YESU NI JIBU

Ijumaa, 23 Mei 2014

FALSAFA YA UKOMBOZI KWA MUJIBU WA BIBLIA HATUA YA MWISHO.


Kwenye toleo lililopita tulipitia vipengele vinavyohusu magonjwa kwa kujibu swali kwamba “Ikiwa Yesu alibeba magonjwa yetu yote kwanini bado tunaugua?” Majibu tuliyopitia yalikuwa ni pamoja na: Dhambi kuendelea kupewa nafasi ya kutawala; Mtazamo kuhusu nafasi ya magonjwa katika miili yetu; na Mashambulizi ya Ibilisi  ya kupima imani yetu.
Leo tuendelee kujikumbusha kuhusu nukuu za maandiko yanayotangaza kazi ya ukombozi wa Yesu msalabani; na kisha tutakwenda kujibu maswali magumu ya umaskini wa kipato kuendelea kutawala ulimwengu wakati Yesu alifanyika maskini ili sisi tuwe matajiri kwa umaskini wake:
Marejeo kuhusu Kazi ya Ukombozi wa Yesu Msalabani
Marejeo kuhusu Kazi ya ukombozi iliyofanywa na Yesu msalabani ni muhimu sana katika mfululizo wa makala haya kwa sababu zifuatazo: Moja, si kila msomaji anayesoma makala haya alianza nasi tangu mwanzo wa makala yenyewe. Kwa hiyo anahitaji kujua kiini cha makala na matarajio yake ni nini. Pili, tunaporejea kusoma maandiko kuhusu ya ukombozi kwenye makala haya tunajiwekea mwongozo wa kutujengea nidhamu ya kujifunza pasipo kutoka nje ya mada.
Kwa hiyo, tunaposema “Kazi ya Ukombozi iliyofanywa na Yesu Msalabani; kimsingi tunamaanisha mambo makuu matatu yafuatayo: 1 Dhambi, 2. Magonjwa, 3. Umaskini wa kipato.
Kwa habari ya dhambi tunashuhudia kimaandiko pale Paulo alipowakumbusha Wakorintho akisema: “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika yeye.” (2.Kor.5:21)
Kwa habari ya magonjwa tunashuhudia kimaandiko pale Mathayo alipoandika katika Injili akisema: “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie line neno lilonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na kuyachukua magonjwa yetu.” (Matt.8:16-17)
Kwa habari ya umaskini wa kipato tunashuhudia kimaandiko pale Paulo alipowakumbusha Wakorintho akisema: “Maana mmejua  neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” (2.Kor.8:9)
Mpendwa msomaji! Kwa kuwa baadhi ya nukuu za maandiko haya zilikwisha kuchammbuliwa katika makala za nyuma; na kwa kuwa huenda msomaji hukupata nafasi ya kusoma yaliyokuwemo; ili kukujengea mtiririko makini napenda kurejea kwa ufupi sehemu ya vipengele muhimu vinavyohusu falsafa ya ukomboai katika tawi lake la umiliki:
Maono asilia ya Mungu kuhusu binadamu
Kwa wale tunaoamini kwamba binadamu ameumbwa na Mungu kama livyoandikwa katika Biblia, tunao ushahidi wa kimaandiko kwamba maono ya Mungu kuhusu binadamu hayakuwa na nia ya kumfanya binadamu kuwa fukara na maisha ya fujo na ghasia duniani.
Tukisoma maandiko kuhusu maono ya Mungu juu ya binadamu tusoma kwamba: “Mungu akasema na tumfanye mtu kwa mfano wetu; na kwa sura yetu; wakatawale…..” (Mw.1:26)
Andiko hili linadhihirisha bayana kusudi la Mungu kuhusu binadamu hata kabla hajamuumba. 1. Kuumbwa kiumbe anayeshabihiana na Mungu kwa fikra, hisia na utashi; 2. Kuumbwa kiumbe atakayemwakilisha Mungu katika utawala wa dunia na viumbe vyote vilivyomo.
Kutokana na Maono haya Mungu aliyatimiza kwa kuwaumba binadamu wa kwanza, Mwanamume na mwanamke, kama ilivyoandikwa: “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale…..” (Mw.1:27-28)
Kutokana na ushahidi wa kimaandiko tuliyosoma hapa juu, tunathibitisha kwamba binadamu wa kwanza waliumbwa katika hali ya utukufu wa Mungu, na wakamilikishwa kuitawala nchi na viumbe vyote vilivyomo. Kwa maelezo mengine ni kwamba, haki na mamlaka ya kumiliki ni ya kimaumbile. Hisia ya kumiliki ni sehemu ya maumbile ya  kila binadamu.
Pasipo kujali binadamu yuko katika mazingira ya aina gani hisia ya kumiliki imo ndani yake. Maswali mengi yanayojitokeza ni kama huu ndio ukweli tena wa kimaumbile kwa kila binadamu, kwanini basi hivi sasa kuna matabaka ya maskini na matajiri, watumwa na mabwana, waajiri na wajiriwa? Majibu ya maswali haya yanatupeleka kwenye sehemu ya pili ya falisafa ya umilikishaji.
Kuvunjika kwa mahusiano na kupoteza mamlaka
Baada ya binadamu wa kwanza kuumbwa, na kumilikishwa kama Mungu alivyowakusudia, binadamu hao hao walifanya maamuzi mabaya ambayo yaliwagharimu matokeo mabaya. Mungu alipowamilikisha aliwapa sheria ya kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, na akawaonya kwamba siku watakapokiuka sheria hiyo, watavunja mahusiano na yeye, na pia watapoteza sio mamlaka ya utwala peke yake, bali wasitisha na maisha ya umilele duniani.
Adamu na Eva walipokiuka sheria ya Mungu; ghafla wakajikuta wamefarakana na Mungu kama livyoandikwa: “…kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;..” (Rum.3:23)
Kwa bahati mbaya, uvunjwaji wa sheria ya Mungu ulifanywa na binadamu wa kwanza wale wale ambao ndio walitakiwa kubaki mfano wa vizazi vya binadamu vinavyofuatia. Biblia imeandikwa kwamba:“Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa      dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote   wamefanya dhambi.” (Rum.5:12)
Kutokana na maandiko tunaona kwamba kwa kosa la binadamu kuliathiri vizazi vyote vya binadamu waliofuata baada yao. Na athari hazikuishia katika kupoteza utukufu wa Mungu, bali ulisababisha kunywang’anywa ile mamlaka ya utawala. Lakini Mungu atukuzwe kwa sababu hakuridhika na athari zilizomsibu binadamu bali aliandaa mpango maalum wa kumkomboa na kumrejesha katika asili yake ya kwanza. Mpango huu tutaupitia katika makala yajayo.
Mpango wa pili wa Mungu ukombozi wa binadamu
Baada ya binadamu wa kwanza kupoteza haki, mamlaka na fursa za kumiliki, na kusababisha athari mbaya za mapigo ya magonjwa na umaskini wa kipato; Mungu aliamua kuonesha upendo wake kwa binadamu kwa kumtuma Mwanawe Pekee ulimwenguni kama tunavyosoma: “Kwa maana jinsi hii, Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa       Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na zima wa milele.” (Yh.3:16)
Ujio wa Yesu Kristo duniani ulibeba misheni yenye mambo mawili muhimu ambayo binadamu aliyapoteza ambayo ni: i) Kurejesha mahusiano yaliyovunjika kati ya binadamu na Mungu ii) Kurejesha mamlaka aliyonyanganywa binadamu na Ibilisi.
Kwa habari ya kurejesha mahusiano yaliyovunjika kati ya binadamu na Mungu, Yesu Kristo alikuja akiwa kufanyika dhabihu ya dhambi iliyomtenga binadamu na Mungu kama ilivyoanidkwa:“Siku ya pili yake akamwoma Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama    Mwakandoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” (Yh.1:29)
Kupitia mateso na kifo cha Yesu Msalabani, Yesu aliupatanisha ulimwengu na Mungu kwa yeye kulipa fidia ya adhabau ya dhambi, tena ya kosa la binadamu wa kwanza. Lakini kwa Yesu kushuka kuzimu na kufufuka katika wafu kulisababisha kurejeshwa mamlaka zote zilizoporwa na Ibilisi pamoja na haki ya kumiliki.
Mtume Yohana aliyekuwa mwanafunzi aliyependwa sana na Yesu, anatusimulia katika Injili aliyoiandikwa akisema kwamba, ujio wa Yesu Kristo ulilenga kurejesha mamlaka ya kifalme kwa wote watakaomwamini Yesu Kristo:“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” (Yh.1:11)
Tendo la mtu kufanyika mtoto wa Mungu limebeba ahadi na mamlaka ya kumiliki mali za mfalme, ambaye ni Mungu Baba, kwa kupitia Mwanawe Pekee. Huwezi kufanyika mtoto wa mfalme ukaendelea kuishi maisha ya ufukara, labda kama unafanya igizo! 
Majibu ya maswali nyeti kuhusu nadharia ya kumiliki
Ninafahamu kwamba yako maswali sugu tena ya miaka mingi ambayo huulizwa na kila mwenye mashaka na nadharia ya kumiliki. Maswali hayo ni kama haya yafuatayo: i) Hivi huu Ukombozi wa Yesu Kristo kwa binadamu ni maisha ya sasa au siku ya kiyama? ii) Kwanini wengi wanaodai kumfuata Yesu Kristo maisha yao ni yale yale ya mateso na umaskini wa kipato? Iii) Je Yesu mwenyewe si alishasema kuwa ulimwenguni tunayo dhiki, na mitume wake nao wakathibitisha kwamba tunaingia mbinguni kwa njia  ya dhiki nyingi?
Majibu ya maswali haya ni muhimu sana kwa kila asomaye makala haya, na bila shaka atapata fursa ya kuzipima nadharia zilizopo na majibu yangu:
1.     Majibu ya ukombozi wa Yesu ni maisha ya sasa au siku ya kiyama?
Ukombozi wa Yesu Kristo kwa binadamu ni maisha ya sasa na kilele chake ni kunyakuliwa kwa kanisa duniani. Ukifuatilia kwa makini katika Injili zote kuhusu maisha ya Yesu Kristo duniani, utakuta alihubiri Injili ya ufalme iliyoambatana na udhihisho wa mamlaka ya kifalme katika kutatua matatizo sugu matatu: kusamehe dhambi, kuponya ulemavu na magonjwa yote; na kushughulikia mahitaji ya chakula yalipojitokeza.
Aidha, kanisa la kwanza lililoanzishwa na mitume jijini Yerusalemu nalo lilidhihirisha maisha ya kifalme kwa kuhakikisha watu wanatubu dhambi na kuzaliwa mara ya pili, kuponywa magonjwa yote, na kila aliyejiunga na kanisa hilo aliacchana na umaskini wa kipato. Kwa hiyo maisha ya ukombozi wa Yesu Kristo yanaanzia hapaa hapa duniani kama yalivyodhihirishwa na Yesu Kristo, mitume wake na wakristo wa kanisa la kwanza!
Hata hivyo, bado mchakato wa kumiliki unaendelea na utafikia kilele chake wakati Yesu Kristo atakapolichukua kanisa lake na kwenda kukaa nalo pale mahali aliposema anakwenda kuliandalia makao.
Kwa kusema haya, sipuuzii uhalisia wa mambo jinsi yanavyoonekana kwa macho hapa duniani kwa hivi sasa. Uhaalisia unaonesha jinsi ambavyo maisha ya wengi waitwao wachaji Mungu, wafuasi waamini wa Yesu ni duni na kujaa changamoto nyingi za kiuchumi. Mimi pia nimepitia maisha haya haya tangu mwanzoni mwa uchanga wa imani yangu katika Kristo na mapokeo niliyofundishwa hapo awali.
Naomba nijibu sio kama majivuno bali kwa unyenyekevu mkubwa kwamba, changamoto zote zinazoonekana hivi sasa, hazitokani na wala sio sehemu ya Injili ya Yesu Kristo na Mitume wake. Haya ni matunda ya ukengeufu wa karne nyingi huko nyuma ambao ulizalisha “Ukristo bandia” katika ulimwengu huu!
Nadharia ya kwamba, maisha ya dhambi na umaskini ndio dhiki za mkristo duniani mpaka Yesu atakaporudi mara ya pili; ni matokeo ya ukengeufu ule ambayo Yesu Kristo mwenyewe aliutabiri kuwa utakuja na kuwakumba walio wengi! Kumbukeni mfano wa ngano na magugu ambao Yesu aliwaambia waanfunzi wake na tafsiri aliyoitoa.
Ukristo bandia umeshika nafasi kubwa ulimwenguni kwa kuwaaminisha watu kuishi katika dhambi kisha kuungama na kuendelea maisha ya dhambi kanisani; badala ya kuzaliwa mara ya pili na kupokea   uwezo wa kushinda dhambi (wanaona  ni fahari kuitwa wenyedhambi)
Hata kwa wale wanaopokea neema ya kuujua Ukristo wa kweli, na kuzaliwa mara ya pili, kwa sababu ya mapokeo ya ukristo bandia, bado huendelea kuaminishwa kwamba, maisha ya umaskini wa kipato ni njia mojawapo ya utakatifu, na kwamba kumiliki uchumi ni tamaa za kiulimwengu. Kwa imani hii, huendelea kuishi maisha duni, ambayo matokeo yake walio wengi huiacha imani na kurudi duniani.
Lakini tukumbuke kwamba KANISA LA KWANZA kwa muda wa miaka 40 mfululizo, likiwa na zaidi ya washirika 30,000 lilidhihirisha maisha ya ukombozi wa Kristo duniani; dhambi ilikemewa, wagonjwa wote waliponywa, na hapakuwepo miongoni mwao hata mmoja aliyekuwa maskini wa kipato!
 2.     Majibu kuhusu dhiki iliyotajwa na Yesu na mitume wake
Neno hili “dhiki” limekuwa likitafsiriwa kinyume ili kuhalalisha maisha ya mikandamizo ya kipepo, nagonjwa na umaskini wa kipato kwa wachaji Mungu kanisani. Yametumika kama faraja lakini nyuma yake ni mbinu za adui za kufanya wahusika kuchukuliana na maisha haya kwa kudhani ni mapenzi ya Mungu wawe hivyo haoa duniani!
Kwa kifupi Maneno ya Matoleo ya Biblia za Kiingereza yaliyotumika kutafsiri neno hili “dhiki” ni “hard times” “persecutions” na “tribulations”! Tafsiri ya maneno haya ni “Nyakati ngumu”, “mateso” na “mateso makali” au adha! Hapa hatusomi habari za dhiki kuitwa “magonjwa” wala “umaskini uliokithiri”!
Baadhi ya maandiko ambayo yametumiwa sana ni kauli ya Yesu Kristo aliwapowambia kwmaba: “..Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” (YH.16:33)
Maana ya neno “dhiki” lililotajwa hapa ni upinzani mkali dhidi ya imani katika Kristo ;upinzani wenye kuambatana na vitisho, na mateso ya mapigo ya viboko, na vifungo  vya gerezani. Hii ndiyo dhiki aliyomaanisha Yesu. Isitoshe, Yesu aliwoanya pia wanafunzi wake kwamba sio kwamba watateswa kwa sababu ya imani yao kwake, bali hata kuuawa pia: “watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.” (Yh.13:2)
Baada ya Yesu kupaa, na mitume wake kuchukua nafasi ya kuhubiri Injili ambayo ilikuwa imepigwa marufuku na wakuu wa dini na dola, ndipo yalipotimia maneno ya Yesu Kristo ya kupatwa na “dhiki nyingi” ambazo zimetajwa na Luka alipoandika: “Wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.” (Mdo.14:22)
Majumuisho ya majibu ya maswali
Kama nilivyokwisha kuanisha hapa juu, nadharia ya kumilikisha ni urithi wa Agano Jipya kwa wote wanaomjia Yesu Kristo. Ukombozi wa Yesu Kristo unajumuisha msamaha wa dhambi, unaosababisha kufutwa kwa adhabu ya maradhi na umaskini wa kipato. Jamii ya waaminio imeahidiwa kuishi maisha ya kifalme duniani na kilele chake ni mbinguni Yesu atakapolichukua kanisa lake. Dhiki inayotajwa duniani sio umaskini wa kipato bali chuki na upinzani dhidi ya imani unaoambatana na vitisho na mateso ya kimwili pamoja na kuuawa inapobidi.
Ni kweli kabisa kwamba Mkristo halisi, kuna nyakati maalum ambapo atapitia kwenye mapito magumu ya kiuchumi; ikiwa ni mashambulizi ya ibilisi ambaye anajua uchumi ukiwa mikononi mwa Mkristo utatumika kubomoa ufalme wake. Hata hivyo, pamoja na ukweli kwamba Mkristo hupitia mapito magumu ya kiuchumi; bado mapito hayo nayo ni ya mpito pia; na wala sio kuwa huu ndio mfumo wa maisha ya Mkristo halisi duniani!
 

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni