YESU NI JIBU

Jumatatu, 19 Januari 2015

WATUMISHI WA MUNGU WAMETAKIWA KUWAKUMBUKA WENGINE AMBAO WAPO KATIKA HUDUMA KWA MUDA MREFU.



MCHUNGAJI  kiongozi wa kanisa la EAGT City Centre Florian Josephat Katunzi amekabidhi nyumba ya kisasa aliyoijenga kwa ajili ya Mdhamini Mkuu wa Kanisa hilo Mdhamini na Mshauri Mkuu wa kanisa la EAGT, ambaye pia ni mmoja wa waanzilishi wa kanisa hilo, Mch. Anyandwile Mwakisyala,  katika eneo la Nsonyanga Mbarali Mbeya,  katika sherehe iliyoliza na kuchekesha viongozi na wakazi wa mbeya..
Akiongea kwa furaha ya ajabu mbele ya ummati wa wachungaji wa kanisa hilo, wakiongozwa na Kaimu Askofu Mkuu, Asumwisyene Mwaisabila, Mdhamini huyo  alisema yeye alizaliwa mwaka 1924, na katika maisha yake hakupata mtoto wa kumzaa, alijitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote, lakini alikuwa akiishi machakani,  Mch. Katunzi amemuokoa  kwa kumjengea nyumba ya kisasa yenye kila kitu ndani.
“Wengi wanaomba  watoto wanafika mpaka Ulaya kutafuata watoto, lakini hawapati, mimi toka ujana wangu sina mtoto.. hatuna mtoto  natamka mbele ya umati huu, na Unaponisikiliza sauti hii imfikie  Mungu. Natamka nasema huyu Katunzi ndiye mtoto wangu wa kwanza, huyu ni mtoto wangu wa kwanza kuanzia sasa…. Kwa jambo lililotokea hata angetoka tumboni mwangu asingelifanya  ila angeweza kuja kuniharibu  na tena huenda angeweza kutamka kuwa mbona huyu kesho atakufa, lakini huyu mtoto alipotoka simjui, kwao sikujui, mama yake simjui, baba yake simjui, sasa kwa kuwa Mungu amefanya hivyo, kufuatana na huyu mtoto aambatane na mimi na mimi naambatana naye kwamba yeye ndiye mtoto wangu  mpaka maisha yangu nitakapokwenda kwa Mungu ni mtoto wangu wa maisha yangu,”alisema  na kuongeza:
“Maana alitoka kwa Mungu kujenga jengo hili si kawaida  ni la gharama , ni la mamilioni, sasa mamilioni haya angekuwa sijui si Mungu wapo wanaoua baba zao wakiona nyumba hii kama hii anaweza kumuwahisha baba yake, leo huyu hawezi kuniwahisha. Mama umesikia hawezi kutuwahisha mpaka siku zetu zitakapokwisha namuomba Mungu amuweke nyuma yetu na ninakokwenda mimi anifuate. Mwanangu hakika ni Mungu sio wewe.”
Kisha Mdhamini huyo aliongeza: “Naweka mkono juu yako kukuambatanisha na mimi, bara za Mungu na ulizi ziwe juu yako, Mungu asikuacha na akuinua na kukuweka mahali pa juu, uwe mkuu katika utumishi huu ufuate nyayo za Askofu Kulola Mwanzilishi wa kanisa  hili.”
KAIMU ASKOFU MKUU
Naye Kaimu Askofu Mkuu wa kanisa la EAGT, alipopokea kipaza sauti alisema: “Nyumba hii haikujengwa na Kanisa la EAGT, wala haikujengwa na Kamati kuu, wala Mfuko Mkuu, Yupo katibu mkuu hapa ni shahidi, bali ni Mungu wa mbinguni. Ashukuriwe kumuona mzee huyu anakula matunda yake ya huduma ya kazi yake. Yesu alisema alipokuwa anambatiza Yohana, usiseme tuna baba yetu ibrahimu, Mungu anaweza akainua mawe wawe watoto wake, kwa hiyo mtu au watu walioijenga nyumba hii hata mimi kama Askofu sijui ila wewe ……mimi na mshauri  mkuu na Mwakipesile (Brown Mwakipesile Katibu Mkuu) tumeitwa na kumkabidhi nyumba hii baba huyu ….Mwacheni Mungu aitwe Mungu aliyefanya maajabu haya, inatosha..”
Kisha alipopewa nafsi ya pili kuongea Kaimu Askofu Mkuu alisema: “Tunahitaji vijana ndani ya kanisa kama Mchungaji Katunzi wenye kuona na kuthamini wazee, wenye mzigo na kazi ya Mungu. Mfuateni huyu mchungaji Mungu ambariki sana.”
KATIBU MKUU
Katibu Mkuu katika maombi yake alisema: “Sisi ni watu wa Mungu na leo tunasimama mbele ya jengo hilo, jengo ambalo ni tukufu kwa Mungu na kama ambavyo tumesikia pale kanisani na Mjenzi wa nyumba ni mtumishi wa Mungu  na mama hapa kupata nyumba hii ni heshima kwa Mungu, heshima kwa kanisa, Baraka kwa familia na Baraka kwa kanisa pia name nasoma mstari mmoja tu juu ya jambo hili katika Injili ya Yohana 1:1, Biblia inasema………….. Bila Yesu Mzee wetu asingepata nyumba hii, lakini kwa sababu amemwamini Yesu Yeye ndiye mwanzo wa nyumba hii na ndiye mwisho wa nyumba hii name katika jina la Mungu baba na Mungu Mwana na Roho Mtakatifu nakata utepe huu kama ishara ya kuifungua nyumba hii.”
MCHUNGAJI KATUNZI
Mchungaji  Katunzi alipopewa kipaza sauti alisema: “Wazee wangu, Askofu wetu Mkuu, Katibu wetu Mkuu  na maaskofu wote mliopo, nawasalimu katika jina la Bwana. Niseme kitu kimoja tu, nilifika hapa  mwaka jana mwezi wa sita, nilikuwa nakwenda Tunduma kwenye huduma nikasema ngoja nikamsalimie mzee kwa mara ya kwanza nilifika hapa mwaka jana nashukuru Mungu nikapata mzigo wa kiimani kabisa kwamba tumjengee mzee wetu nyumba nzuri, kama yeye alivyo mzuri, nikamwambia mzee nitakujengea nyumba, lakini nilisema kwa imani nasikujua itakuwa kumbwa hivi. Nashukuru Mungu ametufanikisha nyumba ni hii sasa ipo. Ni heshima kwa Mungu …..”
Mshauri huyo alimuwekea mikono mchungaji Katunzi na kumbariki akimuomba Mungu amuinue na kunyooshea safari yake ya utumishi, katika kanisa lake la EAGT. Aibariki familia yake  na kuyanyoosha mapito yake.
Tukio hilo linaakisi  lile la Askofu Mkuu na Mwanzilishi wa EAGT, Dk. Moses Kulola alilolifanya siku chache kabla ya kutwaliwa alipomuwekea Mchungaji Katunzi mikono na kumuambia kuwa amemwachia mikoba ya kazi ya uinjilisti aliyokuwa akiifanya katika uhai wake na akamtaka kufuata nyayo zake.
Askofu Kulola aliandika hata kwenye wosia wake kuwa Katunzi ndiye msimamizi wa mali zake alizoacha.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni