YESU NI JIBU

Ijumaa, 19 Agosti 2022

Samia kupamba Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA

Na Alexander Joseph

RAIS Samia Suluhu Hassana anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya WanawakeWakatoliki Tanzania (WAWATA) yatakayofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Septemba 11, mwaka huu,

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa WAWATA kitaifa, Eveline Ntenga, mbele ya vyombo vya habari katika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ilisema tukio hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na watu 60,000 wakiwamo maaskofu, Bodi ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO), wajumbe wa bodi kutoka nchi za Afrika, Umoja wa Makanisa ya Kikristo (UWAMAKDA), Spika Mstaafu wa Bunge, Anne Makinda na Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika, Getrude Mongella. 

TAMKO RASMI LA WAWATA TAIFA HILI HAPA

 

NURU YETU IANGAZE, ILI TUTAKATIFUZE MALIMWENGU

 Tumsifu Yesu Kristo…

Ndugu waandishi wa habari,

Leo hii tumekutana nanyi ili kuelezea juu ya Maadhimisho ya Jubileo ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kitume cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) hapo Septemba 11 mwaka huu wa 2022.

Hiki ni chombo cha kuwaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu ikijishughulisha na shughuli zote za kuwaendeleza wanawake kiroho na kimwili ili kuwawezesha kutoa mchango wao kikamilifu kuliendeleza na kulistawisha Kanisa na jamii kwa ujumla katika nyanja za kiroho, matendo ya huruma na kiuchumi likiongozwa na Dhamira yake Kuu:  Kwa Upendo wa Kristo Tutumikie na Kuwajibika.

Licha ya WAWATA kuanzishwa rasmi mwaka huo wa 1972 baada ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuridhia katiba yake,  lakini pia chombo hiki ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO-World Union of Catholic Women Organization) iliyoanzishwa mwaka 1910 yenye makao yake makuu Ufaransa.

Tukio la Maadhimisho ya Jubilei hii ya Miaka 50 ya WAWATA, lilizinduliwa rasmi Uzinduzi wa Jubilei ulifanyika Julai 25 mwaka 2021 katika eneo la TEC, Kurasini, Dar es Salaam kwa kuongozwa na Kaulimbiu ya Jubilei isemayo  "Miaka 50 ya WAWATA: Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji, ambayo ndani yake imemeba ujumbe wa Kaulimbiu tatu ambazo ni pamoja na ile ya WAWATA yenyewe (Upendo…), kaulimbiu ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu wa Fratelli Tutti 2018) pamoja nay a Waraka wa Baba Mtakatifu ya UADILIFU WA UUMBAJI- Laudato Si.

Ndugu Waandishi,

Baada ya uzinduzi huo wa kuelekea kilele cha Jubilei tuliazimia kufanya mambo kadhaa ambayo ni pamoja na:

Ø  Kufanya uzinduzi ngazi za kanda, majimbo, parokia mpaka kwenye jumuiya

Ø  Kuendelea kutoe elimu ya kina juu ya utume wa  mwanamke Mkatoliki na wajibu wake katika malezi ya familia.

Ø  Kampeni ya kusafisha mazingira na kupanda miti isiyopungua 34,000  ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa Baba Mtakatifu wa Laudato Si (Sifa kwako Ee Mungu) – (Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote)

Ø  Kuwafikia wahitaji na wale waliosukumizwa pembezoni (yaani kuwa sauti ya wasio na sauti) bila kujali imani zao tukitambua sote ni viumbe wa Mwenyezi Mungu.

Ø  Kutoa elimu kwa vijana ama WAWATA chipukizi kwa mpango wa Mafunzo ya Wakufunzi (TOT - Training of Trainers) bila kuwasahau VIWAWA  (Vijana wa Kiume)  na tumefanya hivyo ili kuyaishi kwa matendo Maandiko Matakatifu (Mithali 31 Maneno Ya Mfalme Lemueli juu ya mafundo aliyopewa na mama yake na 1Timotheo 1:5 tunapata Habari za Eunike na Lois waliomfundisha Timotheo Imani.

Ø  Kuendeleza na kufufua miradi mbalimbali iliyopo majimboni ili kutoa ajira kwa mama aweze kuchangia pato la familia na kutegemeza Kanisa mahalia na kuchangia pato la Taifa  ambapo hadi sasa tuna vikundi mbalimbali vikiwemo vya vya SILC na SACCOS

Ø  Elimu kwa Watoto wetu juu ya tunu Msingi za Maisha ili kuwezesha watoto  kutambua kuwa wanategemeana na watambue upendo binafsi (wajipende), upendo kwa Mungu – Upendo kwa mama Ardhi – Laudato Si.

Baada ya kuhitimisha kilele cha jubilee ngazi za Parokia, Majimbo na Kanda sasa tunaingia hatua ya kilele cha kuhitimisha Jubilei hii Kitaifa (WAWATA Taifa) tukio linalotarajiwa kufanyika Septemba 11 mwaka huu wa 2022 katika viwanja vya Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.

Tukio hili pia linatarajiwa kuhudhuriwa takribani watu 60,000 wakiwemo wakiwamo maaskofu, Bodi ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO), wajumbe wa bodi kutoka nchi za Afrika, Umoja wa Makanisa ya Kikristo (UWAMAKDA), Spika Mstaafu wa Bunge, Anne Makinda na Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika, Getrude Mongella na WAWATA kuanzia ngazi zote yaani  Jumuiya Ndogondogo za Kikiristu, Vigango, Parokia, Dekania, Jimbo hadi Taifa kama ulivyo muundo wa Kanisa Katoliki Tanzania kwa kuzingatia kwamba  kila mwanamke Mkatoliki ni mwanachama wa WAWATA kwa ubatizo wake.

Napenda kutumia fursa hii kuwaalika waamini wooooooote tujongee Uwanja wa Taifa hapo 11/09/2022 katika Misa Takatifu itakayoanza 4:00 asubuhi (saa nne kamili asubuhi na Askofu Mkuu Jude Thadeus Ruwaichi (OFM Cap), wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Mbali na waamini, pia tunawaalika watu wenye mapenzi mema kujumuika nasi pia kwenye matukio mengine yatakayofanyika baadaya ya Misa ambapo pia kitazinduliwa Kitabu cha historia ya WAWATA, kutakuwa na maonyesho ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha na WAWATA kutokana na miradi yao, burudani mbalimbali, tunategemea pia kuzindua kitabu cha historia yetu.

Karubuni sana mjumuike nasi wana WAWATA ili :-

Ø  Shukrani kwa Mungu

Ø  Kufanya toba kwa yale ambayo hatukufanya sawasawa

Ø  Kuomba neema ya kusonga mbele

Kwa Upendo wa Kristo….. Tutumikie na Kuwajibika.

Evaline Malisa Ntenga.

Mwenyekiti WAWATA Taifa.