KILA
JENEZA LILILOBEBA MAISHA NA USTAWI WA WATU WA MUNGU NDANI MWAKE,LITAWAREJESHEA
UHAI TENA.
Neno la Mungu linasema, “Baadaye kidogo alikwenda
mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na
mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti
anachukuliwa nje ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini
wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie.
Akakaribia, akaligusa jeneza wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, kijana
nakuambia, inuka. Yule maiti akainuka
akaketi akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote wakamtukuza
Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu na Mungu amewaangalia watu
wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi
zote za kando kando” Luka 7:11-17
Kwa kila jambo kuna
majira yake na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu hivyo kuna wakati wa
kuzaliwa na wakati wa kufa, kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka ,kuna
wakati kubomoa na wakati wa kujenga tena, kuna wakati wa kushushwa chini
vilevile kuna wakati wa kuinuliwa.
Hivyo napenda utambue juu ya nyakati hizi za kiimani
ambazo lazima tuzipitie katika maisha yetu ya kimungu aliye hai na ndizo zitakazosimama katika maisha yetu
daima.
Tambua ya kuwa katika kila kusudi la kimungu kuna mguso
wa pili nasi kwa imani katika Yesu kristo tunakwenda kuguswa tena katika mguso wa pili
na kila kilichokufa kitafufuka tena, aliyefungwa atafunguliwa tena na biashara
iliyondani ya jeneza itatoka tena.
MGUSO WA KWANZA:
Katika mguso wa kwanza Bwana Yesu Kristo anaingia katika
mji uitwao Naini lakini
alipokaribia lango la mji anakutana na watu wenye msiba wa kufiwa na mpendwa
wao.
Pamoja na msiba
huo wapo wengine walikuwana msiba magonjwa, madeni na pia uchungu mioyoni mwao.
Msiba huu unatokana na sababu ya kuwa kila walichokuwa
wakijaribu kukifanya kinakufa kwa kuzaa mapooza hivyo BWANA alipomwona yule
mama aliyefiwa, akamwonea huruma na akamwambia
asilie.
“Akakaribia, akaligusa jeneza wale waliokuwa wakilichukua
wakasimama.”
Huu ndio mguso wa
kwanza ambapo kijana aliyekufa na kubebwa na watu ndani ya jeneza na wakiwa njiani walikutana na Yesu langoni na
akaligusa jeneza.
Swali la kujiuliza Kwanini Yesu aligusa jeneza?, jibu
lake ni hili , jeneza ndicho kizuizi cha kwanza kinachomfanya aliye kufa
asiguswe moja kwa moja na Yesu Kristo ili apokee muujiza.
Hii ndio
maana ya jeneza, “Tazama mkono wa Bwana
haukupunguka hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia lakini
maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso
wake msiuone, hata hataki kusikia.” Isaya 59:1-2
Neno hili
linatudhihirishia ni nini maana ya jeneza ,ambapo ni dhambi na uovu ambazo
humziba mtu wa Mungu asiguswe na Yesu
Kristo.
Wapo watu wengi ambao ni
wakristo lakini wamo kwenye majeneza ya ulevi, uzinzi,uongo, dhuluma , fitina
na mambo yote yanayofanana na hayo , elewa ya kuwa majeneza hayo ni mazito na lazima yakutane na Yesu
Kristo katika mguso wa kwanza ili ayasimamishe yasiendelee na safari ya kwenda
makubirini maana mshahara wa dhambi ni mauti.
“Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa
milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Warumi 6:23
Mkristo lazima uache
kutenda dhambi maana huwezi kuendelea kufanya dhambi na ukataka kuona baraka za
Mungu , fahamu ya kuwa Mungu hadhihakiwi na apandacho mtu ndicho atakachovuna.
“Msidanganyike Mungu hadhihakiwi kwa kuwa cho chote
apandacho mtu ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake katika
mwili wake atavuna uharibifu bali yeye apandaye kwa Roho katika Roho atavuna
uzima wa milele.” Wagalatia 6:7-8
Hivyo yakupasa
usidanganyike ya kuwa unaweza kuwa na maisha ya dhambi ndani mwa kanisa na bado
ukapata baraka katika maisha yako, tambua ya kuwa hakuna atakayemwona Mungu katika maisha yake
ya sasa na ya baadaye asipokuwa na huo utakatifu
“Tafuteni
kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao;” Waebrania 12:14Hivyo huu ni wakati wako wa kuacha dhambi na kuokoka,“Kwa maana atakaye kupenda maisha na kuona siku njema auzuie ulimi wake usinene mabaya, na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya atende mema atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake husikiliza maombi yao bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya.” 1Petro 3:10-12
Hivyo kwa maneno haya ni
wazi kuwa katika mguso wa kwanza ndipo tunapookoka na kuanza maisha mapya ya
kimaombi. Hivyo zingatia kweli hii ya kuwa afichaye dhambi hatafanikiwa hata
kama ana mipango ya mafanikio bali yule
aziungamaye atapata rehema.
“Afichaye dhambi zake hatafanikiwa bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata
rehema.” Mithali
28:13.Na hapa msomaji wangu endelea kufuatilia sehemu ya
MGUSO WA PILI:
Yesu alipoona ya kuwa waliobeba jeneza lenye mwili wa kijana yule aliyekuwa amekufa wamesimamisha safari yao ndipo alipoligusa jeneza na kusema ,“..... Akasema kijana nakuambia Inuka.Yule maiti akainuka akaketi akaanza kusema. Akampa mama yake.” Luka 7:14-15
Katika mguso huu
wa pili tunaona muujiza wa kuinuka mara ya pili kutoka katika kifo maana
aliyekuwa amekufa amerejeshewa uzima na Yesu Kristo na ndipo alipoinuka tena kwani kilimchofanya kijana awekwe kwenye jeneza
ilikuwa ni nguvu ya mauti.
Mauti ni
nguvu ya kufisha ambapo Yesu Kristo anasema “Na aliye hai nami nalikuwa nimekufa na tazama ni hai hata milele na milele.
Nami ninazo funguo za mauti na za kuzimu” Ufunuo 1:18
Inawezekana katika mguso
wa kwanza umeumia lakini fahamu ya kuwa upo mguso wa pili wenye uwezo wa
kimungu wa kukufungua na kukuondoa katika bonde la vilio.
Huu ni wakati wa kutoka katika bonde la vilio kwa
kuamishwa na Yesu Kristo toka kwenye umasikini na taabu, hivyo ni lazima uamishwe
sasa kiroho na kimwili maana “Naye
alituokoa katika nguvu za giza akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa
Mwana wa pendo lake;” Wakolosai 1:13
Naye Yesu Kristo
alituokoa toka katika nguvu za mauti,magonjwa,madeni,mapepo,uchawi,utasa na
mateso mbalimbali na pia alituhamisha kutoka katika jeneza la mauti,magonjwa na
madeni na kutuingiza katika ufalme mwana wa pendo lake, baraka na
ustawi,uponyaji na uzima na pamoja na kustawishwa kiuchumi na kifedha.
Maana BWANA atageuza bonde la vilio kuwa bonde la baraka,”Wakipita kati ya bonde la vilio hulifanya kuwa chemchemi naam
mvua ya vuli hulivika baraka”Zaburi 84:6
BWANA anageuza na hata
sasa ageuze maisha yako wewe na watoto wako
na alete baraka na ustawi katika maisha yenu.
Kama ambavyo aliweza kugeuza mauti ya kijana ikawa uzima
na sasa atageuza ndoa zilizokufa ziinuke tena ,elimu zilizokufa ziinuke tena,kazi
zilizokufa ziinuke a na zipate uzima tele.
Pia atageuza
magonjwa yote yatoke kwako na upate uzima na mkono wake Kristo ukae thabiti
katika maisha yako ya kiroho na kimwili sawasawa ” Ambaye mkono wangu
utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu.,Adui hatamwonea, Wala
mwana wa uovu hatamtesa.Bali nitawaponda watesi wake mbele yake, Nitawapiga
wanaomchukia.” Zaburi 89:21-23Katika mguso wa pili mkono wake Kristo utakugusa na utakuwa thabiti kwako na mkono wake utakuletea nguvu ya kupata utajiri na heshima “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.” Kumbukumbu 8:18
BWANA anapotupa ukombozi
sharti aturejeshee tena uwezo na nguvu ili tupate kutawala kimwili na adui zako
hawatakuonea tena wala mwana wa uovu yaani wachawi na waganga ,wafunga majini
na awarusha mikosi hawatakupata tena.
BWANA anasema
hawatakutesa na wale waliokutesa wanakwenda kuteswa wao maana Yesu atawaponda
watesi wako na kuwapiga wanaokuchukia. Pia mguso huu wa pili utakuletea ustaei
wa kazi ya mikono yako, “Na
uzuri wa Bwana Mungu wetu uwe juu yetu na
kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti naam kazi ya mikono yetu uithibitishe”Zaburi
90:17.
Endelea kufuatilia mfululizo wa ujumbe huu kutoka
kwa mtumishi wa Mungu mch.Florian Josephat Katunzi.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni