Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu, amewataka viongozi wa dini kuwakemea kwa sala watu
wanaojihusisha na ujangili kwenye hifadhi za wanyamapori nchini, ili waachane
na vitendo hivyo.
Nyalandu alitoa wito huo jana wakati
akizungumza na viongozi hao kwenye ziara yao ya kutembelea hifadhi ya
wanyamapori ya Tarangire mkoani hapa, iliyoandaliwa na wizara yake kwa
kushirikiana na taasisi ya kimataifa ya kupambana na mauaji ya wanyamapori na
biashara ya pembe za ndovu na faru ya Wild Aid.
Alisema wizara yake imeamua
kuwashirikisha wadau wote katika vita dhidi ya ujangili wa wanyamapori wakiwamo
tembo na faru.
“Nawaomba viongozi wa dini muwakemee
kwa sala wale wote wanaoua wanyama wetu, waelezeni faida za wanyama hawa kwa
taifa ili waache vitendo hivi viovu haraka sana, ” alisisitiza Nyalandu.
Kwa upande wao, viongozi hao
wameitaka serikali kuweka sheria kali katika uhifadhi wa wanyama pori na
mazingira ili kutokomeza uwindaji haramu wakiwamo tembo na faru.
Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dk.
Valentino Mokiwa, alisema viongozi wa dini wana uwezo mkubwa
wa kueneza taarifa za kupiga vita mauaji ya tembo kwa kuwaonya na kuwaelekeza
waumini katika misikiti na makanisa.
Aliitaka serikali kutazama kwa kina
utalii wa uwindaji ili kuona kama ndiyo kichocheo cha mauaji ya tembo ili
kuendelea kuhifadhi wanyama pori.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Alhad Salum, alisema amefurahishwa na wizara hiyo kuwapa fursa ya
kuangalia wanyama katika hifadhi hiyo kwa sababu imewasaidia kufahamu maisha
yao, hivyo atahamasisha waumini kuungana kupiga vita ujangili.
Mwakilishi wa Jumuiya za Kikristo
Tanzania, Mchungaji Grace Masakulangwa, aliitaka serikali kutokomeza mtandao wa
biashara ya pembe za ndovu nchini.
“Serikali inafahamu mtandao wa
wahalifu hawa wanaotumalizia wanyama. Ilivunje genge la watu hao haraka
kwani vyombo vya ulinzi na usalama vina taarifa zao, ” alisema
Masakulangwa.
Nabii Askofu, Ephata Mwingira,
alisema serikali imefanya jambo jema kuwashirikisha na kuwataka viongozi wake
waonyeshe dhamira ya kweli katika mapambano ya kulinda rasilimali.
Je wewe unamaoni gani kwa hili ambalo viongozi wa dini kuombwa kukemea majangili kwa sala.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni