi wa jamii, baadhi ya mila na desturi na baadhi yao wenyewe kutojiamini.”

Akijikita katika nadharia za uongozi katika mtazamo wa jinsia, mtaalamu wa masuala ya jinsia na maendeleo, Michael Marwa, alisema kitendo cha wanawake kujifunza majukumu yao mengi wakiwa katika umri mdogo, huathiri mitazamo yao na uchaguzi wa shughuli zao za kimaisha.

“Hili ndilo husababisha mtazamo kuwa jamii au kundi fulani ni viongozi bora kuliko wengine katika jamii jambo ambalo si kweli,” alisema.

Marwa ambaye pia ni Mkuu wa Mipango katika taasisi ya C-SEMA mkoani Dar es Salaam, alisema ukosefu wa uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika uongozi si matokeo ya kinachodaiwa na baadhi ya watu kuwa uwezo mdogo au wanawake kutojiamini, bali imani potofu kuwa wanawake hawawezi kuwa viongozi bora.

“Jamii inapaswa kubadili mitazamo yao na kuweka usawa baina ya wanawake na wanaume,” alisema Marwa.

Ijumaa, 19 Agosti 2022

Samia kupamba Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA

Na Alexander Joseph

RAIS Samia Suluhu Hassana anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya WanawakeWakatoliki Tanzania (WAWATA) yatakayofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Septemba 11, mwaka huu,

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa WAWATA kitaifa, Eveline Ntenga, mbele ya vyombo vya habari katika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ilisema tukio hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na watu 60,000 wakiwamo maaskofu, Bodi ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO), wajumbe wa bodi kutoka nchi za Afrika, Umoja wa Makanisa ya Kikristo (UWAMAKDA), Spika Mstaafu wa Bunge, Anne Makinda na Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika, Getrude Mongella. 

TAMKO RASMI LA WAWATA TAIFA HILI HAPA

 

NURU YETU IANGAZE, ILI TUTAKATIFUZE MALIMWENGU

 Tumsifu Yesu Kristo…

Ndugu waandishi wa habari,

Leo hii tumekutana nanyi ili kuelezea juu ya Maadhimisho ya Jubileo ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kitume cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) hapo Septemba 11 mwaka huu wa 2022.

Hiki ni chombo cha kuwaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu ikijishughulisha na shughuli zote za kuwaendeleza wanawake kiroho na kimwili ili kuwawezesha kutoa mchango wao kikamilifu kuliendeleza na kulistawisha Kanisa na jamii kwa ujumla katika nyanja za kiroho, matendo ya huruma na kiuchumi likiongozwa na Dhamira yake Kuu:  Kwa Upendo wa Kristo Tutumikie na Kuwajibika.

Licha ya WAWATA kuanzishwa rasmi mwaka huo wa 1972 baada ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuridhia katiba yake,  lakini pia chombo hiki ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO-World Union of Catholic Women Organization) iliyoanzishwa mwaka 1910 yenye makao yake makuu Ufaransa.

Tukio la Maadhimisho ya Jubilei hii ya Miaka 50 ya WAWATA, lilizinduliwa rasmi Uzinduzi wa Jubilei ulifanyika Julai 25 mwaka 2021 katika eneo la TEC, Kurasini, Dar es Salaam kwa kuongozwa na Kaulimbiu ya Jubilei isemayo  "Miaka 50 ya WAWATA: Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji, ambayo ndani yake imemeba ujumbe wa Kaulimbiu tatu ambazo ni pamoja na ile ya WAWATA yenyewe (Upendo…), kaulimbiu ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu wa Fratelli Tutti 2018) pamoja nay a Waraka wa Baba Mtakatifu ya UADILIFU WA UUMBAJI- Laudato Si.

Ndugu Waandishi,

Baada ya uzinduzi huo wa kuelekea kilele cha Jubilei tuliazimia kufanya mambo kadhaa ambayo ni pamoja na:

Ø  Kufanya uzinduzi ngazi za kanda, majimbo, parokia mpaka kwenye jumuiya

Ø  Kuendelea kutoe elimu ya kina juu ya utume wa  mwanamke Mkatoliki na wajibu wake katika malezi ya familia.

Ø  Kampeni ya kusafisha mazingira na kupanda miti isiyopungua 34,000  ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa Baba Mtakatifu wa Laudato Si (Sifa kwako Ee Mungu) – (Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote)

Ø  Kuwafikia wahitaji na wale waliosukumizwa pembezoni (yaani kuwa sauti ya wasio na sauti) bila kujali imani zao tukitambua sote ni viumbe wa Mwenyezi Mungu.

Ø  Kutoa elimu kwa vijana ama WAWATA chipukizi kwa mpango wa Mafunzo ya Wakufunzi (TOT - Training of Trainers) bila kuwasahau VIWAWA  (Vijana wa Kiume)  na tumefanya hivyo ili kuyaishi kwa matendo Maandiko Matakatifu (Mithali 31 Maneno Ya Mfalme Lemueli juu ya mafundo aliyopewa na mama yake na 1Timotheo 1:5 tunapata Habari za Eunike na Lois waliomfundisha Timotheo Imani.

Ø  Kuendeleza na kufufua miradi mbalimbali iliyopo majimboni ili kutoa ajira kwa mama aweze kuchangia pato la familia na kutegemeza Kanisa mahalia na kuchangia pato la Taifa  ambapo hadi sasa tuna vikundi mbalimbali vikiwemo vya vya SILC na SACCOS

Ø  Elimu kwa Watoto wetu juu ya tunu Msingi za Maisha ili kuwezesha watoto  kutambua kuwa wanategemeana na watambue upendo binafsi (wajipende), upendo kwa Mungu – Upendo kwa mama Ardhi – Laudato Si.

Baada ya kuhitimisha kilele cha jubilee ngazi za Parokia, Majimbo na Kanda sasa tunaingia hatua ya kilele cha kuhitimisha Jubilei hii Kitaifa (WAWATA Taifa) tukio linalotarajiwa kufanyika Septemba 11 mwaka huu wa 2022 katika viwanja vya Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.

Tukio hili pia linatarajiwa kuhudhuriwa takribani watu 60,000 wakiwemo wakiwamo maaskofu, Bodi ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO), wajumbe wa bodi kutoka nchi za Afrika, Umoja wa Makanisa ya Kikristo (UWAMAKDA), Spika Mstaafu wa Bunge, Anne Makinda na Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika, Getrude Mongella na WAWATA kuanzia ngazi zote yaani  Jumuiya Ndogondogo za Kikiristu, Vigango, Parokia, Dekania, Jimbo hadi Taifa kama ulivyo muundo wa Kanisa Katoliki Tanzania kwa kuzingatia kwamba  kila mwanamke Mkatoliki ni mwanachama wa WAWATA kwa ubatizo wake.

Napenda kutumia fursa hii kuwaalika waamini wooooooote tujongee Uwanja wa Taifa hapo 11/09/2022 katika Misa Takatifu itakayoanza 4:00 asubuhi (saa nne kamili asubuhi na Askofu Mkuu Jude Thadeus Ruwaichi (OFM Cap), wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Mbali na waamini, pia tunawaalika watu wenye mapenzi mema kujumuika nasi pia kwenye matukio mengine yatakayofanyika baadaya ya Misa ambapo pia kitazinduliwa Kitabu cha historia ya WAWATA, kutakuwa na maonyesho ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha na WAWATA kutokana na miradi yao, burudani mbalimbali, tunategemea pia kuzindua kitabu cha historia yetu.

Karubuni sana mjumuike nasi wana WAWATA ili :-

Ø  Shukrani kwa Mungu

Ø  Kufanya toba kwa yale ambayo hatukufanya sawasawa

Ø  Kuomba neema ya kusonga mbele

Kwa Upendo wa Kristo….. Tutumikie na Kuwajibika.

Evaline Malisa Ntenga.

Mwenyekiti WAWATA Taifa.

 

 

Jumatano, 9 Machi 2022

RAIS SAMIA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZA NA MKURUGENZI WA UN WOMEN DK.MAXIME HOUINATO IKULU TUNGUU ZANZIBAR

    

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi wa UN Women Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini Dkt. Maxime Houinato alipofika Ikulu Tunguu Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa UN Women Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini Dkt. Maxime Houinato na Ujumbe wake mara baada ya kumalizika mazungumzo yao Ikulu Tunguu Zanzibar

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mke wa aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mama Fatma Karume alipomtembelea kumjulia hali nyumbani kwake Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar Dkt. Abdallah Sadala Mabodi na Familia yake, alipomtembelea nyumbani kwake Chukwani Mkoa wa Mjini Magharibi  Unguja leo tarehe 09 Machi, 2022 kwa ajili ya kumfariji kutokana na kupotelewa na Mtoto wake  kwenye ajali ya Ndege.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar Dkt. Abdallah Sadala Mabodi na Familia yake, alipomtembelea nyumbani kwake Chukwani Mkoa wa Mjini Magharibi  Unguja leo tarehe 09 Machi, 2022 kwa ajili ya kumfariji kutokana na kupotelewa na Mtoto wake  kwenye ajali ya Ndege.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Familia ya Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Ahmed Nassor Mazrui alipowatembelea nyumbani kwao Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi  Unguja leo tarehe 09 Machi, 2022 kwa ajili ya kuwafariji kutokana na kupotelewa na Mtoto wao  kwenye ajali ya Ndege.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Familia ya Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Ahmed Nassor Mazrui alipowatembelea nyumbani kwao Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi  Unguja leo tarehe 09 Machi, 2022 kwa ajili ya kuwafariji kutokana na kupotelewa na Mtoto wao  kwenye ajali ya Ndege.

Jumanne, 8 Machi 2022

MKEMIA MKUU AHIMIZA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI.

 


Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amewahimiza wajasiriamali kuzingatia matumizi salama ya kemikali wanazotumia katika uzalishaji wa bidhaa zao ili kulinda afya za binadamu na mazingira.

Dkt. Mafumiko ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea maonesho ya wanawake wajasiriamali yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ambayo yanafanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.

Aliwaeleza wajasiriamali hao kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) katika utekelezaji wa majukumu yake imekuwa ikitoa mafunzo kuhusu matumizi salama ya kemikali kwa wadau wake mbalimbali wanaotumia kemikali wakiwemo wajasiriamali ili kuwapa elimu ya matumizi salama ya kemikali pamoja na namna bora ya kuhifadhi bidhaa zao.

“Kwa nafasi yetu kama wasimamizi wa sheria ya kemikali tuna jukumu la kuhakikisha watumiaji wa kemikali kama vile watengeneza batiki na wanaosindika bidhaa za vyakula pamoja na dawa asili wanazingatia taratibu za kiusalama, hivyo tunawaahidi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wadau hao,” alisisitiza Dkt. Mafumiko.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TWCC, Mercy Sila alisema kuwa katika zoezi la kuwafikia wajasiriamali, taasisi yake inapata ushirikiano mzuri kutoka GCLA kwenye kuwaelimisha wajasiriamali hao namna bora na salama ya kutumia kemikali katika uzalishaji wa bidhaa.

Aidha, baadhi ya wajasiriamali waliowahi kupata mafunzo ya matumizi salama ya kemikali kutoka GCLA walieleza kuwa elimu waliyoipata imewasaidia kuboresha bidhaa zao na kulinda afya zao bila kuchafua mazingira.

Naye mjasiriamali kutoka Zanzibar, Salma Othman ameiomba GCLA iendelee kutoa elimu kwa wadau wengi zaidi kupitia njia mbalimbali ili kuhakikisha jamii ya Watanzania inazingatia usalama wa afya za watu na mazingira.

Maonesho hayo ya pili ya wajasiriamali wanawake yaliyoandaliwa na TWCC yalianza Machi 3 mwaka huu na yanatarajiwa kukamilika Machi 8, 2022 ambayo ni Siku ya Wanawake Duniani.



MKAKATI WA MKOA WA DAR ES SALAAM NI KUONGEZA MAPATO BAJETI 2022/23

 


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla leo ameongoza kikao Cha Kamati ya ushauri ya Mkoa RCC kuhusu mapendekezo ya bajeti ya Mkoa huo kwa Mwaka wa fedha 2022-2023 ambapo Mkoa huo umeomba kupatiwa kiasi Cha Shilingi bilioni 650.97 kwaajili ya utekelezaji wa Shughuli mbalimbali ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 88.7 kwa Mwaka 2021/2022.


Akizungumza wakati wa kikao hicho, RC Makalla amesema kiasi hicho kinajumuisha Mishaha Shilingi Bilioni 338.2, Miradi ya maendeleo Shilingi Bilioni 77.7 na Matumizi mengine kiasi Cha Shilingi bilioni 10.8 ambapo upande wa makusanyo Mkoa umelenga kukusanya Shilingi Bilioni 224.

Aidha RC Makalla amesema miongoni mwa vipaombele vitakavyozingatiwa ni pamoja na kudumisha amani, ulinzi na usalama,  Ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kuboresha Elimu, Afya, Mazingira Bora ya Biashara, miradi ya kimkakati, ustawi wa jamii, kudhibiti na Kupunguza Majanga.

Ili kuhakikisha Serikali inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, RC Makalla ametoa wito kwa Halmashauri kuhakikisha zinasimamia kikamilifu *makusanyo ya mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato.

Kikao hicho pia kwa kauli moja kimeazimia kumpongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jijini humo pamoja na kutoa fedha kwa wakati jambo linalosababisha miradi kutekelezeka kwa wakati pasipo usumbufu wowote.