YESU NI JIBU

Jumatatu, 22 Septemba 2014

MAOMBI YA UREJESHO NA UKOMBOZI SEHEMU YA PILI MGUSO WA PILI (Second touch)

TOKA NDANI YA KABURI, FUNGUA SANDA ILI UWEZE KUSTAWISHWA.

Wiki jana nilikufundisha ni kwa namna gani BWANA anaweza kukugusa kwa mara ya pili na nilikutolea mfano juu ya yule mtoto wa mwanamke Mshunami ambaye alikuwa ndani ya jeneza tayari kwa kwenda kuzikwa lakini BWANA awezaye kutenda miujiza aliligusa jeneza na kumwambia kijana amka na ikawa hivyo.
Bado naendelea na somo hili na leo utakwenda kuangalia na  mfano wa mtumishi wa Mungu Lazaro, endelea...
Neno la Mungu linasema, “Basi mtu mmoja alikuwa hawezi  Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake.Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi. Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema Bwana, yeye umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia  alisema, Ugonjwa huu si wa mauti bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro. Basi aliposikia ya kwamba hawezi alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo. Kisha baada ya hayo akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena.Wale wanafunzi wakamwambia Rabi juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe nawe unakwenda huko tena?Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu.Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake.Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo akawaambia Rafiki yetu Lazaro amelala lakini ninakwenda nipate kumwamsha.Basi wale wanafunzi wakamwambia Bwana ikiwa amelala atapona.Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi Lazaro amekufa.Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na twendeni kwake.....Basi Yesu alipofika alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne.Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu kadiri ya maili mbili hivi na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani.Basi Martha akamwambia Yesu Bwana kama ungalikuwapo hapa ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa.Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka.Martha akamwambia najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.Yesu akamwambia mimi ndimi huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu yule ajaye ulimwenguni.....Bali wengine wao wakasema, Je! Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?Basi Yesu hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango na jiwe limewekwa juu yake.Yesu akasema liondoeni jiwe. Martha dada yake yule aliyefariki, akamwambia Bwana ananuka sasa maana amekuwa maiti siku nne.Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia.Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa amefungwa sanda miguuni na mikononi na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake. Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu na kuyaona yale aliyoyafanya wakamwamini.Lakini wengine wakaenda zao kwa Mafarisayo wakawaambia aliyoyafanya Yesu” Yohana 11:1-46
 Ni dhahiri kuwa vipo vifungo vingi vinavyofuata maisha ya watu wa Mungu waliokoka na vimekuwa vikwazo vizito ambavyo vinahitaji mguso wa pili ili vitoke.
MGUSO WA KWANZA
Katika mguso wa kwanza tunaona jinsi Yesu alivyomfufua Lazaro kutoka  kaburini maana Yesu Kristo yeye ndiye mwenye funguo za mauti na kuzimu sawa na neno hili, “Na aliye hai nami nalikuwa nimekufa na tazama  ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. Ufunuo 1:18
 Yesu Kristo  anafunguo za mauti na kuzimu na ndio maana  aliweza kumfungua Lazaro toka katika kaburi na mauti maana ni ahadi yake, “Nitawakomboa na nguvu za kaburi nitawaokoa na mauti ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Kujuta kutafichwa na macho yangu” Hosea 13:14
Yesu Kristo alipofika kaburini alimwita  Lazaro na kumwambia  atoke nje na mara Lazaro akatoka nje  yule aliyekuwa amekufa  yapata siku nne. Hivyo hata kama biashara, kazi na elimu yako  zimekufa leo zitafufuka maana mwenye funguo yupo tayari kukugusa.
MGUSO WA PILI
Katika mguso wa pili tunaona  mara baada ya kumwambia Lazaro atoke nje akawaambia wamfungue sanda alizokuwa amefungwa na wamuache aende zake, “Akatoka nje yule aliyekufa amefungwa sanda miguuni na mikononi na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia mfungueni, mkamwache aende zake”
Hivyo ni dhahiri kuwa BWANA atakuinua tena hata kama walikuangusha ili wapate  kukuangamiza huu ni wakati wako wa kuinuliwa ,” Hapo watakapokuangusha utasema, kuna kuinuka tena naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa” Ayubu 22:29
BWANA  anasema huu ni wakati wa kuinuka kiroho na kimwili ,baraka zako lazima ziinuke na ustawi wako lazima uinuke mali na zako pia.“Nami nitakatilia mbali uchawi  usiwe mkononi mwako wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana” Mika 5:12
Kama ambavyo sanda ya Lazaro ilivyofunguliwa ndivyo sanda ya uchawi na mikosi iliyofunga  mikono yako isishike pesa, biashara yako isifanikiwe itakatiliwa mbali na ndipo utakapo stawishwa tena .
BWANA  anasema nitakufungua na nitakuacha  uende zako  na wao waliokushusha,waliokufilisi, waliosema hautaolewa, waliosema hautazaa wala hutofauli masomo  yako nawaambia ya kuwa  mimi  BWANA Mungu wako nitakutoa nje na kukufungua hayo yote.
Kama ambavyo Yesu Kristo alisema Lazaro toka nje  ndivyo nasi leo tutakavyomwita Lazaro wetu atoke nje na akisha tumfungue sanda.
“Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka na kuziba mahali palipobomoka nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale” Amosi 9:11
BWANA  anataka tuinuke kiroho na kiuchumi na miguu iliyofungwa tuifungue kwa jina lake kama ambavyo  Lazaro alifungwa mikono, miguu na uso kwa sanda na ilikuwa na maana ya kuwa  pamoja na kufufuka bado asingeweza kutembea na kwenda popote maana amefungwa sanda.
Hivyo maisha ya Lazaro yakawa giza wala haoni mbele hivyo basi hata sisi yatupasa tufungue sanda zote ili  maisha yetu yatiwe  nuru.
“Mwenye haki atasitawi kama mtende  atakua kama mwerezi wa Lebanoni. Waliopandwa katika nyumba ya Bwana watasitawi katika nyua za Mungu wetu. Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, watajaa utomvu  watakuwa na ubichi” Zaburi 92:12-14
Yakupasa  usiogope wala kufadhaika maana upo  mguso wa pili na  utarejeshewa upya, “Utukufu wangu utakuwa mpya kwangu, na uta wangu hurejezwa upya mkononi mwangu”Ayubu 29:20
Pia hapatakuwapo na utasa katika nyumba yako,  Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba wala aliye tasa katika nchi yako na hesabu ya siku zako nitaitimiza” Kutoka 23:26
Magonjwa hayatainuka kwako , Nanyi mtamtumikia Bwana Mungu wenu naye atakibarikia chakula chako na maji yako nami nitakuondolea ugonjwa kati yako” Kutoka 23:25
Wachawina tunguli zao hawatakupata maana,  “Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! “ Hesabu 23:23



Bwana amenipa funguo lazima ufunguliwe katika mguso wa pili.“Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake  yeye atafungua wala hapana atakayefunga naye atafunga wala hapana atakayefungua” Isaya 22:22
Ni wazi kuwa huu ni wakati wa kuinuliwa lazima uinuke na ufungue  sanda katika kazi zako,ndoa yako na unatakiwa kusimama mwenyewe katika zamu yako kama ambavyo Isaka alisimama na kumlilia Mungu juu ya Rebeka mkewe na akapata mtoto, “Isaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia na Rebeka mkewe akachukua mimba”Mwanzo 25:21.
Hivyo maneno haya yafanyike chachu katika maisha yako na unapaswa kusimama uombe mbele za Mungu naye atakuitikia na sanda zote zitakuachia.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni