YESU NI JIBU

Jumatatu, 9 Februari 2015

KAULI YA RAIS OBAMA IMEZUA KIZAAZAA DUNIANI NA BAADHI WAHOJI KUWA KIONGOZI HUYO WA KWANZA MWEUSI WA MAREKANI NI MKRISTO:



Kauli ya Rais Barack Obama ya kuwataka Wakristo kujua kuwa Uislamu si dini pekee inayohusishwa na vurugu na mauaji, imezua kizaazaa duniani na baadhi wameanza kuhoji kama kiongozi huyo wa kwanza mweusi wa Marekani ni Mkristo.
Obama alitoa kauli hiyo Jumatano wakati wa Siku ya Taifa ya Maombi (National Breakfast Prayer) alipofananisha Vita vya Msalaba na vitendo vya ugaidi vinavyofanywa na vikundi vya Kiislamu vyenye imani kali.
“Hadi tutakapokuwa juu ya farasi na kufikiri kuwa jambo hili ni la pekee kwa baadhi ya sehemu, kumbuka kwamba wakati wa Vita Vitakatifu (crusades) na Mahakama ya Kanisa Katoliki (Inquisition), watu walifanya vitendo vya kutisha kwa Jina la Kristo,” Obama alikaririwa na Shirika la Habari la AFP akizungumza kwenye hafla hiyo Jumatano.
 “Na katika nchi yetu, utumwa na sheria za kibaguzi (Jim Crow), zote pia zilihalalishwa kwa jina la Kristo.”
Obama alikuwa akitoa hotuba yake kuhusu dini kwenye hafla hiyo iliyofanyika Washington, D.C. Akitumia maandiko ya dini za Kiislamu, Kiyahudi na kikristo, Obama alisifu imani yake.
“Utamaduni wa maombi umetuweka pamoja, ukitupa nafasi ya kukusanyika kwa unyeyekevu mbele ya Mungu na kutukumbusha nini kinatakiwa kushirikiana kama watoto wa Mungu,” alisema.
Obama pia aliwageukia magaidi wa kijihadi aliosema “wanaasi Uislamu”. Alilinyooshea kidole kundi la Islamic State ambalo alisema “limefanya vitendo visivyoweza kutamkwa vya ukatili “ Mashariki ya Kati pamoja na wanamgambo ambao hivi karibuni waliua watu kadhaa kwenye ofisi za gazeti la vibonzo la Charlie Hebdo nchini Ufaransa.
Lakini kauli yake imekosolewa sehemu mbalimbali.
Katibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Saba Raymond alisema alichozungumzia Obama ni historian a hivyo dunia inatakiwa ijifunze.
“Kama kimetokea, kimetokea. Tunatakiwa kujifunza kutokana na kilichotokea. Katika ulimwengu wa sasa ni fursa ya kujifunza yale yaliyotokea na hayafai na wakati huu yasitokee tena... wale wanaoyataka, washindwe,” alisema Padri Raymond
Padri Raymond aliongeza kusema: “Utumwa ulikuwa haufai na Marekani walijihusisha kwa hili (kuuondoa) na hii ni historia ambayo wanapaswa kuiacha.”
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema:” Ni kauli ya kujihami na anaogopa kuwanyooshea kidole moja kwa moja... Wamarekani wasingependa yatokee kama yaliyowahi kutokea huko nyuma.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni