Mwanamume alishangaza familia yake, marafiki na wanakijiji alipoamua
'kufunga’ ndoa na marehemu mkewe katika kijiji cha Kadzinuni, tarafa ya
Kikambala, Kaunti ya Kilifi (Mombasa),wakati wa mazishi yake.
Kiti Mwangudza Chilango aliamua kutimiza ahadi aliyokuwa amempatia mkewe
miaka michache iliyopita kwamba wawili hao wangefunga ndoa rasmi.
Akiwa amevalia suti, Bw Chilango alisimama kando ya jeneza la mkewe akiwa
pamoja na msafara wa wasimamizi wake sawa na jinsi inavyofanyika wakati wa
harusi.
Pia kulikuwepo na keki ambayo aliikata na kisha ikagawanywa kwa
waombolezaji kabla ya mwili kuzikwa.
Kulingana na rafiki wa karibu wa marehemu, Bi Mbeyu Mbura, Bw
Chilango alikuwa amemuoa kwa kitamaduni lakini mkewe alikuwa akishinikiza
wafanye harusi kanisani.
Bi Mbeyu alifichua kuwa marehemu ambaye alikuwa akiugua ugonjwa
usiojulikana alikuwa amemtaka mumewe aape kuwa atamheshimu kwa kumfanyia harusi
awe hai ama akiwa amekufa, na ndio sababu mumewe hakuwa na namna nyingine ila
kutimiza ahadi hiyo.
“Tunahofia kuwa kitu kibaya huenda kikatokea kwa mumewe ama familia ikiwa
ombi la marehemu halitatimizwa. Mumewe anaweza hata kufa,” alieleza Bi Mbeyu.
Mzee wa kijiji Kai Mwandeje alisema kuwa hakuna jambo kama hilo limewahi
kutokea eneo hilo na kusema kuwa kitendo hicho huenda kikaleta matatizo mengine
baadaye ikiwa mume ataamua kuwa anataka kuoa tena katika siku za usoni.
“Kuvalia mavazi ya harusi kunamaanisha kuwa roho ya mume tayari
imeunganishwa na ya marehemu. Itakuwa vigumu kuoa tena isipokuwa kama ahadi
hiyo itavunjwa,” alisema Bw Kai.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni