YESU NI JIBU

Jumatatu, 4 Mei 2015

KANISA KUU KATOLIKI JIMBO LA DODOMA LAJIPANGA KULKABILIANA NA VITENDO VYA KIGAIDI KWA KUTUMIA KIFAA MAALUM CHA KUKAGULIA WAUMINI KABLA YA KUINGIA IBADANI.



Kutokana na kushamiri kwa matukio yenye viashiria vya kigaidi nchini, Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Dodoma limeanzisha utaratibu wa kukagua watu wote wanaoingia katika ibada kwa kutumia kifaa maalumu cha kugundua silaha au kifaa chochote hatarishi na vile vya mlipuko.
Aidha, wito umetolewa kwa waumini wa madhehebu ya Kikatoliki wanaohudhuria ibada zao kwenye Kanisa hilo, kuchukua tahadhari zote kukabiliana na suala la tishio la usalama kwa matukio ya kigaidi, yanayoweza kujitokeza kanisani hapo, kutokana na mkusanyiko mkubwa wa watu wanaohudhuria ibada siku za Jumapili.
Paroko wa Kanisa hilo, Padri Sebastian Mwaja alitoa wito huo jana wakati akiendesha ibada za kawaida za Jumapili.
Alisema kanisa hilo limeanzisha utaratibu wa kuwakagua watu wote wanaoingia katika ibada hizo kwa kutumia kifaa maalumu cha kugundua silaha au kifaa chochote hatarishi na vile vya mlipuko.
Padri Mwaja alisema idadi ya waumini imeongezeka ghafla hususani baada ya Jimbo la Dodoma kumpata na kumsimika rasmi Askofu Mkuu mpya wa Jimbo la Dodoma.
“Pia mji wetu kuwa na desturi ya kupokea wageni wengi wa kiserikali, ni wazi hatuwezi kujisahau na kuacha suala la usalama wa waumini wetu,” alisema paroko huyo.
Alitaja baadhi ya hatua zilizoanza kuchukuliwa kukabiliana na matishio ya vitendo vya kigaidi kuwa ni pamoja na kuundwa kwa kamati ya ulinzi ya kanisa hilo ijulikanayo kwa kifupi “KAUKA”, ambapo baadhi ya taratibu za awali tayari zimeshawekwa na kamati hiyo, ikiwamo tahadhari kwa waumini wote kuhakikisha anamtambua jirani yake aliyekaa naye kanisani, na kama atamtilia shaka yoyote, atoe taarifa mapema katika kamati hiyo.
Hatua nyingine iliyochukuliwa ni pamoja na kuhakikisha kila muumini anayeingia kanisani hapo anakaguliwa ndipo aingie ndani ya kanisa na pia magari yote pamoja na pikipiki kuachwa nje ya ua wa parokia hiyo katika eneo maalumu lililoandaliwa ili kudhibiti usalama.
Paroko huyo ametaja pia changamoto iliyojitokeza wakati wa kutekeleza ulinzi huo, ikiwemo upungufu wa vifaa vya ukaguzi ambapo hadi sasa kipo kifaa kimoja tu kinachotumika kwenye lango (geti) moja na mengine kubakia yamefungwa.
Alieleza kifaa hicho kina thamani ya Sh 750,000 na vinatakiwa takribani vinne ili vitumike kwa wakati mmoja wakati wa ibada za asubuhi.
Pia, ametoa wito kwa waumini wenye uwezo wa kutoa ufadhili wa vifaa hivyo kama ilivyofanyika kwa kilichopo sasa, kufanya hivyo mapema ili waumini wawe na uhakika wa usalama wao wanapokuwa katika ibada.
Pameonekana msururu mrefu wa waumini wanaotaka kuwahi kuingia katika ibada za asubuhi siku za Jumapili, lakini huchelewa kutokana na ukosefu wa vifaa vya kutosha.
Kwa upande mwingine, kampuni moja inayojihusisha na ukusanyaji wa kodi ya kuegesha magari hapa Dodoma, nayo inaonekana kufurahia mpango huo wa magari kutoingia ndani ya kanisa hilo, na wao kukusanya kodi zao za maegesho nyakati za asubuhi.
Waumini wengi wameonesha kuridhishwa na hatua hiyo ya kamati ya ulinzi, ikielezwa Dodoma iko hatarini zaidi kutokana ujio wa wageni wengi katika mji huo mkuu wa Tanzania, wakitolea mfano Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Aidha, kushikiliwa kwa mwanafunzi wa kitanzania anayetajwa kujihusisha na ugaidi katika Chuo Kikuu cha Garisa nchini Kenya kumeongeza hofu, kwani alikuwa akisoma shule ya sekondari Bihawana, nje kidogo ya mji huu.
Mbali na Dodoma, viashiria vya matukio ya kigaidi vimejitokeza katika mkoa jirani wa Morogoro, ambako bomu lililotupwa na kijana ambaye hajafahamika, limejeruhi vibaya watu watano. Tukio hilo la mwishoni mwa wiki lilitokea kijiji cha Msolwa kata ya Sanje wilaya ya Kilombero.
Na Sifa Lubasi,

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni