MCHUNGAJI MTIKILA ASHINDA KESI, ASEMA YESU AMEMJIBU MAOMBI YAKE.
Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameshinda kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili.
Inadaiwa kuwa Oktoba 21 mwaka jana katika maeneo ya Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC), Ilala, jijini Dar es Salaam Mchungaji Mtikila alitoa
maneno ya uchochezi, dharau na kujenga chuki dhidi ya Serikali na Rais.
Akizungumza na mtandao wa Global Publishers baada ya kushinda kesi hiyo, Mtikila amesema “Ushindi huu niliutarajia maana hata asubuhi kabla ya kuja mahakamani niliongea na Yesu na sasa amenijibu”.
Mara baada ya kushinda kesi hiyo lilizuka timbwili lingine baada ya mtu
mmoja kujitokeza akiwa na RB (Report Book) akimtuhumu Mchungaji Mtikila
kuwa alimtishia kumuua na ni mwizi wa viwanja. Baada ya kutaka kukamatwa
na polisi mmoja aliyekuwa na cheo cha Koplo, Mchungaji alikataa kwa
madai kuwa yeye ni kiongozi wa kitaifa hivyo hawezi kukamatwa na polisi
mwenye cheo cha Koplo, labda polisi mwenye cheo cha SSP (Senior
Superintendent of Police). Kwa kauli hiyo polisi alishindwa kumtia
nguvuni.