YESU NI JIBU

Alhamisi, 10 Machi 2016

NGUVU ZA ROHO MTAKATIFU KWA MWAMINI NA KARAMA ZAKE.

Utangulizi

"Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.  Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.  Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.  Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.  Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;  mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;  na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;  lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye." (1 KOR. 12:4-11)

Maandiko yaliyonakiliwa hapa juu tunakutana na vitu vinavyoitwa karama za vipatavyo tisa. Karama ya kwanza ni Neno la hekima, pili neno la maarifa, tatu karama ya kupambanua roho, nne karama ya imani, tano karama za kuponya magonjwa, sita karama ya matendo ya miujiza, saba karama ya unabii, nane karama ya aina za lugha na tisa karama ya kutafsiri lugha.


Ili kuweza kuzielewa vizuri karama hizi nitazigawa tatu tatu katka mafungu makuu matatu. Kila fungu lina karama tatu zinazofanya kazi zinazoendana au kuhusiana kwa karibu.

Fungu la kwanza ni karama za Neno la hekima, neno la maarifa na karama ya kupambanua roho. Hili kundi linabeba karama za MAFUNUO. 

FUNGU la Pili limejumuisha karama za Imani, karama za kuponya magonjwa, na matendo ya miujiza. Hili kundi limebeba karama za NGUVU. 

Fungu la tatu limebeba karama za unabii, aina za lugha na tafsiri za lugha. Hili fungu limesheheni karama za MAWASILIANO/NDIMI
Uchambuzi wa karama
ya Neno la Hekima

Kwa mpangilio huu, sasa napenda kuanza uchambuzi wa karama moja kutoka fungu la kwanza la karama za mafunuo. Nianze na karama ya NENO la hekima:

 Neno la hekima ni uwezo wa kimungu unaowasilisha sehemu ndogo sana ya hekima ya Mungu ili kutoa ufumbuzi katika Jambi/Tatizo/ shida inayohitaji maamuzi ya kuzuia au kuwezesha jambo lililokwama.

Tunapata neno la hekima lilifanya kazi na Yusufu akatoa mkakati kiuchumi wa kuinusuru Misri na njaa iliyokuwa inaikabili kwa kipindi cha miaka saba mfululizo. Mtu mwingine ni mfalme Sulemani aliyeamua kesi ya wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto. Hiki kisa maarufu sana katika Biblia ambacho kilimpa umaarufu mkubwa sana Sulemani

NENO la hekima ni karama ambayo humwezesha mwanafunzi wa Kristo kupata wazo au ufunuo wa jambo ambalo likifanyiwa kazi linazalisha mambo makubwa yasiyotarajiwa. Wakati mengine kupitia Neno la hekima anaweza kupata ufumbuzi wa migogoro au mahali penye kutokuelewana na kufanya upatanisho . Hii inaweza hata kufanya mapatano na maelewano kati ya wanandoa na wanafamilia. 

Uchambuzi wa Karama
 ya Neno la Maarifa

Jana nilitoa utangulizi wa somo la karama za Roho Mtakatifu. Nilizipanga karama tata tatu ktk mafungu matatu maalum. Kisha katika fungu kwanza la karama za mafunuo nilichambua kwa ufupi karama moja ya NENO la hekima

Leo napenda kuchambua karama ya NENO la maarifa. Ningependa kutoa kisa kimoja katika Biblia ili kuonesha utendaji wa karama ya neno la maarifa.

Kisa hiki kinahusika na WATU wawili katika Biblia wanaitwa Anania na safiraa. Walikuwa washirika wa kanisa la kwanza ambao waliahidi kuuza kiwanja na kuleta thamani fedha yote kanisani ili kusaidia huduma za kikanisa.

Wanandoa hawa walipouza kiwanja kile, badala ya kutimiza nadhiri yao wakapatana kwa siri nyumbani kuficha sehemu ya fedha na kuleta sehmu isiyo kamili kanisani.

KUMBE WAKATI wanaendelea na kikao chao cha siri nyumba huku Petro hekaluni akapata maono yanayoonesha kuhusu kikao hicho na kusikia kila siri ya udanganyifu. 

Ilipofika wakati wa ibada na kipindi cha sadaka za fedha za viwanja, Anania akaleta fedha na kuiwasilisha miguuni pa Petro. Ghfala Petro akamuuliza Anania kama fedha aliyoiwasilisha ndiyo hiyo hiyo thamani ya kiwanja walichouza. Anania akajibu uongo.

“Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?  Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.  Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya.”(MDO 5:3-5)

Hapa tumesikia imeandikwa kwamba Shetani alimjaza Anania moyo wa kumwmbia Roho Mtakatifu uongo. Hapa ndipo tunaona utendaji wa karama ya NENO la maarifa. Ni uwezo wa Roho Mtakatifu wa kutambua vitu vyenye hila vinavyofanyika sirini na kuvifunua hadharani ili kuepusha unajisi au upotoshaji wenye athari 

Jambo la kutisha ni kwamba, taarifa ya ghafla ya kuumbuka hadharani ilisqababisha mshtuko wa moyo na kufa papo hapo. Baadaye alikuja Safira mkewe akaulizwa naye Akasema uongo na kufa pale pale. Akaenda kuzikwa.

Sasa watu wakiambiwa utendaji wa Roho Mtakatifu wanadhani kila wakati Roho ni mpole mkimya na asiye na ukali. Sio kweli. Tunaweza kuujua ukweli huu kupitiia baadhi ya karama zake, moja ikiwa ni hii ya karama ya maarifa. Kufichua maovu yaliyofichika ndani ya mioyo ya wanafiki.

Utendaji wa Karama
ya Kupambanua roho

Karama ya kupambanua roho ni karama makini sana. Wengine huichanganya karama hii ya NENO la maarifa. Lakini hii ni tofuati. Wakati karama ya NENO la maarifa ni uwezo wa kufichua siri/njama/hujuma zilizofichika katika mioyo ya wanadamu; karama ya kupambanua inahusika zaidi na kutofautisha aina ya roho zinazotenda kazi huku zikijifananisha na Roho wa Mungu wakati sio. 

Ni uwezo wa kugundua kimungu aina ya roho inayotenda kazi kupitia mtu. Kama ni Roho wa Mungu au ni pepo mchafu. Na kama ni pepo mchafu anatenda kwa kutumia hila gani ili kuweza kumtambua na kumkemea kama ilivyotokea kwa kisa cha akina Paulo:

"Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.  Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.  Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile." (MDO 16:16-18)

Unaweza kuona jinsi huyu pepo alivyosumbua kwa muda mrefu. Paulo alijua kwamba ni pepo wa utambuzi amekwisha kuwajua. Lakini Paulo hakujua mara moja ni kwanini anawatabiria akina Paulo mambo ya kweli na huku anaendelea kuvuta wafuasi waende kwake mganga badala ya kwenda kwa Paulo wasikie injili yao.

Safari karama ya kupambanua ikampa Paulo ufunuo wa uharibifu wa huyo pepo na kwamba ufmbuzi ni kumkemea amtoke yule mganga kitu ambacho kilikuwa ni kuvunja na kuharibu biashara ya uganga uliokuwa ukitajirisha vigogo wengine mjini humo

Karama ya kupambanua hufanya kazi kila mahali ambapo kuna utendaji wa karama nyingine hasa Karama ya unabii ambayo huchanganywa sana na utabiri wa nyota au utabiri wa kipepo. Hata wakati wa kutoa unabii kuna roho za nabii za uongo ambazo hujitambulisha kama unabii kutoka kwa Mungu kumbe ni pepo tu.

Leo ndo tumekamilisha uchambuzi wa karama ya kupambanua roho kutoka katika fungu la karama za MAFUNUO. unaona jjnsi ambavyo zote kazi yake ni kufunua, kufichua na kuweka waziwazi vilivyositirika ili ukweli halisi ujulikane.
Itaendelea toleo lijalo...

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni