YESU NI JIBU

Jumatano, 23 Septemba 2015

MRITHI WA VIATU VYA MWANAINJILI ASKOFU DR MOSES KULOLA APATIKANA.

Huyu Ndiye Askofu Mkuu Mteule wa Kanisa la EAGT. Brown Mwakipesile! Ndie Ameshika nafasi ya aliyekuwa Askofu Mkuu Babu Moses Kulola.
Hatimaye mrithi wa kiti cha mwanzilishi wa kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT), Mwanainjili, Dk. Moses Samwel Kulola, aliyemaliza kazi yake na kutwaliwa, atajulikana amejulikana baada ya wachungaji kutoka kila kona ya nchi watakapokutana mjini Dodoma, katika mkutano mkuu utakaomchagua Askofu Mkuu wa Pili wa kanisa hilo la kiroho.
Kiti cha Askofu Mkuu wa EAGT, kimekuwa kikikaimiwa na Makamu Askofu, Asumwisye Mwaisabila, tangu, Askofu Dk. Kulola alipoimaliza kazi, alhamisi Agosti 29, mwaka 2013, na kwa mujibu wa katiba ya kanisa hilo, mwaka huu ni wa uchaguzi na tayari maaandalizi yote yamekamilika.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la EAGT, Mch. John Henry Mfuko, kuhusu mwelekeo wa uchaguzi, sifa za anayestahili kukikalia kiti hicho na matarajio ya wana-EAGT, katika kipindi hiki muhimu.
Mzee huyu aliyetembea na Askofu Kulola katika safari za Injili wakitaabika nyikani, jangwani na mstuni katika hali zote alisema:
“Tunaelekea Dodoma kumchagua Askofu wa pili wa kanisa letu. Nitaenda Dodoma…lazima niende. Uchaguzi wa wakati huu ni tofauti sana kwa kuwa watu wameomba na tunaendelea kuomba na mkono wa Mungu uko juu yetu.”
Kisha aliongeza: “Si Yesu alisema ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, bisheni nanyi mtafunguliwa? Tunakwenda kumpata yule aliyestahili kuliongoza kanisa na si kwa mazoea, ni yule ambaye ataliongoza kanisa kulingana na hitaji la sasa.”
Alisema; wakati wao Injili ilienezwa kwa mbinu tofauti na hali ilivyo sasa, wakati huu Kiongozi anayetakiwa wala si kwa kigezo cha elimu tu, bali ni yule atakayeongoza kwa vitendo kulipeleka mbele kanisa na si mtawala.
Mzee huyo wa Injili aliyezaliwa mwaka 1930, alisema kuwa Kiongozi wa anayestahili kuvaa viatu vya Askofu Kulola ni lazima akidhi malengo ya kikatiba ambayo ni kuhubiri Injili ya Yesu Kristo.
Pili; awe mtu atakayeliinua kanisa la EAGT na kuliletea maendeleo ya kiroho na kimwili, badala ya kujinufaisha yeye mwenyewe.
Tatu, awe mtu anayejitolea kuongoza wengine kwa vitendo akijitolea mapato yake kuwasaidia wenzake, sio mtawala ni Kiongozi.
Akasisitiza kuwa Askofu Kulola kamwe hakuwa mtawala bali alikuwa Kiongozi wa watu.
Sifa ya nne; alisema kuwa ni lazima mtu huyo awe ni yule anayeweza kueneza Injili na kuliinua kanisa la EAGT mbele ya jamii kwa njia ya habari, kwani hiyo ndiyo inayoweza kuwafikia mamilioni ya watu kwa dakika chache tu, badala ya watu kujilimbikizia fedha, wakati watu wanakufa dhambini.
Kiongozi huyo mkongwe katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake, Temeke, mkabala na Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, alisema kuwa hitaji la Injili kupitia vyombo vya habari ni muhimu sana wakati huu ili kukabiliana na wimbi la Imani potofu ambazo zinaenezwa kwa njia hiyo hiyo ya habari, hivyo kanisa ni lazima litumie vyombo hivyo kupeleka Injili iliyo sahihi.
Akitoa mfano alisema; Askofu Sylvester Gamanywa (WAPO MISSINON INTERNATIONAL) alifanya mkutano Mbeya na kuwafikishia habari mamiloni ya watu kwa muda mfupi sana kupitia vyombo vya habari na hiyo ndiyo Injili ya sasa.
Alipoulizwa nini mtazamo wake kuelekea uchaguzi, mwenyekiti huyo wa bodi ya wadhamini (chombo chenye dhamana ya mali za kanisa) alisema:
“Inaweza kuwashangaza watu sana kwani Mungu atajitwalia Joshua wa kuliongoza kanisa, anaweza kutoka katika kundi lisilotegemewa, kutoka watu wa chini tu ambaye amejitoa na anaonekana kujitolea kulitumikia kusudi la Injili na kuwajali wenzake.”
Alisema Mungu anakanuni zake, hanaangalii vigezo vya wanadamu kama elimu na mambo mengine, Yeye hulitazama kusudio lake, alimuita Petro akiwa mvuvi tu na akawa mtumishi wa Injili.
Alinukuu andiko la Biblia kwenye kitabu cha Matendo ya mitume 4:13; “Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kujua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa wakastaajabu, wakatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.”
“Kanisa la EAGT, linahitaji Kiongozi mwenye kuwa na Yesu, kama alivyokuwa Askofu Kulola,”alisema kiongozi huyo wa kiroho na kufafanua kuwa Kiongozi hupimwa kwa matendo yake. Kiongozi wetu tunayemtaka ni lazima awe mtu wa kuwarehemu wachungaji wa chini, awakumbatie na kuwasaidia, si kuwaswaga, huku akijilimbikizia mali tena zinazotokana na kanisa la EAGT.
“Wewe si umekuja kwangu, umeona maisha yangu, kanisa langu lipo pale Keko Juu katika ukumbi wa shule, Mungu akinisaidi nikipata kiwanja kingine nitafurahi kanisa likiwa tofauti na ukumbi ule nilioutoa kwa ajili ya ibada bure miaka yote.”
“Mimi nimekuwa mdhamini wa kanisa tangu lilipoanza 1991, vijana wengi tumewapokea wakiwa hawana kitu, lakini leo ni matajiri wakutupwa, wakati kanisa halina maendeleo kama taasisi. Mimi ni mzee na kama wanasema mvi ni hekima basi wasikie wana-EAGT.”
Alisema kuwa uchaguzi wa sasa ni wa tofauti kwa kuwa kwa mara ya kwanza kanisa linafanya uchaguzi bila ya kuwepo kwa mwanzilishi wake, tangu lilipoanzishwa mwaka 1991.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni