YESU NI JIBU

Jumatano, 20 Mei 2015

HALI NI MBAYA HUKO MKOANI IRINGA,POLISI WADAIWA KUUA MWANANCHI KWA RISASI.









Askari wa FFU Njombe wakifungua barabara kuu ya Njombe - Iringa iliyofungwa kwa kuchomwa mataili na waandamanaji



 Viongozi wa Chadema Njombe wakivutana na polisi eneo la Kibena 





Mmoja wa majeruhi ambaye amejeruhiwa katika vurugu za FFU na Raia.


ASKARI  wa kikosi cha  kutuliza  ghasia (FFU) Njombe  watumia mabomu ya machozi  kuwatawanya wananchi  waliotaka kuchukua mwili  wa mwenzao anayedaiwa kuuwawa na polisi  kuupeleka  kituo cha  polisi .
Wakizungumzia  mtandao huu wa www.matukiodaima.co.tz juu ya vurugu   hizo  baadhi ya  wananchi  walisema  kuwa  jana majira ya saa 3 usiku askari  wawili   wakiwa na slaha  walivamia  kilabu  cha  pombe  za kienyeji  kilichopo   eneo la Zenge mtaa wa Kambarage na  kuwakamata  wananchi wote  zaidi ya 20  waliokuwemo klabuni hapo na  kuwaweka  chini ya  ulinzi .

Hata   hivyo  baada ya  wananchi hoa  kukamatwa  wakiwemo  wahudumu  inadaiwa  polisi hao  wawili  waliovalia kininja kwa  kuziba sura  zao  walianza kuwapiga  raia  walioonyesha  kukaidi agizo la  kutaka kutoa pesa  walizonazo kama faini ya  kunywa  pombe   usiku huo.

Hivyo  kutokana na baadhi yao  kushindwa  kulipa adhabu hiyo akiwemo kijana mmoja aliyetambuliwa  jina la Bashir Mwalongo  ambae  ni  fundi  ujenzi  katika  mji  huo wa Njombe aliyekuwa  akitaka  kutoka mlangoni hapo ndipo  alipopigwa na  kitu  kinachosadikika kuwa ni  risasi  tumboni  na  kufa papo hapo

Mmoja kati ya  rai  waliokamatwa na askari  hao  kwa  kunywa  pombe  usiku  Bi Veronica Ng'ara  alisema  askari  hao  walifika  eneo hilo huku  marehemu huyo akiwa   mlangoni  kutoka  kutoka nje na ndipo alipozuiliwa na kulazimishwa kuingia ndani ya klabu hicho .

"Kabla  ya  kufyatuliwa  risasi  kijana  huyo  alikuwa  amesimama  mlangoni akitaka  kutoka  na ndipo  askari  mmoja kati ya  watatu  waliofika eneo hilo  kumpiga na risasi ..... hawa  watu  sisi hatujui kama ni askari ama majambazi kwani  walikuwa  wamejifunika usoni .... walipoona  raia  tunamsaidia aliyepitwa risasi ndipo  walipoanza  kufyatua risasi  ovyo na kuingia katika gari na kukimbia ....tulipiga  simu kwa mkuu wa  polisi usiku  huo na yeye alikataa kuwatuma askari  hao ambao  walikuja kutaka posho  usiku  huo "

Alisema askari  hao  walilazimika  kufyatua  risasi za  moto  ovyo  klabuni hapo  ili  kuokoa maisha yao baada ya  wananchi  kutaka  kuwazingira kwa kosa la  mauwaji .

 Kuwa  kutokana na vurugu   hizo jana usiku kwa  wananchi hao  kuupeleka  mwili  wamarehemu huyo Hospitali ya  wilaya ya  Njombe  pamoja na majeruhi mmoja asubuhi  ndipo  wananchi  walipoandamana kwenda  Hospitali hapo  kuchukua  mwili  huo ili  kuupeleka kituo  cha polisi .

Alisema wananchi  waligoma  kuzika mwili   huo na kutaka kuuchukua  ili  kuupeleka polisi ili  wao askari  waliooa ndio  wakauzike .

Majeruhi  Lupiana Mandera  ambae  amelazwa katika  Hospitali ya wilaya ya  Njombe  alisema  kuwa wakati   vurugu  hizo  zikiendelea nje ya  Hospitali ya  wilaya  ya  Njombe kwa polisi  wa FFU kutumia mabomu ya machozi  kuwatawanya  raia  zaidi ya 1000  walikuwa  wameziba barabara  kuu ya Njombe - Ruvuma kwa  kuchoma moto katikati ya barabara  ndipo askari  walipomvamia na  kumshambulia kwa  virungu .

Alisema  kuwa  kwa  upande wake  alikuwa akiwaonya  vijana  waliokuwa  wakichoma moto mataili barabarani  kuachana na zoezi  hilo ndipo  polisi  walipomvamia na  kumpiga katika kichwa  chake kabla ya  kumjeruhi  vibaya  kichwani na mkononi .

Mama  mdogo  wa marehemu   Mwalongo  anayedaiwa  kuuwawa kwa  kupigwa  risasi na polisi katika  klabu  cha  pombe   Bi  Regina Msemwa alisema  kuwa  alipigiwa  simu usiku  kujulishwa  juu ya tukio la  kifo cha mtoto  wake   huyo mdogo na asubuhi  alifuatwa na  kundi la  watu wakiwemo viongozi  wa vyama vya siasa kumtaka  kwenda kuchukua mwili Hospitali ya  Kibena  ili  kuupeleka kituo  cha  polisi.

Alisema kuwa kimsingi  yeye  alikuwa bado katika mazungumzo na ndugu mbali mbali waliopo nje ya Njombe  ili  kupanga taratibu  za mazishi ila alifika katika Hospitali  hiyo ya  Njombe  baada ya  kutakiwa na viongozi na  wananchi  kuungana  nao katika maandamano hayo.

Mwenyekiti  wa mtaa wa Kambarage Ally  Mhagama ( Chadema) ambae  alikuwepo katika  vurugu  hizo katika  Hospitali ya  wilaya ya Njombe alisema  kuwa  vurugu  hizo  zimeanzishwa na polisi  wenyewe  baada ya  kuzuia mwili  kutolewa kwenda  kupeleka polisi .

Kwani  alisema  wao   kama  viongozi  walitaka  majeruhi  mmoja ambae  alipigwa  risasa sehemu zake za siri  kutolewa  Hospitali hapo na kupelekwa Hospitali ya  Rufaa Mbeya ama  Iringa kwa ajili ya matibabu  ila hakuna kilichofanyika juu ya majeruhi  huyo ambae alipigwa   risasi  pamoja na Marehemu Mwalongo .

Hata hivyo  alisema  kuwa anashangazwa  na hatua ya polisi hao  kutumia nguvu kubwa  kuwakamata wanywaji wa  pombe na  kuwaacha waarifu .

Mhagama  alisema  kuwa wao kama  chama  wanapowapongeza  wananchi  waandamanaji ambao  walifika  kupinga  vitendo vya kionevu  vya  polisi na  hata  wananchi hao  kumchangia majeruhi   huyo .

HIvyo  alisema  wanachoomba  ili kumaliza  vurugu hizo ni polisi na  serikali  kumpeleka Hospitali  kubwa ya Rufaa majeruhi  hao pamoja na kuueleza  umma jinsi  ambavyo maiti  hiyo  itakavyozikwa .

Mwandishi wa habari hizi  alishuhudia polisi wa FFU wakilazimika  kuwatawanya  waandamanaji hao ambao walitaka  kuandamana kutoka Hospitali ya wilaya  kwenda  ofisi ya mkuu wa mkoa wa Njombe Dr Rehema Nchimbi  ili kufikisha malalamiko  yao kabla ya  kutawanywa kwa  mabomu .

Pia  shughuli  mbali mbali  zikiwemo za usafiri wa kutoka na  kuingia mjini Njombe kwa  wasafiri  wa mikoa ya Ruvuma  , Mbeya , Iringa na  Dar es Salaam  wakikama kwa  muda  huku magari yao yakipigwa mawe  na maduka  kufungwa kwa  zaidi ya masaa 3 baada ya  vurugu  kuhamia katikati ya mji  wa Njombe .
Barabara  kuu ya Njombe - Ruvuma na  Iringa ya  Njombe - Iringa na Njombe  - Makete  zilifungwa na  waandamanaji hao ambao  walichoma  mataili  kila  kona kabla ya  jeshi la polisi  kutumia mbinu  zaidi  kufungua barabara  hizo.

Huku  watu kadhaa  wakijeruhiwa kwa  kupigwa mawe na waandamanaji hao na  wengine  kupigwa na polisi wakati  wa  vurugu  hizo na baadhi yao kukamatwa kwa  kuhusika na vurugu  hizo.

Majira ya saa 7 mchana kamanda wa  polisi mkoa wa Njombe alitaka  kuzungumza na wanahabari  kuelezea  hali  hiyo ila hakuweza  kufanya   hivyo  kutokana na hali kuchafuka tena na  hivyo kulazimika kikao  chake na  viongozi  wa Chadema Njombe  kukatishwa na wote   na viongozi hao wa Chadema kuongozana mitaani kutuliza vurugu   hizo.

Hata   hivyo kamanda  wa  polisi wa mkoa wa Njombe alisema hawezi  kugumza na  wanahabari  hao kwa madai bado  hali  si shwari .
 source:www.matukiodaima.co.tz

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni