YESU NI JIBU

Jumanne, 28 Oktoba 2014

HOJA YA ASKOFU SYLVESTER GAMANYWA JUU YA ONGEZEKO LA IMANI ZA UCHAWI MAKANISANI TANZANIA:

Katika toleo lililopita tulianza makala na Marejeo ya athari za imani za uchawi makanisa; kisha tukagusia kwa ufupi historia ya uchawi ambao mwasisi wake anasadikiwa kuwa ni Nimrodi; na tukikomea kwenye kipengele kinachohusu ”Nguvu za uchawi na uganga dhidi ya Musa” ambapo tulishuhudia jinsi wachawi wa Farao walivyopambana na Musa kwa kuigiza miujiza aliokuwa akiifanya Musa. Leo tunaendelea na uchambuzi huo:



Ukomo wa nguvu za uchawi

katika kuigiza miujiza ya Musa 
“BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri.  Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.  Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama.  Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.” (KUT. 8:16-19)

 Maandiko tuliyonukuu hapa juu, yanadhihirisha jinsi ambavyo hapo mwanzo wachawi wa Farao walijaribu kuigiza miujiza ya Musa ili kushindana naye. Na ukweli wa macho walionekana kufanikiwa na kumpa Farao Kiburi. Hali ingeliweza kumchanganya Musa, kuona wachawi nao wanafanya miujiza ile ile anayoifanya. Lakini Musa hakuteteleka kiimani, badala yake alimwamini Mungu kujitetea kwa kudhihirisha uweza wake dhidi ya nguvu za wachawi wa Farao. Hatimaye, tunashuhudia katika maandiko wachawi walikwama kuigiza “muujiza wa kuleta chawa”. Tunasoma kwamba: “….Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze;….” Baada ya kushindwa ilibidi wakiri waziwazi kwa Farao wakisema kwamba: ”jambo hili ni chanda cha Mungu…”
Kana kwamba hii haikutosha, miujiza mingine iiliyofuatia ya mapigo ya Musa dhidi ya Farao; hata waganga wake hawakusalimika. Tunajionea kupitia maandiko kuhusu muujiza wa pigo la majipu ambapo tunasoma: “Basi wakatwaa majivu ya tanuu na kusimama mbele ya Farao; na Musa akayarusha juu mbinguni nayo yakawa majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama. Nao wale waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa kwa sababu ya hayo majipu, kwa maana hao waganga walikuwa na majipu, na Wamisri wote walikuwa nayo.” (Kut.9:10-11)



Mapambano kati ya Simoni mchawi

na Filipo aliyejaa Roho Mtakatifu



Injili iliyohubiriwa na mitume na wainjilisti wa kanisa la kwanza nayo pia iliambatana na ushindani dhidi ya nguvu za uchawi. Ili kuupata ushahidi wa haya nisemayo, hebu twende kwenye kitabu cha Matendo ya Mitume na kuangalia kisa cha mchawi aliyekua maarufu sana katika jimbo la Wasamaria:



“Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa.  Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu.  Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake.  Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.  Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka. (MDO 8:9-13)

Kwa mujibu wa maandiko tuliyosoma tunathibitisha kwamba, mchawi Simoni aliwashangaza Wasamaria kwa muda mwingi kwa uchawi wake; tena akasifiwa sana kwamba alikuwa na “uweza mkuu wa Mungu”. Na kwa kuwa hapakuwepo mshindani wake, aliteka usikivu wa watu wote kuanzia mdogo hadi mkubwa. Bila shaka alifanya utapeli huu kwa miaka mingi.
Lakini wakati muafaka ulifika dhidi ya Mchawi Simoni kupata changamoto. Tumesoma habari za Mwinjilisti Filipo ambaye aliingia Samaria na kukuta Simoni akiendelea na mazingaombwe yake. Filipo hakutaka kushindana na Simoni ana kwa ana kwa kumkemea na kumgombeza kwa matamko ya matishio ya maneno. Filipo aliamua kuihubiri Injili ya Kristo na kumruhusu Roho Mtakatifu afanye kazi yake.
Tumeshuhudia jinsi ambavyo Filipo alitumiwa kufanya miujiza iliyovunja rekodi ya uchawi wa Simoni, na wateja wote wa Simoni walimwamini Yesu Kristo aliyehubiriwa na Filipo wakafunguliwa katika vifungo vya pepo na kuponywa magonjwa na kuponywa ulemavu wa viungo vya mwili. Hatimaye tumeshuhudia mchawi SImoni naye “akibwaga manyanga” yake na kujisamilisha kwa nguvu za Roho Mtakatifu aliyekuwa naye Filipo.


Paulo alivyoshindana

 na mchawi Bar-Yesu

 Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu;  mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu.  Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani.  Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho,  akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?  Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.  Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana. (MDO 13:6-12)


Kwa mujibu wa maandiko haya, tunashuhudia jinsi ambavyo uchawi unaweza kutafsiriwa kuwa ni huduma ya kinabii. Kwa sababu ya miujiza ya kimazingaombwe inayofanywa na wachawi/waganga, watu wengine hudanganyika kwa kudhani kuwa hizo ni nguvu za Mungu, hasa pale ambapo mchawi husika anapoamua kutumia mwavuli wa dini kama kinga ya kuficha uchawi wake. Lakini, pamoja na hao wachawi, kujificha chini ya mwavuli wa dini; hawawezi kushindana na utendaji halisi wa nguvu za Roho Mtakatifu! Tunamwona Paulo akitumia nguvu za Roho Mtakatifu kumdhibiti Bar-Yesu!

  Itaendelea toleo lijalo
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni