Ni matumaini yangu msomaji wa blog hii ya amaninafuraha kuwa unaendelea kupata mafundisho sahihi kutoka kwa mtumishi wa MUNGU askofu mkuu wa WAPO Mission International juu ya falsafa mbalimbali kwa mujibu wa biblia sasa kazi kwako kuamini na kutendea kazi na ni imani yangu kuwa utafunguliwa na kuwa huru katika maisha yako ya kila siku.
Zaidi ya yote utaanza kumiliki kwa mujibu wa biblia sasa endelea kuungana na mtumishi wa MUNGU
Ikiwa Yesu
alibeba magonjwa
yetu yote kwanini
bado tunaugua?
Kama ambavyo kazi ya Yesu Kristo
msalabani ilivyovunja nguvu ya dhambi; hali kadhalika na magonjwa yote nayo
yalishughulikiwa kwa wakati mmoja, na kwa mara moja kama ilivyotabiriwa na
mtunga Zaburi alipotabiri akisema:
“Akusamehe
maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi,
akutia taji ya fadhili na rehema, ushibisha mema uzee wako, ujana wako ukarejezwa
kama tai;..” (Zab.103:3-5)
Maandiko haya yanatabiri waziwazi
kuhusu ujio wa Yesu Kristo na kazi ambayo angeifanya kwa ajili ya dhambi pamoja
na magonjwa. Anaweka bayana kwamba, dhambi itashughulikiwa 100% na magonjwa
nayo yatashughulikiwa 100%!
Hata kabla Yesu hajasulubiwa
msalabani alionesha mamlaka kamili ya kusamehe dhambi na kuponya magonjwa yote,
pamoja na kufukuza pepo wachafu ambao ndio mawakala wa magonjwa yote:
“Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo;
akawatoa pepo kwa Neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie
lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu,
Na kuyachukua magonjwa yetu.” (MT. 8:16, 17)
Maana
kamili ya Yesu kubeba magonjwa yetu, haina maana kwamba aliugua magonjwa yenyewe
alipokuwa juu ya msalaba. Maana yake hasa ni kwamba Yesu alipokuwa msalabani,
mwili wake ulibeba maumivu na mateso yatokanayo na aina zote za magonjwa ya
binadamu. Aliuhisi uchungu na maumivu ya aina zote ya binadamu wote, wa vizazi
vyote.
Kwa
njia hii, nguvu za magonjwa ziliharibiwa juu ya mwili wa Yesu, ili kwamba,
magonjwa yote yasitawale tena katika miili ya wote watakaoikubali na kuitambua
kazi aliyoifanya Yesu msalabani.Yesu
alipofufuka katika wafu, alifufuka na mwili mpya wa utukufu ambao, huo pia ni
ahadi kwa kila anayemwamini Yesu ataupokea baada ya maisha ya duniani kufikia
ukomo.
Mpango wa ukombozi wa Kristo, ni pamoja na kuishi maisha
yenye afya bora, pasipo magonjwa kabisa. Huu ni ukweli wa kibiblia tena kwa
Agano Jipya. Maisha huru mbali na magonjwa. Ukweli huu unaweza kuwa mgumu
kuuamini kwa binadamu wa kizazi hiki, lakini Neno la Mungu lenyewe halibadiliki
vizazi vyote.
Sasa turudi kwenye swali letu la msingi.
Ikiwa kweli Yesu alisulubiwa na kwa kupigwa kwake ili kila amwaminiye apate fursa
ya kuwa na afya njema pasipo maradhi; mbona bado magonjwa yanawaandama wale
waitwao wafuasi wa Kristo? Nilisema kwamba kuna sababu. Kila ugonjwa unapoingia
katika mwili wa binadamu una sababu. Kumbuka kwamba ugonjwa siyo sehemu ya
maumbile ya binadamu. Ndiyo maana unapoingia katika mwili wa binadamu
unasababisha maumivu, mateso, kero na usumbufu wa kiafya. Lakini kila uingiapo
ugonjwa kuna sababu. Na katika kujibu swali la msingi nitazitaja baadhi ya
sababu hizo kama ifuatavyo:
1.
Bado dhambi
imepewa nafasi ya kutawala
Sehemu ya makala iliyopita
nilichambua sababu za dhambi kuendelea kutawala hapa ulimwenguni, hususan kati
ya jamii ya wale wanaomwamini Yesu; kwamba ni “mtazamo ambao haujabadilika kuhusu nafasi ya dhambi ulimwenguni.”
Nilisema kwamba kama mtu hajabadili mtazamo wake kuhusu nafasi ya dhambi
ulimwenguni, na kwamba bado anaamini bado dhambi ingali na nguvu zake katika
maisha ya mwamini mpaka sasa, basi dhambi itaendelela kutawala kana kwamba Yesu
Kristo hajawahi kuja duniani na kusulubiwa msalabani.
Sasa tukisimamia katika ukweli
huu, tunapata jibu la leo la ni kwanini
bado magonjwa yanaendelea kutawala ulimwenguni. Kutokubadili mtazamo kuhusu
dhambi ndio mlango wa magonjwa nayo kuendelea kutawala pia? Haviachani kabisa.
Kama alivyosema: akusamehe maovu yako
yote na akuponya magonjwa yako yote; hali kadhalika, kama mtazamo wa
kuondolewa dhambi bado una mushkeli, magonjwa nayo yanafunguliwa mlango wa
kuwepo kwa sababu; kila mahali dhambi ilipo na magonjwa nayo hapo ndio mahali
pake! Kwa maelezo mengine, dhambi ni kivutio cha magonjwa. Labda nimnukuu Bwana
Yesu mwenyewe katika suala hili:
“Baada ya hayo
Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, angalia, umekuwa mzima; usitende
dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.” (Yh.5:14)
Hii ni mara ya pili kwa Yesu
kutamka kauli ya katazo la aliyesamehewa dhambi asitende dhambi tena. Mara ya
kwanza alimwammbia Yule mwanamke aliyekamatwa kwenye uzinzi akaletwa ili apigwe
mawe na iliposhindikana akaachwa huru na Yesu akamtamkia akisema: “usitende
dhambi tena”. Lakini katika maandiko haya Yesu anaongeza kusema madhara
yatokanayo na kuponywa magonjwa na kurudi katika maisha ya dhambi hatimaye
husababisha magonjwa makubwa zaidi kuliko yale yaliyokuwepo kabla. “usitende dhambi tena, lisije likakupata
jambo lililo baya zaidi….”
2. Mtazamo kuhusu
nafasi ya magonjwa katika miili yetu
Sababu ya pili ni “kutokubadili mtazamo kuhusu nafasi ya magonjwa” katika ulimwengu wa
sasa na katika maisha ya mwamini. Hapa ninachomaanisha ni kwamba, si kila
ugonjwa unaompata mwamini ni kwa sababu ametenda dhambi ya aina fulani. La
hasha.
Lakini kama mwamini kimtazamo bado
anafikiri na kusadiki kwamba “kuugua ni sehemu ya maisha yake” ;na “kwa sababu
bado anao mwili wa mauti” na kwa hiyo “kuugua ni lazima” kwake; basi kwa
mtazamo huo peke yake unatosha kuyaruhusu magonjwa kufanya makao katika mwili
wake! Hii ndiyo kweli tupu hata kama
inauma na kuudhi! Narudia tena, kama ilivyo kwenye “kutokubadili mtazamo kuhusu dhambi” kunaifanya dhambi iendele
kutawala; ndivyo ilivyo hata kwa magonjwa pia!
Narejea kusema tena ya kwamba,
japokuwa magonjwa mengine huwapata waamini kwa sababu ya kuishi katika dhambi
kimtazamo na kitabia; sio kila ugonjwa unatokana na dhambi. Lakini kuamini
kwamba ni wajibu kuugua ni mlango kamili wa kuita magonjwa yaje mwilini kwa
sababu yamekaribishwa na mhusika kwa hiari yake mwenyewe.
3. Mashambulizi ya Ibilisi ya kupima imani yetu
Sasa tunakuja kwenye sababu ya
tatu. Tumekwisha kupitia sababu mbili za mwanzo ambazo, kimsingi, chanzo chake
ni kutokana na mhusika binafsi.. Lakini sababu ya tatu hii ni mashambulizi
kutoka kwa Shetani na malaika zake. Tukumbuke kwamba, kama vile ambavyo bado Shetani
ameruhusiwa kuwajaribu/kuwashawishi waamini kwa habari ya dhambi; hali
kadhalika Shetani huyo huyo hutumia vitisho vya magonjwa ili kutikisa imani za
waamini.
Mashambulizi haya huwapata waamini
kwa muda fulani ili kujaribu ufahamu walio nao kuhusu “kazi iliyofanywa na Yesu
msalabani ya kubeba magonjwa yetu yote” na kwamba kwa muda wote ambao uhusiano
wetu na Mungu ni safi; Shetani hana mamlaka ya “kupandikiza magonjwa” yake
katika miili yetu.
Kimsingi, mashambulizi haya
yanapompata mwamini, kazi yake ni kutumia mamlaka ya Jina la Yesu kukemea,
kufukuza au kuamuru magonjwa hayo yasifanye makazi katika mwili wake. Narejea
tena hapa kwamba hili ni suala la “mtazamo wa mwamini” kukumbuka kwamba ugonjwa
hautakiwi kufanya makazi katika mwili wake kwa mujibu wa kazi iliyofanywa na
Yesu Kristo msalabani!
Na hapa ndipo penye changamoto
kweli kweli. Wengine wanatafsiri kwamba, pamoja na mashambulizi ya Shetani,
bado mtu wa Mungu na yule aliyejitoa kumtumikia Mungu kwa uaminifu; ati hapaswi
kuugua kwa namna yoyote. Pengine wenye mtazamo huu wamepitiliza kiasi.
Nasema wamepitiliza kiasi kwa
sababu tunayo maandiko yanayoweka waziwazi baadhi ya watumishi wa Mungu
walioshambuliwa na Shetani kwa magonjwa, na wengine wakanusurika hata kufa.
Lakini kwa maombi na rehema za Mungu wakapokea uponyaji na kurejea katika afya
zao tena. Baadhi yao ni hawa wafuatao:
“Erasto alikaa
Korintho. Trofimo nalimwacha huko Mileto, hawezi.” (2 Tim.4:20)
Huyu Erasto alikuwa mwamini na
mtumishi wa Injili pamoja na mtume Paulo. Wakiwa katika msafara wa Injili
akashambuliwa na ugonjwa na akalazimika kulazwa na kuachwa na wenzake. Haya
ushahidi wa maandiko mengine ni haya hapa chini:
“Lakini naliona
imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mtendakazi pamoja name; tena
ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu. Kwa kuwa alikuwa na shauku kwenu
ninyi nyote, akahuzunika sana, kwa sababu mlisikia ya kwamba alikuwa hawezi.
Kwa maana alikuwa hawezi kweli kweli, karibu na kufa; lakini Mungu alimhurumia;
wala si yeye peke yake, ila na mimi pia; nisiwe na huzuni juu ya huzuni.” (Flp
2:25-27)
Bila shaka kwa maandiko haya hapa
tumeuthibitisha ukweli wa mashambulizi ya magonjwa kutoka kwa Shetani. Kimsingi
Paulo mwenywe ameeleza waziwazi kwamba mara kadhaa walitaka kwenda mahali fulani
lakini Shetani akawazuia:
“Kwa hiyo
tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na
Shetani akatuzuia.” (1 Thes.2:18)
Kwa maandiko haya, tushuhudia
kwamba Shetani amekuwa mpinzani wa Mungu na watumishi wake; na amekuwa akiweka
vipingamizi vya kuzuia huduma za Injili zisiwafikie wengine wamjie Kristo.
Bila shaka msomaji unaweza
kuchanganyikiwa ukifikiri kwamba, kama Shetani anaweza kutupa magonjwa kwa
watumishi wa Mungu wakaugua mpaka kunusurika kufa; je hii sio kudhoofisha kazi
ya Yesu iliyofanyika msalabani? Kwa mtazamo wa haraka inaweza kutafsiriwa
hivyo. Lakini tukitafakari kwa kina tunaweza kuona kwamba, kushambuliwa na
shetani kwa magonjwa ni tofauti na mwenye aliyeshambuliwa kuyaruhusu magonjwa
hayo kufanya makao ya kudumu katika mwili wake.
Mashambulizi ya Shetani kwa
magonjwa huwa ni ya kitambo maalum; na kila akipingwa na kukemewa kwa mamlaka
ya Kristo pasipo kukoma lazima shetani atakimbia na magonjwa yake!! Pili, Mungu
alijua kwamba shetani ataleta mashambulizi kwa watumishi wake, na ndiyo maana
akamtuma Roho Mtakatifu na karama za kuponya magonjwa ili kumpinga shetani na
magonjwa yake. Ndio maana hao tuliosoma katika maandiko ya kuwa walishambuliwa
na magonjwa tunaona walipambana kwa maombi mpaka wakapokea uponyaji.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni