YESU NI JIBU

Jumamosi, 4 Aprili 2015

MWANANCHI AFUNGUA KESI POLISI AKILALAMIKA KUKWAZWA NA LUGHA ILIYOTUMIKA NA ASKOFU GWAJIMA.

Mwananchi mmoja  ambaye amejulikana kwa jina la Abubakar Yusufu, mkazi wa Kiluvia wilaya ya Kisarawe, ndiye aliyefungua kesi polisi akilalamika kukwazwa na lugha iliyotumika na Askofu Gwajima dhidi ya Askofu Mkuu Kanisa Katoliki jimbo kuu la Dar es Slaam, Kardinali Pengo.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilishindwa kuendelea kumhoji Askofu wa Huduma ya Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu tuhuma za kumtukana Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Askofu Gwajima alifika kituo cha Polisi cha Kati akiwa katika baiskeli ya kusukumia wagonjwa ambapo kutokana na hali yake kiafya kutokuwa nzuri alishindwa hata kupandisha ngazi.

Askofu Gwajima alifika katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central), ,ikiwa ni siku mbili tangu aliporuhusiwa kutoka katika Hospitali ya TMJ alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Wakili wa askofu huyo, John Mallya alisema  kuwa mteja wake alifika kituoni hapo saa 2.10 asubuhi, lakini Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam alipomuona, alisema hawawezi kumhojiano kwa kuwa afya yake haijaimarika.
“Alitutaka turudi na badala yake kufike kituoni hapo Aprili 9, mwaka huu,” alisema Wakili Mallya aliyeongozana na Askofu Gwajima pamoja na wachungaji wanane wa kanisa hilo.
Askofu Gwajima alijisalimisha mwenyewe  kituoni hapo Ijumaa iliyopita, baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Jeshi la Polisi, akituhumiwa kumkashfu Kardinali Pengo wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam, wakati akiendesha ibada kanisani kwake.
 Awali, wakati akihojiwa, aliishiwa nguvu na hatimaye kupoteza fahamu, hivyo kupelekwa hospitali kwa matibabu.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amesema Askofu Gwajima lazima atahojiwa na ofisi yake ili kujiridhisha zaidi na shughuli anazozifanya, ikiwamo umiliki na uhalali wa kutumia eneo la Kiwanja cha Tanganyika Packers, kilichopo Kawe.
Paul Makonda awali alipomtembelea hospitalini kumjua hali askofu Gwajima.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni