Katika toleo lililopita tulianza mada mpya ya
“ukiheshimiwa heshimika” ambapo tulichambua maeneo matatu yaliyojumuisha “Utangulizi”;
“Vyanzo vya heshima”; na “Tishio la kujivunjia heshima baada ya kuheshimiwa”!
Leo tutaingia katika sehemu muhimu ya sababu kubwa ya kibibilia ambayo husababisha
wengi wanaofanikiwa na kuheshimiwa hupoteza heshima zao katika jamii:
Mtazamo wa Yesu kuhusu kujikinai
na kuacha kuheshimika
Bwana Yesu aliwahi kuongelea tatizo la hali ya kujikinai baada ya
kufanikiwa kiasi cha kudhani mafanikio ni “kibali cha kuishi milele duniani”! Katika
kuweka mkazo kuhusu tabia hii, Yesu alitoa mfano wa mtu mmoja tajiri
aliyeonesha kujikinai kwa utajiri wake na kutamba kuishi duniani bila ukomo:
“Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo
katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema,
Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni
mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.
Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa
zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha,
nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka
mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia,
Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea
tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba,
asijitajirishe kwa Mungu. “ (LK. 12:15-21)
Kwa kupitia maandiko haya, unaweza kusoma baadhi ya kauli za tajiri jinsi
alivyojikinai akisema: “….ee nafsi yangu,
una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule,
unywe, ufurahi…” Kumbuka kwamba huyu tajiri hakuupata utajiri wake kwa njia
za ufisadi. Aliupata kwa njia halali kabisaaaa. Alilima shamba lake “likazaa sana…”
Aidha, mpango wa kujenga ghala za kuhifadhi mali zake haukuwa jambo baya
hata kidogo! Tatizo lake lilikuwa ni kujikinai, na kujisahau, kwa kufikiri
kwamba alifikia kilele cha mafanikio hayo kwa nguvu zake binafsi na kwamba uhai
wake utalindwa na wingi wa mali zake!
Ni upumbavu kuacha nyuma mali nyingi
uondokapo badala ya kuzitanguliza uendako
Kutokana na maneno ya Yesu, inaonesha kwamba tabia ya kukusanya na
kijilimbikizia mali nyingi kisha ukaondoka na kuziacha bila kuzifaidi ni
“Upumbavu”! Kwa mujibu wa maneno ya Yesu ni kwamba upumbavu huu hauishii katika
kujilimbikizia peke yake, bali kushindwa kuzitumia mali kwenye mambo ya ufalme
wa Mungu; na matokeo yake mhusika kuondoka duniani ghafla na mali zake
kuchukuliwa na wengine wasiozitaabikia tangu mwanzo:
“….Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu
ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye
nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu..”
Uchunguzi wangu wa kimaandiko katika mada hii, nimebaini kwamba,
kujikinai sio kujisifia utajiri peke yake, wala sio kumsahau Mungu peke yake,
bali ni matumizi ya utajiri wenyewe ambayo Yesu amesema kwamba “….ndivyo
alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”
Mambo mawili muhimu hapa. Kwanza, ni tatizo la kujilimbikizia akiba
isiyo na matumizi bali imekaa tu kwenye hifadhi yake. Pili, kukataa kutumia
akiba ya mali katika vipaumbele vya Mwenyezi Mungu alivyoamuru kwa wale
wanaomiliki mali nyingi!
Yesu aliposema “kujitajirisha kwa Mungu” maana yake halisi kwa tafsiri
ya toleo la Biblia ya Kiingereza cha Amplified
limesema: “So it is with the one who
continues to lay up and hoard possessions for himself and is not rich his
relation to God…..” Haya maneno ya “…to lay up and hoard possessions…” yana
maana ya kukusanya na kujilimbikizia..”
Maana yake na ulimbikizaji ambao matumizi yake hayana mchango wa uhusiano na
huduma za kimungu.
Katika uchambuzi huu kuhusu mfano wa Yesu tunajifunza mambo muhimu
yafyatayo:
1. Tishio la mali kuchukuliwa na wengine
Mtazamo wa kujilimbikizia mali nyingi ili hatimaye ndipo mkusanyaji
apate kuzifaidi hapo baadaye si kitu kipya. Yupo mchaji Mungu aliyepata kuwa
tajiri sana kuliko wengi duniani, ambaye alifanya utafiti kuhusu hatma ya
utajiri ambapo alihitimisha kwa kusema hayo
nayo ni ubatili:
"Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya
jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata. Naye ni nani ajuaye
kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi
yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonyesha hekima
chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili."(MHU. 2:18, 19)
Kuna maneno haya “……kazi yangu
yote niliyojisughulisha nayo chini ya jua,…..” “……..sina budi kumwachia yeye atakayenifuata…….” “…… atatawala juu ya kazi yangu yote
niliyojishughulisha nayo…….” hayo
nayo ni ubatili.”
Aliyeandika haya ni mfalme Sulemani ambaye alijikusanyia mali na utajiri
mwingi kuliko matajiri wote wa ulimwengu waliowahi kuwepo kabla na baada yake. Ushahidi
mwingine wa utafiti wa Mhubiri unapatikana katika maandiko yafuatayo:
“Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa
ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni
ubatili, nayo ni baa kuu.” (MHU. 2:21)
Katika maandiko haya tunakutana na maneno haya.. “….Mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na maarifa, na kwa ustadi….”
“…….naye atamwachia mtu asiyeshughulika
nayo kuwa sehemu yake…”
Hili jambo lilimchanganya sana Sulemani. Mtu anakusanya mali nyingi kwa
muda mrefu na nguvu nyingi, akisha kufikia kilele cha ulimbikizaji kabla
hajazifaidi anaondoka ghafla, na mtu mwingine anazichukua bila kuzitaabikia!!
2. Kufananishwa na Mpumbavu
Yesu anamtaja tajiri Yule kuwa “Mpumbavu”! Ukifuatilia kwa makini
Bibilia inamtafsiri “mpumbavu” ni mtu yeyote asiyetambua uwepo wa Mungu:
“Mpumbavu amesema moyoni, hakuna Mungu; wameharibu matendo yao na
kuyafanya chukizo, hakuna atendaye mema.” (Zab.14:1)
Hivi ndivyo Yule tajiri mkulima alivyoonnesha upumbavu wake ambapo Yesu
aliutafsiri kwamba ni “dhana potofu ya uzima wa mtu kuwa katika wingi wa vitu
vyake alivyo navyo..”
3. Jinsi ya kuweka akiba yenye tija ya
milele
Haya basi, baada ya kuuthibitisha hasara ya kujilimbikizia mali na kisha
kufa ukaziacha na kuondoka patupu, Yesu alipendekeza njia ya kunufaika na mali
za duniani hata baada ya kuondoka duniani ni kuhakikisha matumizi ya mali hizo
yanatoa kipaumbele kwa mambo ya ufalme wa Mbinguni:
“Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi hujunja na
kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu,
wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo
utakapokuwapo na moyo wako.” (Mat.6:19-21)
Katika maandiko haya, ukiyatafsiri kwa mtazamo wa mfano wa tajiri
aliyejilimbikizia mali kibinafsi, utagundua maana kama ifuatavyo: Kwanza,
kukusanya mali na kuzitumia kwenye mambo ya ufalme wa Mungu ndiyo njia pekee ya
kulimbikiza mali mahali salama kwa maana kwamba mali zinakutangulia uendako
badala ya kuziacha nyuma yako uondokapo.
Majumuisho kuhusu kujikinai na kupoteza
heshima
Watu wengi hutumia nguvu na muda mwingi katika kutafuta mafanikio kwa
njia mbali mbali. Baada ya kufikia mafanikio na wahusika kupata kutambuliwa, na
kupata umaarufu na heshima kutokana na mafanikio waliyoyapata, ghafla
hubadilika kitabia na kupotesha heshima ile ile waliyokuwa wameipata kutokana
na kazi kubwa waliyokwisha kuifanya.
Moja wapo ya tabia mbaya inayopoteza heshima ni kujikinai na kudhani
kwamba, mafanikio hayo ni juhudi binafsi na Mungu hana sehemu wala jamii
inayowazunguka. Kimsingi hakuna mtu afanikiwaye yeye peke yake kwa juhudu zake
binafsi, pasipo ridhaa ya Mungu, na pasipo mikono ya watu wengine kuhusika kwa
njia moja au nyingine. Hata kama maono, mipango na mikakati ya utekelezaji
imebuniwa na mtu mmoja; bado ufanisi wake lazima hujumuisha wengi hata kama
waliohusika walifanya hivyo kwa malipo.
Aidha, ni upumbavu wa hali ya juu, pale ambapo mtu afikiapo mafanikio ya
kiuchumi, kufikiri kwamba ataishi milele duniani ili kunufaika kibinafsi na
utajiri aliojilimbikizia hapa duniani. Tunao ushahidi wa maelfu ya watu wengi
ambao kwa muda fulani walifanikiwa katika kumiliki uchumi na kupata umaarufu
lakinii ghafla wahusika wakatoweka ghafla kwa maradhi yaliyooshindikana
kutibika japokuwa walikuwa na mali nyingi. Mali zile hazikuwasaidia kudhibiti
na kurefusha maisha yao, wakaondoka pasipo kutaka.
Kana kwamba hii haitoshi, watu wengi waliojilimbikizia mali nyingi,
wanapoondoka ghafla haichukui muda mrefu hata na mali zile walizohifadhi
huangukia mikononi mwa watumiaji wasio na uchungu nazo, na kisha kutoweka na
kubaki historia tu.
Matokeo haya, ya kujikinai na kuishia kupoteza heshima ni changamoto kwa
jamii ya kizazi cha wanaofanikiwa katika karne hii ya ishirini na moja. Katika
toleo lijalo tutapitia kwa kina matumizi mabaya ya mali na utajiri na athari
zake kwa wahusika pamoja na jamii kwa jumla.
Itaendelea toleo lijalo,