Falsafa ya
ukombozi kwa mujibu wa Biblia-2
UNGANA NA ASKOFU GAMANYWA KUJIFUNZA FALSAFA YA UKOMBOZI KWA MUJIBU WA BIBLIA.
Mapitio
kuhusu mambo makuu 3 ya UKombozi wa Kristo msalabani; Maana na sababu ya Yesu kufanyika dhambi. Leo tunaendelea na
mfululizo wa makala kuhusu nafasi ya dhambi katika ulimwengu wa sasa:
Muhutasari kuhusu
Maana na
sababu ya Yesu
kufanyika dhambi
Kwa mujibu wa maandiko ya
(2 KOR.5:21;1 PET. 2:24)
tuliweza kuona kuona ugumu wa Paulo alichoandika kuwa ni: “….Yesu asiyejua dhambi alimfanya kuwa
dhambi kwa ajili yetu;” na jinsi ambavyo Mtume Petro aliturahisishia
tafsiri akisema: “….Mwenyewe alizichukua
dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti…” Maandiko yote haya kwa pamoja yalitufundisha
kwamba:
a) Yesu alikubali kuhukumiwa adhabu kama
mkosaji lakini bila kosa kibinafsi
b) Yesu alikubali kubeba hukumu ya adhabu
kwa niaba yetu
c) Yesu alikubali “Nguvu ya dhambi” kuharibiwa
juu ya mwili wake
d) Yesu alikusudia kwamba “Nguvu ya dhambi”
isiendelee “kutawala katika miili yetu”
Aidha, maandiko ya Mtume Yohana katika
(Yh.8:34;Yoh.8:35; 1 Yh.3:8) yalitufundisha
sababu zilizomfanya Yesu kufanyika dhambi kwa ajili yetu ambayo ni Kutukomboa
kwenye utumwa wa dhambi na Kuzivunja kazi za Ibilisi ili asiwe na mamlaka juu
yetu. Leo tunaingia sehemu ya pili ambayo inashughulikia maswali magumu na
majibu makini kuhusu nafasi ya dhambi katika ulimmwengu wa sasa.
Kama Yesu alivunja nguvu ya dhambi
kwanini bado inaendelea kutawala ulimwengu?
Baada ya kutoa ufafanuzi kama
ilivyoanishwa hapo awali; mara yanakuja maswali mazito, magumu tena mfululizo
yenye kuhoji uhalisia wa maelezo yangu. Yanakuja maswali yakihoji kuwa 1. Kama
kweli Yesu Kristo aliihukumu na kuiharibu dhambi hiyo isiendelee kutawala
katika maisha yetu; kwanini bado dhambi inaonekana kuendelea kutawala katika
ulimwengu huu? 2. Kwanini wale tuitwao
kanisa la Kristo bado tunasumbuliwa na dhambi?
Kutokana na maswali magumu
yaliyotangulia kuna nadharia na dhana nyingi ambazo zimejaribu kutoa majibu ya
kuhalalisha ni kwanini mado dhambi inaonekana kuendelea kutawala. Baadhi ya
majibu hayo ni pamoja na:
a) Kazi ya Yesu Msalabani bado
haijakamilika kiuhalisia mpaka hapo tutakapoondolewa katika ulimwengu huu
b) Dhambi inaendelea kutawala katika miili
yetu kwa sababu bado tuna miili ya mauti na hatujavikwa miili ya utukufu
Ukiyatazama majibu haya, yanaonekana
kuwa na ushawishi mkubwa sana kwa mtu Yule ambaye anatafuta kisingizio cha
kuendelea kuishi katika maisha ya dhambi. Ni majibu yanayofariji na kuhalalisha
kutenda dhambi kwa visingizio vya kimaumbile. Lakini ukisoma maandiko
matakatifu na tafsiri zake sahihi, utagundua kwamba majibu haya yamefunika
udhaifu wa kiimani; na kuibatilisha kazi ya Kristo ambayo ilimleta hapa
duniani.
Naomba nianze kujibu maswali magumu kwa
kutoa majibu ya makini kwa mujibu wa maandiko yasemayo katika tafsiri yake
sahihi. Ninaomba kwamba, ukweli ubaki kuwa ukweli hata kama ni mgumu
kuutekeleza lakini usipindwe ili kukidhi udhaifu wetu. Jibu langu la kwanza
ambalo sitaki kumung’unya maneno ni hili.
a) Kazi ya Yesu ya kusulubishwa na kufa msalabani
kwa ajili ya dhambi zetu; ililenga “kuivunja nguvu ya dhambi isipate kutawala”
katika “miili yetu ya sasa ya mauti” na sio katika ulimwengu ujao tutakapovikwa
“Miili ya utukufu”!
b) Tangu dhambi ilipohukumiwa juu ya mwili
wa Yesu, haina nguvu zake za asili kama ilivyokuwa kabla ya Yesu Kristo
kusulubishwa juu ya Msalaba.
c) Swali kwamba ni kwanini bado dhambi
inaonekana kuendelea kutawala ulimwenguni, jibu lake ni kwamba; “bado wengi
wetu hatujabadili
mtazamo wetu kuhusu nafasi ya dhambi katika ulimwengu wa sasa”! Nasema
tatizo ni “mtazamo wetu” na sio
kwamba bado dhambi ina nguvu ile ile ya kutawala miili yetu!
Narudia tena. Kwa kuwa wengi wetu bado
hatujabadili mtazamo wetu kuhusu nafasi ya dhambi katika ulimwengu wa sasa; na
kwa sababu bado tunaamini kwamba dhambi bado ina nguvu ile ile kama kabla ya
Yesu kusulubiwa msalabani; basi kwa sababu hiyooooo ya kimtazamoooo ndio mlango
“unaoihuisha
dhambi” au “kuiruhusu dhambi” au ”kuipa
nguvu dhambi” izidi kuendelea “kutawala katika miiili yetu”!
Maandiko
yasemavyo na tafsiri yake
kuhusu nafasii ya
dhambi ulimwenguni
Kimaandiko katika Agano Jipya, na
ushahidi wa maisha ya mitume na Wakristo wa karne ya kwanza; Dhambi yenyewe
katika uhalisia wake haina nguvu kabisa. Lakini kwa mtazamo wetu, na hiari
hiari zetu binafsi; tumeendelea kuipa nafasi dhambi kuwa na nguvu. Nasema tena,
kutokana na mtazamo wako, au kwa itikadi yako vimeipa dhambi ruksa iendelea
kutawala katika maisha yako.
Baada ya kutoa majibu ya msingi, sasa
nataka kuyathibitisha majibu yangu kwa maandiko matakatifu ya Mitume wetu jinsi
ambavyo katika kizazi chao waliweza kuishi maisha ya udhidi dhi ya dhambi
katika ulimwengu wa sasa na kwenye miili
yetu hii ya mauti. Tafadhali soma kwa makini vifungu vya maandiko yafuatayo:
“Tuseme
nini basi, tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha, sisi
tuliofia dhambi tutaishije tena katika dhambi? Hamfahamu ya kuwa sisi sote
tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa
pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo
alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi
tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano
wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; mkijua neno
hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulubishwa pamoja naye, ili mwili wa
dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; kwa kuwa yeye aliyekufa
amehesabiwa haki mbali na dhambi…” (Rum.6:1-7)
“Maana kwa kule kufa kwake, aliifia
dhambi mara moja tu; kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo ninyi
nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na wlaio hai kwa Mungu katika Kristo
Yesu. Basi dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti,
hata mkazitii tamaa zake; wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha
za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya
kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki. Kwa maana dhambi
haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya
neema.” (Rum.6:10-14)
Mpendwa msomaji wangu, maandiko tuliyonukuu hapap juu, yameweka
waziwazi “nafasi ya dhambi” ya dhambi katika ulimwengu wa sasa, hususan katika
miili yetu hii hii ya mauti! Ukihesabu katika mistari hii utakuta neno “dhambi”
limetajwa mara kumi na moja. Katika hizo kumi na moja ziko sehemu tano ambapo
dhambi imetajwa kama kitu kisicho na nguvu tena, na kama kitu kisichostahili
kutawala tena katika maisha yetu. Hebu nikupitishe kwa haraka maandiko hayo
kama ifuatavyo:
a) “…sisi tuliofia dhambi tutaishije tena
katika dhambi?...” Tafsiri ya maandiko haya
maana yake ni “Kuwa ndani ya Kristo” maana yake ni “kutengwa mbali na dhambi”;
na kwamba kuendelea katika dhambi wakati umo ndani ya Kristo ni kinyume kabisa
na kazi ya Yesu iliyofanyika msalabani!
b) “…..utu wetu wa kale ulisulubishwa
pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;…” Tafsiri ya maandiko haya maana yake ni: Wakati Yesu alipokuwa juu ya
msalaba, utu wetu wa kale, kwa wakati huo huo ulihukumiwa juu ya mwili wa Yesu.
Kwa tukio hilo, makali ya dhambi yaliyokuwa yametawala katika miili yetu
yakavunjwa nguvu zake. Na kwa kila mtu atakayempokea Yesu Kristo nguvu ya
dhambi ibatilike katika maisha yake; na asiendelee kutumikishwa kwa mabavu na
nguvu ya dhambi!
c) “…..jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio
hai kwa Mungu katika Kristo Yesu…”
Tafsiri ya maandiko haya maana yake ni: walioko ndani ya Kristo, wajitambue kwa
imani, kwamba kwa habari za maisha ya dhambi wao wamekufa. Na badala yake utu
mpya, tabia mpya za kiungu view hai, na kuonekana kwa uhalisi mbele za Mungu
d) “….dhambi isitawale ndani ya miili yenu
ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake…” Tafsiri ya maandiko haya maana
yake ni kwamba, tunatangaziwa na kutahadharishwa, kuwa makini kutokuiruhusu, au
kuipana nafasi dhambi iendelee kutawala kwa sababu ya vishawishi vitokanavyo na
majaribu ya tamaa za mwili.
Kimsingi, hapa inaonekana
kwamba, japokuwa dhambi yenyewe kama dhambi kiuhalisia, haina tena nguvu ya
kutawala katika miili yetu; lakini upo uwezekano kwetu sisi wenyewe; kwa
mtazamo wetu tu kuiruhusu, kuifungulia dhambi milango ya maarifa ili
irudi na kutawala kama hapo awali. Ikitokea hivyo, kwa mujibu wa maandiko haya,
itambulike kwamba “sio maisha mapya ya ushindi dhidi ya dhambi yaliyokusudiwa
ndani ya Kristo” ; bali kwa mtazamo wetu tumeifufua dhambi kurejea na kuendelea
kutawala katika mwili wake.
e)
“…Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi,…” Tafsiri ya maandiko haya maana yake ni kwamba, dhambi haitatutawala.
Maana yake ni ile ile ikiwa imerejewa tena na tena, ya kwamba dhambi haipaswi
na haina nguvu za kututawala.
Kielelezo cha
imani cha kuvunja
nguvu ya dhambi
katika miili yetu
Baada
ya kupata ushahidi wa kubatilishwa kwa nguvu ya dhambi isiendelee kutawala tena
katika miili yetu; naomba sasa tupitie kwa ufupi kielelezo cha imani,
kilichoamriwa na Yesu Kristo mwenyewe na kutekelezwa na mitume wake. Kielelezo
hicho ni Toba na ubatizo!
Tukumbuke
Yesu Kristo mwenyewe baada ya kufufuka kwake aliwatokea wanafunzi wake na
kuwaagiza kwamba, wakaihubiri Injili ya ukombozi, na kila atakaiamini
itamlazimu kutubu (kubadili mtazamo kuhusu nafasi ya dhambi;) na kuiruhusu kazi
ya ukombozi wa Kristo ifanyike halisi katika
maisha yake. Maana ya Yesu kuagiza ubatizo, ni kwamba hii ndiyo njia
pekee ya kuonesha mfano wa kifo, mazishi na ufufuo wa Kristo katika maisha ya
kila anayemjia Yesu kwa imani.
Kwa
kuwa tendo la ubatizo ni tendo la kuzamisha, kuzika mtu ndani ya maji mengi,
Yesu aliliagiza liwe kielelezo cha kifo
mazishi na kufufuka kiroho na hatimaye kufufuka kimwili siku ya kiyama.
Sasa basi, tukirejea kwenye maandiko yetu yale yale Warumi. 6:1-7; 10-14; tunakwenda
kuthibitisha jinsi kielelezo cha toba na ubatizo kilivyo na uhusiano wa kiimani
na mchakato mzima wa Kusulibishwa, kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo..
a)
“…Yesu aliposulibiwa msalabani……” maana yake “…utu wetu wa kale ulisulubishwa
pamoja naye”
b) “…Yesu alipokufa msalabani……” maana yake “…tuliifia dhambi juu ya mwili wa
Yesu”
c) “Yesu alipozikwa….” Maana yake “…Tulibatizwa katika mauti yake….” Na “…Tulizikwa
pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika
mauti yake…”
d) “Yesu alipofufuka katika wafu…” maana yake “…tuenende katika upya wa uzima…”
e)
Kuishi kwake
Kristo mbele za Mungu maana yake “miili yetu isitumikie dhambi tena…”
Majumuisho
Tumejifunza kwamba, kazi
aliyofanya Yesu Kristo msalabani ilikuwa ni kuivinja nguvu ya dhambi isipate
kutawala katika miili yetu ya mauti na tuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi
katika ulimwengu huu wa sasa. Aidha, tumejifunza pia kwamba dhambi kuendelea
kutawala katika ulimwengu wa sasa na katika miili ya binadamu wa leo; sio kwa
sababu bado ina nguvu kama kablal Yesu hajasulibiwa msalabani; bali ni kutokana
na “kutokubadili mtazamo wetu kuhusu nafasi ya dhambi ulimwenguni, na kwamba
kwa njia hii,, tunaipa dhambi nguvu sisi wenyewe, na inatawala kwa ridhaa yetu!
Kisha tumeshuhudia kwamba toba na ubatizo ni kielelezo cha imani kinachoifanya
kazi ya Kristo iwe halisi katika maisha ya kila anayemwamini.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni