YESU NI JIBU

Jumamosi, 13 Septemba 2014

KAULI YA ASKOFU ZA ASKOFU GAMANYWA:


Ukiheshemiwa heshimika
Utangulizi
Leo nimeona niwasilishe makala ambayo ni kutathimini hali halisi ya tabia na mwenendo wa kila mtu binafsi pamoja na jamii kwa jumla. Na kitu ambacho natamani tukifanyie tathmini kwa kila mmoja wetu ni msamiati wa neno maalum lijulikanalo kama “heshima”! Nataka tulitafakari neno heshima katika maana zake na matumizi yake na kuchunguza ni kwa kiasi gani viwango vyake vinazingatiwa katika jamii ya kizazi hiki.

Na kabla ya kuanza kulitathmini, hebu kwanza tupate tafsiri yake pamoja na matumizi yake asilia. Kwa mujibu wa tafsiri ya Kiswahili sanifu, tunapata maana ya neno “heshima” katika maelezo kama ifuatavyo: 1. Thamani ya utu, utukufu, daraja la juu; 2. Staha, adabu, nidhamu; 3. Kitu anachopewa mtu Kama alama ya kuthaminiwa kwake

Msomaji mpenzi, ukifuatilia kwa makini maana ya “heshima” kwa kupitia maneno yaliyoainishwa hapa juu, unaweza kuigawa “heshima” katika aina kuu mbili za sifa.  Aina ya kwanza ni “sifa za nje” na aina ya pili ni “sifa za ndani.”

Aina ya kwanza ya heshima ya “sifa za nje” ndiyo inayosababisha wahusika kuonekana kuwa na “thamani ya utu”, au “utukufu” au kuwa katika “daraja la juu”. Mambo haya matatu ndiyo humfanya mtu “kujulikana na wengi katika jamii” (Public figure) au “kuwa maarufu” (famous). Kimsingi “kujulikana” na wengi na kuwa “maarufu” ndiko humfanya mhusika kupata “heshima ya hadhara” (reputation)

Kwa maelezo mengine, “sifa za nje” ni  mambo ambayo muhusika amefanikiwa kuyafanya baada ya kujipatia elimu, ujuzi na kufikia utendaji wa viwango vya ubora  vinavyotambulika na mamlaka husika. Kwa kifupi, “sifa za nje” hutokana na “mafanikio ya nje” na kumfanya mtu kuheshimiwa katika jamii.
Aina ya pili ya heshima ni sehemu ya “sifa za ndani” ambayo hutokana na “staha”, “adabu” na “nidhamu” Haya mambo matatu yanahusu tabia na mwenendo wa mtu binafsi kwa jinsi anavyohusiana na watu wengine wanaomzunguka.

Hizi “sifa za ndani” ndizo zinazo muwezesha muhusika baada ya kupata mafanikio ya “kujulikana” na kuwa “maarufu” kuendelea kujistahi na kustahi wengine, kuwa na adabu na nidhamu binafsi.

Hizi ni “sifa za ndani” ambazo hujenga tabia binafsi ya uadilifu na uaminifu na kuendelea kutunza heshima ambayo ni “thamani ya utu”, “utukufu” na “daraja la juu” katika jamii

Vyanzo vya heshima 
Msomaji mpenzi, kama tulivyokwisha kujifunza tafsiri ya msamiati wa neno “heshima”; tumeshuhudia kwamba yako mambo maalum ambayo ni chimbuko na vyanzo vya heshima. Mpaka mtu afikie kiwango cha “kuheshimiwa” mbele ya jamii, lazima awe amefanya mambo na kuonesha ufanisi unaozingatia viwango vya ubora. Baadhi ya mambo ambayo ni vyanzo vya mtu kuheshimiwa katika jamii ni pamoja na:

      1.Kipaji cha uongozi wenye ushawishi mkubwa katika utawala na utumishi wa umma
      2.Kipawa cha kiroho katika utumishi wa mambo ya dini
      3.Elimu ya juu na ujuzi wa kitaaluma
      4.Hekima na uwezo wa kumiliki mali na utajiri
      5.Vipaji maalum vya sanaa na michezo

Japokuwa vinaweza kuwepo vyanzo vingine zaidi katika kumfanya mtu “kuheshimiwa” mbele za jamii, lakini mambo haya matano niliyoyataja yamebeba uzito wa juu na uchambuzi wangu utalenga haya.

Tunao watu waitwao “waheshimiwa” kutokana na juhudi katika kujipatia elimu na ujuzi wakafanikiwa kupanda madaraja ya kitaaluma na hivyo wakajulikana na kuwa maarufu na hivyo “wakaheshimiwa” na jamii.

Tunao wengine ambao kupitia vipaji vya uongozi walivyojaliwa katika utumishi wa umma na kwenye madhehebu yetu ya dini, wamejikuta wamejulikana na kuwa maarufu na wanaitwa “waheshimiwa” kwa misamiati ya majina ya vyeo na madaraka waliyonayo katika jamii

Tunalo pia kundi la baadhi ya watu ambao wamejaliwa hekima na uwezo wa kufanya shughuli za za uzalishaji mali na kumiliki utajiri ambao umewafanya kujulikana na kuwa maarufu na jamii imewaheshimu kwa sababu hiyo.

Kana kwamba hii haitoshi, tunalo kundi la wenye vipaji vya sanaa na michezo ambao wameonesha uwezo na ubunifu na umahiri katika tasnia za burudani mbalimbali na kujikuta wamejulikana na kuwa maarufu, na kupata heshima mbele za jamii inayowazunguka.

Hawa wote, wamejulikana na kuwa maarufu, kupitia vyanzo nilivyovitaja, wakapokea heshima kuliko watu wengine.

Tishio la kujivunjia heshima
baada ya kuheshimiwa

Hapo mwanzo tumekwisha kuigawa heshima katika aina kuu mbili za sifa za nje na sifa za ndani. Bila shaka tunaweza kujiuliza ni “Heshima” ipi iliyo bora? Ni sifa za nje au sifa za ndani? Kwa tathmini naweza kusema kwamba “ubora wa heshima” ni muunganiko wa “sifa za nje” na “sifa za ndani”.
Hakuna “ubora wa heshima” unaotegemea sehemu moja pasipo nyingine. Heshima ya umaarufu na kujulikana hudumu tu iwapo wahusika watazingatia  tabia za kujistahi, adabu na nidhamu binafsi mbele za watu wanaowazunguka.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya, watu wengi wenye kupata heshima zitokanazo na sifa za nje, baada ya muda si mrefu sana hujikuta wanapoteza heshima zao mbele ya jamii. Na hata kama wahusika bado wanaendelea kujulikana na kuwa maarufu kwa kutegemea sifa za nje; lakini wanapoacha kujistahi, kuwa na adabu na nidhamu binafsi, tayari hupatwa na mmomonyoko wa maadili ambao huathiri “thamani ya utu” wao, na kuutia dosari umaarufu wao; na hata kudhalilisha “madaraja ya juu” waliyokwisha kujipatia mbele za jamii

Heshima ya mtu ili iwe endelevu, lazima ijengwe juu ya "sifa za ndani" ambazo hutokana na mtu kujizoeza katika mambo ya "staha, adabu na nidhamu" mambo haya ndiyo humjengea mtu tabia ya uadilifu na uaminifu!

Kwa bahati mbaya "waheshimiwa" wengi hutoa kipaumbele kwa "sifa za nje" ili kutengeneza umaarufu (reputation);  na kisha kupuuza uboreshaji wa "sifa za ndani" za "staha”, “adabu”, na “nidhamu"; ambazo kimsingi ndizo huifanya heshima kuwa bora (integrity)


Itaendelea toleo lijalo,

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni