Kutokujiheshimu ni kupunguza au kuacha kabisa kufanya mambo yale yaliyokufanya uheshimike.
Kufanya mambo kinyume na matarajio ya wale waliokuwa
wanakuheshimu.
Mara nyingi watu wakutanapo kwa mara ya kwanza, kwa kuwa hawafahamiani
kabisa, kila mmoja hujaribu kujiheshimu kwa muda, na kweli kwa muda huo
huheshimika mbele ya wasiomjua.
Lakini kwa kadiri wahusika wanapokaa pamoja kwa mudaa mrefu
zaidi, kila mmoja huanza kujivua “heshima bandia” aliyokuwa amejivika kwa muda
na kuonesha baadhi ya tabia zake.
Hali hii hutokea katika mijumuiko mbali mbali inayokutanisha
watu wageni kwa ajili ya matukio au shughuli za kijumuiya. Maeneo kama
mashuleni, kambini, makazini, makazi mapya na katika majengo ya mikutano na
ibada na kadhalika.
Kuanzia hapo viwango vya heshima ambavyo muhusika alikuwa
amejipatia mioyoni mwa wasiomjua, tayari huanza kupoteza mvuto, tena huendelea
kufifia zaidi kwa kadri muhusika anavyozidi kuonesha madhaifu yake ya kitabia.
Iko mifano mingi katika jamii ya baadhi ya watu walioupata
umaarufu wa kuheshimiwa, na baada ya wahusika kuanza au kuweka hadharani vitendo
visivyokubaliana na heshima stahiki, ghafla wamepoteza heshima zao!
Viashiria vya kupoteza heshima
Hivi mtu atajuaye kwamba amepoteza heshima mbele ya
waliokuwa wakimheshimu? Kitu cha kwanza ni kupoteza sifa zile alizokuwa
akizipata muhusika. Kama alikuwa anapongezwa kwa mambo yale ambao yamepatia
heshima, sasa anaanza kupata lawama badala ya pongezi.
Kama alikuwa ana wafuasi wengi wanaomsikiliza, mara
anapoteza wafuasi kwa sababu kile walichokuwa wanakifuata hakipo tena, au
kimechuja kwa sababu watu wamepoteza imani naye.
Kama muhusika alikuwa akitoa huduma bora kwa watu wengi
ambao walikuwa wanapenda huduma zake; baada ya muhusika kuchakachua viwango vya
ubora wa huduma zake, hupoteza wateja wake kwa kuwa huduma hizo hazikubaliki
wal kuaminika kama hapo awali.
Naomba nitoe angalizo hapa mapema. Si kila mwenye wafuasi
wengi, au wateja wengi anafuatwa kwa kuwa anafanya mambo ya heshima. Ziko
huduma zisizo na heshima, na hivyo hata wafuasi au wateja nao pia; hata kama ni
wengi sana huenda ama hawajali mambo ya heshima ya mtu au wenyewe binafsi pia hawana
heshima.
Kwa hiyo “wingi” wa wafuasi au wateja sio kigezo pekee cha
kuthibitisha heshima ya mtu. Heshima ya mtu hutambulika kwa tabia na mwenendo
wa aina ya huduma anazozitoa sambamba na aina ya wafuasi au wateja wake.
Madhara ya kupoteza heshima
1. Kuvunja imani za wengine
Kama tulivyokwisha kudokeza huko nyuma ni kwamba, mtu
maarufu anaposhindwa kutunza heshima yake, sio kwamba anaacha kuheshimika kama
hapo awali; bali hii huleta madhara mengine kwa wale waliokuwa wakimheshimu.
Madhara yenyewe ni wafuasi au wateja kupoteza imani na mtu mwenyewe.
Kupoteza imani na mtu hakuishii kumpuuza muhusika peke yake,
bali waathirika hupoteza imani na wengine wenye kutoa huduma zinazofanana na
yule aliyechakachua maadili ya huduma husika. Wengi hujenga mtazamo hasi dhidi
ya wengine ambao hata kama wao bado wanajiheshimu; nao pia huanza kushukiwa
vibaya kwamba huenda hata wao wanafanana na huyo; kwa tafsiri ya mithali
isemayo kwamba “Samaki mmoja akioza, wote wameoza”!
Kimsingi, kipengele hiki ndicho kinachobeba uzito wa makala
na mada hii. Nasema hivi kwa sababu nimeshuhudia na wengine ni mashahidi katika
hili. Hivi sasa sio siri kwamba huduma nyingi za kikanisa ziko kwenye mazingira
tata na hatarishi.
Kashfa nyingi zinazowaandama wale wanaoitwa “watumishi wa
Mungu” au “wakuu wa dini” au “viongozi wa taasisi binafsi za kiroho” zimechafua
imani za wafuasi wengi kiasi kwamba “imani za wengi zimeathirika”! Watu wengi
sio kwamba waanazidi kupoteza imani na watumishi wa huduma za kikanisa, bali
wanapoteza imani na Mungu huyo anayehubiriwa na hao “watumishi bandia”!
2. Kufilisika
Madhara mengine yatokanayo na kupoteza heshima, ni pamoja na
muhusika kuishiwa na kufikia ukomo wa ubora wa huduma alizokuwa anazitoa hapo
awali. Kinachosalia ni “bora huduma” badala ya “huduma bora”! Kukoma kwa ubora
wa huduma pia husababisha kukoma kwa mapato yaliyokuwa yakiambata na huduma bora.
Hii ndio maana ya kufilisika.
Madhara ya kufilisika ni pamoja na kushindwa kumudu gharama
za uendeshaji huduma pamoja na matumizi binafsi nayo kuathirika. Katika
mazingira ya jinsi hii, muhusika hulazimika ama kuuza vitu vya thamani ili
kulipa bili na madeni huzidi huongezeka.
3. Maradhi
Kupoteza heshima sio kitu kidogo na rahisi. Japokuwa hapo
mwanzo muhusika anaweza kujifanya hajali sana na kujitetea kwa maneno mengi;
lakini kwa ndani ya nafsi tayari anayo maumivu makali ambayo hatimaye humletea maradhi
yatokanayo na maumivu ya hisia hasi. Maradhi hayo ni pamoja na “msongo wa
mawazo” (Stress) au “mfadhaiko wa mawazo” (Depression)!
Magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari, hata saratani ni
baadhi ya chanzo kikuu ni mfadhaiko na msongo wa mawazo ambapo muhusika katika
kujituliza hujikuta akila na kunywa vyakula ambavyo huathiri afya yake pasipo
yeye kujua.
4. Kufupisha maisha
Hapa sasa mambo yakifikia kilele cha kero ndipo muhusika
huamua kufanya maamuzi magumu. Wengi hujiua kwa ama kujinyonga, kunywa sumu, au
kujipiga risasi. Kwa bahati mbaya watu wengi wana tafsiri potofu kuhusu kifo.
Wanadhani kufa ni kuepukana na shida na matatizo ya duniani na kupumzika
milele. Kwa dhana hii wenye kujiua wanadhani wakifa watapumzika. Kumbe ndiyo
wameanza awamu ya pili yenye mateso yasiyokoma milele!
Kilele cha mambo yote
ni hukumu ya milele
Katika kifungu kidogo cha 4 hapa nimedokeza kuhusu dhana
potofu kuhusu kifo. Kufikiri kufa ni kupumzika. Nilidokeza kwamba kwa wengine
kufa ni kuanza awamu ya pili yenye mateso yasiyokoma. Pengine hapa niweke
bayana suala hili ili kuweka waziwazi ukweli wa mambo.
Yesu Kristo alitoa mfano wa watu wawili walioishi duniani na
kila mmoja wakati wa uhai wake aliishi aina fulani ya maisha ambayo yalikuwa na
mwonekano tofauti katika jamii. Watu hao mmoja alikuwa tajiri na wa pili
alikuwa maskini na mwenye maradhi ya ngozi. Tajiri aliishi maisha ya anasa na
udhalimu wakati maskini aliishi maisha ya uchaji Mungu. Yesu alisimulia kwamba
wote walikufa. Kisha Yesu akasema kila mmoja alikwenda mahali maalum kulingana
na aina ya maisha aliyoishi duniani. Tajiri alikwenda kuzimu mahali penye
mateso makali kupindukia. Yule maskini kwa kuwa alikuwa mchaji alikwenda mahali
paitwapo “kifuani pa Ibrahimu”.
Kisa kinasimulia kwamba Yule Tajiri kule kuzimu aliweza
kuwaona Ibrahimu na yule maskini Razaro na kuomba Razaro amletee angalau tone
la maji kwani alikuwa akiunguua vibaya sana. Ibrahimu alimjibu kama ifuatavyo: “Mwanangu
kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro
vivyo hivyo alipata mabaya; na sasa yeye upo hapa anafarijiwa, na wewe
unaumizwa…..” Unaweza kusoma kisa kizima katika Luka 16:19-31)
Nilichotaka kusisitiza hapa ni kwamba, si kila mfu afaye
huenda kupumzika. Inategemea mfu husika aliishi aina gani ya maisha machoni pa
Mungu. Pili, mahali aendako mtu baada ya kufa hutegemeana na uchaguzi wa maisha
aliyoishi duniani.
Mfano wa tajiri alioutoa Yesu hakuma akilaani utajiri wa
Yule tajiri, bali alikuwa akionesha “matumizi mabaya ya utajiri” ambayo ndiyo
yalisababisha aende kuzimu kwenye maumivu makali. Matumizi ya tajiri yalikuwa
ni kuvaa na kula kwa anasa duniani.
Alikataa kutumiia mali zake kuwasaidia maskini, hata wale
walioletwa mbele zake aliwapuuza kwa kuwatupia makombo akiwemo Lazaro. Ndiyo
maana alipokufa ilibidi apokee laana nyingi kuzima badala ya Baraka:“Mwenye
kuwagawia masikini hatahitaji kitu, bali afichaye macho yake atakuwa na laana
nyingi.” (Mith.28:27);
Hitimisho
Nataka kumaliza kwa kauli ya mada hii ya kwamba,
“ukiheshimiwa heshimika”! Tumesoma kwamba juhudi katika kutafuta mali na
umaarufu si dhambi. Lakini baada ya kuvipata unavitumiaje, na wewe mwenyewe
tabia yako inasomekaje mbele za wengine katika jamii. Tumepitia uchambuzi wa
baadhi ya wengi wenye kufanikiwa duniani wakaheshimiwa kwa mafaniko, na kisha hushindwa
kutunza heshima zile walizozipata; hatimaye kujikuta wanapoteza heshima hizo.
Tulijifunza kuhusu tatizo la kujikinai baada ya kufanikiwa. Naweza kusema
kwamba kwa walio wengi changamoto sio kufanikiwa, bali ni jinsi ya kuyatunza
mafanikio yenyewe.
Binadamu hujisahau upesi hata kusahau kule alikotoka. Haya
basi hilo linaweza kuzungumzika. La kushangaza zaidi ni binadamu kutokujali
kule aondako! Na miye napenda kukumbusha tena, na kwa wengine, hii yaweza kuwa
ni onyo la mwisho kwa wahusika. Mungu amesema waziwazi katika neno lake kwamba:
“Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni;
bali sasa anawaagiza watu wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku
atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu Yule aliyemchagua; naye amewapa
watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.” (Mdo.17:30-31)
“Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti
cha hukumu cha Kristo ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili,
kadiri ya alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.” (2 Kor.5:10)
“hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche
Mungu, nawe uzishike amri zake, maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana
Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au
likiwa baya.” (Mhu.12:13-14)
“Ukeheshimiwa heshimika”
mwisho
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni