YESU NI JIBU

Jumatatu, 19 Januari 2015

OPERESHENI MAVUNO YAZINDULIWA BCIC MBEZI BEACH.



Baada ya kuhitimisha “Operesheni Milikisha” ambayo imevuma mwaka 2014 ikiendesha elimu ya ujasiriamali kwa maelfu ya vijana wa MVIMAUTA ambayo ilizunduliwa mwezi 15/2/2014; jumapili iliyopita (4/1/2015) kwenye ibada maalum ya kuweka wakfu mwaka mpya, tuliamua kuitangaza rasmi operesheni mpya inayoitwa MAVUNO ambayo utambulisho wake ni kama ifuatavyo:
Utangulizi
Utendaji wa huduma za WAPO MISSION INTERNATIONAL ambaye ndiye mmiliki wa vyombo vya habari vya WAPOMEDIA, likiwemo gazeti Msemakweli, huzingatia mpango mkakati wake wa MAADILI KWA KIZAZI KIPYA ambao una mikakati mkubwa mitatu:
1.    Urejesho wa maadili kwa kwa vijana
2.    Kuinua vipaji vya uongozi
3.    Kumilikisha uchumi endelevu kwa kizazi kipya
Katika kutekeleza mikakati hii, kila mwaka unakuwa na kampeni maalum inayolenga mikakati hii, kulingana na vipaumbele husika. Kampeni hizi hupewa majina maalum ili kuhamasisha na kuelimisha na kushirikisha walengwa katika utekeleza wa mikakati yenyewe.
Mwaka juzi (2013 tulikuwa na OPERESHENI TAKASIKA ikilenga mikakati ya urejesho wa maadili kwa vijana. Mwaka jana (2014) kipaumbele kilikuwa utekelezaji wa mkakati wa kumilisha uchumi ambao kampeni yake ilijulikana kama OPERESHENU MILIKISHA. 
 
Japokuwa OPERESHENI MILIKISHA imehitimishwa mwaka 2014, bado Mkakati wenyewe wa “Kumilikisha uchumi” unaendelea sawasawa na “Urejesho wa maadili” nao bado unaendelea.
Kwanini Kampeni ya mwaka huu
imepewa jina la OPERESHENI MAVUNO?

Jina la kampeni hii kuitwa mavuno ni kwa sababu ya vipaumbele vyake ambavyo lengo kuu ni kuanza kupata matunda ya mipango mingi iliyokwisha kuandaliwa katika miaka takribani mitatu iliyopita. Ninaposema matunda nina maana ya kuanza kuona kwa macho matokeo ya mipango iliyobuniwa wakati uliopita.
Ufafanuzi mzuri ni miradi ya vijana ya kumilikishwa uchumi ambayo mwaka jana walikuwa wakiandaliwa kimafunzo, sasa mwaka huu wanaingizwa katika utendaji wenyewe ili waone uhalisia wa mikakati ya kumiliki uchumi
Wakati wa kuweka wakfu operesheni mavuno nilitumia mfano wa kibiblia ambapo Isaka alipanda mbegu na kuvuna mavuno mengi sana katika mwaka ule ule, japokuwa ilikuwa ni wakati wa njaa katika nchi ile.
Katika mwaka huu, tumetoa kipaumbele cha kuwepo kwa mradi ambao utatoa mazao ambayo yanatawahamasisha vijana kuondokana na kukata tamaa kimaisha kwa sababu ya “ukosefu wa ajira”  
Lakini mbali na mavuno ya kiuchumi, pia tunakwenda kutoa kipaumbele kwa mavuno ya kiroho. Mavuno ya kiroho ni msamiati wa Yesu Kristo mwenyewe aliposema, “Mavuno ni mengi, bali watendakazi ni wachache.”! Yesu hakumaanisha kuvuna mahindi, bali “wenyedhambi kurejesha mahusiano ya kiimani na Mungu wa kweli baada ya kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.
Kwa maelezo haya unaweza kuona kwamba, zoezi la “mavuno ya kiroho” ni utekelezaji endelevu wa “urejesho wa maadili ya kibiblia kwa jamii” ukienda sanjari na “kumilikisha uchumi” kwa walengwa.
Programu mpya za Operesheni Mavuno
Kampeni ya Mwaka huu inakuja na program mpya ambazo zitanatarajiwa kuanza rasmi mwezi Februari kwenye huduma za kila Jumapili kwenye kituo cha BCIC Mbezi beach ambazo ni kama ifuatavyo:
1.    Ibada za Kiingereza kwa jamii ya kimataifa
Kufuatia ongezeko la wageni kutoka mataifa ya nje ndani ya miji mikuu likiwemo jiji la Dar es Salaam, tayari hitaji maalum ya huduma za kiroho limekuwa kubwa kuliko miaka ya nyuma. Kuna ongezeko kubwa la wafanyabiashara na wataalamu mbali mbali, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa mataifa ya nje wanaokuja kusoma kwenye vyuo vikuu hapa nchini.
Katika kukidhi mahitaji ya kiroho kwa jamii ya kimataifa, Februari tunafungua ibada maalum kwa ajili yao, ambazo zitaendeshwa kwa lugha ya Kingereza.
2.    Chuo cha Biblia cha Jumapili
Uzoefu wa huduma za kiinjili umetufundisha kwamba, kumekuwepo tatizo sugu la watu wengi wanaookolewa huishia kuwa mbegu zilizoanguka “njiani” au kwenye “miamba” kama Yesu alivyosimulia katika maandiko.  
Chanzo kikubwa cha tatizo hili sugu la udumavu wa kiroho ni utekelezaji dhaifu wa agizo kuu la Yesu Kristo aliposema: “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote hadi ukamilifu wa dahari.” (MT 28:19-20)
UKifuatilia kwa makini kile Yesu alichomaanisha katika agizo hili ni kwamba alitaka “jamii ya Wasioamini” kutengenezwa kutoka kutokuamini/upagani na kufanyika wanafunzi wa Yesu kweli kweli. Aidha, Yesu alionesha kuwepo kwa mfumo wa kufundisha/kuelekeza jinsi ya kutekeleza katika maisha, amri na maagizo ambayo Yesu aliwaamuru wanafunzi wake kuyaishi.    
Kisha Yesu anatoa ahadi kwamba yeye mwenyewe atahakikisha udhihiriko wa utendaji wa nguvu za Roho Mtakatifu za kuleta mageuzi ya kitabia, kufukuza majeshi ya pepo wachafu yenye kusababisha magonjwa na ufukara uliokithiri. Lakini ukifuatilia katika uhalisia wa kiinjili utashuhudia udhaifu kama ifuatavyo:
  • Upungufu wa Injili kamili yenye mamlaka ya kuwafanya wasioamini kutubu na kugeuka kutoka kwenye mapokeo ya mila, desturi za kipagani;
  • Hofu ya kuihubiri na kuifundisha kweli kwa visingizio vya wafuasi kuhama madhehebu ya dini, na kupungua kwa matoleo ya sadaka kwenye makusanyiko
  • Mfumo dhaifu wa kuwafanya kuwa wafuasi wa mapokeo ya madhehebu ya kidini, yasiyo Neno hai lenye nguvu za Mungu za kubadilisha tabia na mienendo ya wafuasi
Katika kutaka kushughulikia tatizo hili tumeazimia Kuanzishwa kwa chuo cha Biblia cha Jumapili chenye mitaala iliyobeba kile ambacho Yesu aliagiza “kufundisha kuyashika yote aliyowaamuru”!
Itaendelea toleo lijalo.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni