YESU NI JIBU

Jumatatu, 13 Aprili 2015

ASKOFU GWAJIMA AMWOMBA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE KUWASIHII VYOMBO VYA DOLA KUACHA KUMFUATILIA KUMFANYIA MAHOJIANO JUU YA MAMBO BINAFSI.



Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuvikemea vyombo vya dola vinavyomfuatafuata vikihoji mambo binafsi na kwamba akishindwa kufanya hivyo itakuwa wazi kwamba yeye ndiye anawatuma.
Akihubiri mamia ya waumini wa kanisa hilo, Gwajima alisema amekuwa akifuatwafuatwa na vyombo vya Serikali utadhani yeye si raia wakati ni Mtanzania halisi.
“Rais Kikwete tafadhali namuomba awakemee watu hawa... asipowakemea, basi kanisa langu litajua kwamba yeye ndiye anayewatuma,” alisema Gwajima huku akishangiliwa na waumini waliokuwa wakimsikiliza.
Huku wakinyeshewa na mvua, waumini hao walikuwa wakimsikiliza Askofu Gwajima, siku tatu baada ya kiongozi huyo kuhojiwa kwa mara ya pili na polisi na kutakiwa awasilishe mambo 10 yanayohusiana na usajili wa kanisa, uongozi na mali zake.
Akielezea juu ya Uraia wake amesema kuwa,
“Mimi ni Mtanzania halisi acheni nifanye kazi ya Mungu, kama mnadhani mimi si Mtanzania, basi mmepotoka kwani kwa hilo mtashindwa,” alisema.
Alisema makundi ya jamii yamekuwa yakitoa kauli mbalimbali lakini hayabughudhiwi anavyofanyiwa.
“Madaktari, wanasiasa, wafanyabiashara wamekuwa wakitoa misimamo yao lakini hawabughudhiwi iweje Gwajima tu? Nitaendelea kuwapa vidonge vyenu kila mtakapopotoka, nafanya kazi ya bwana,” alisema.
 Na kwa upande wa utajiri wake,
Gwajima alisema amekuwa akishangazwa na vyombo vya Serikali vinavyohoji utajiri alionao bila kujua anaongoza idadi gani ya waumini. Alisema anaongoza kanisa lenye waumini zaidi ya 70,000 ambao ni kama watoto wake na kwamba yeye ni baba yao wa kiroho.
“Waumini hawa mimi ni baba yao wa kiroho, nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 tu nitakuwa na Sh70 milioni, halafu mnahoji utajiri ninaupata wapi?” alisema na kisha kuwauliza waumini hao... “Hivi baba yenu nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 mtanipa au mtaninyima?”
Alijibiwa, “Tutakupaaaa!” Baada ya majibu hayo waumini hao walianza kupeleka fedha katika jukwaa kuu huku wakiimba nyimbo za kumtukuza Mungu.

Una maoni gani,

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni