Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli,
amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)
Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu Mstaafu Plasdus
Gervas Nkalanga (OSB) kilichotokea Ijumaa tarehe 18 Desemba, 2015 katika
hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho, Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.
Mhashamu Askofu Nkalanga aliyekua Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba
alistaafu uaskofu mwaka 1974 na kujiunga na watawa wabenediktini wamonaki
ambapo aliamua kwenda kuishi katika Abasia ya Hanga iliyopo katika Wilaya ya
Namtumbo Mkoani Ruvuma.
Katika salamu zake Rais Magufuli amesema Askofu Nkalanga
aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96 atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa
alioutoa kuhimiza imani na uchapakazi kazi katika kipindi chote cha miaka 54 ya
uaskofu wake na utawa wake akiwa katika Abasia ya Hanga.
Amesema Marehemu Askofu Nkalanga ambaye baada ya kustaafu aliamua
kuingia katika utawa akianzia katika ngazi ya chini kabisa ya Unovisi hadi alipofunga nadhili za
milele za utawa mwaka 2009, ameacha mfano mzuri unaohimiza jamii kuishi kwa
upendo, unyenyekevu na kutokata tamaa.
"Kupitia kwako Baba Askofu Ngalalekumtwa napenda kuwapa pole
nyingi Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Abate wa Abasia ya Hanga,
watawa na waumini wote wa kanisa Katoliki kwa kupoteza mtu muhimu aliyetoa
mchango mkubwa katika maendeleo ya kanisa na jamii kwa ujumla" amesema
Rais Magufuli.
Rais John Pombe Magufuli amemuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya
Marehemu Mhashamu Askofu Mstaafu Plasdus Gervas Nkalanga mahali pema peponi,
Amina.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
20 Desemba, 2015
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni