YESU NI JIBU

Jumamosi, 13 Desemba 2014

Ukiheshemiwa heshimika-2 ungana na askofu mkuu wa WAPO Mission International na makala haya:



Katika toleo lililopita tulianza mada mpya ya “ukiheshimiwa heshimika” ambapo tulichambua maeneo matatu yaliyojumuisha “Utangulizi”; “Vyanzo vya heshima”; na “Tishio la kujivunjia heshima baada ya kuheshimiwa”! Leo tutaingia katika sehemu muhimu ya sababu kubwa ya kibibilia ambayo husababisha wengi wanaofanikiwa na kuheshimiwa hupoteza heshima zao katika jamii:
Mtazamo wa Yesu kuhusu kujikinai
na kuacha kuheshimika

Bwana Yesu aliwahi kuongelea tatizo la hali ya kujikinai baada ya kufanikiwa kiasi cha kudhani mafanikio ni “kibali cha kuishi milele duniani”! Katika kuweka mkazo kuhusu tabia hii, Yesu alitoa mfano wa mtu mmoja tajiri aliyeonesha kujikinai kwa utajiri wake na kutamba kuishi duniani bila ukomo:
 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.  Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;  akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.  Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.  Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.  Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?  Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu. “ (LK. 12:15-21)

Kwa kupitia maandiko haya, unaweza kusoma baadhi ya kauli za tajiri jinsi alivyojikinai akisema: “….ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi…” Kumbuka kwamba huyu tajiri hakuupata utajiri wake kwa njia za ufisadi. Aliupata kwa njia halali kabisaaaa. Alilima shamba lake “likazaa sana…”

Aidha, mpango wa kujenga ghala za kuhifadhi mali zake haukuwa jambo baya hata kidogo! Tatizo lake lilikuwa ni kujikinai, na kujisahau, kwa kufikiri kwamba alifikia kilele cha mafanikio hayo kwa nguvu zake binafsi na kwamba uhai wake utalindwa na wingi wa mali zake!

Ni upumbavu kuacha nyuma mali nyingi
uondokapo badala ya kuzitanguliza uendako
Kutokana na maneno ya Yesu, inaonesha kwamba tabia ya kukusanya na kijilimbikizia mali nyingi kisha ukaondoka na kuziacha bila kuzifaidi ni “Upumbavu”! Kwa mujibu wa maneno ya Yesu ni kwamba upumbavu huu hauishii katika kujilimbikizia peke yake, bali kushindwa kuzitumia mali kwenye mambo ya ufalme wa Mungu; na matokeo yake mhusika kuondoka duniani ghafla na mali zake kuchukuliwa na wengine wasiozitaabikia tangu mwanzo:

“….Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?  Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu..”

Uchunguzi wangu wa kimaandiko katika mada hii, nimebaini kwamba, kujikinai sio kujisifia utajiri peke yake, wala sio kumsahau Mungu peke yake, bali ni matumizi ya utajiri wenyewe ambayo Yesu amesema kwamba   “….ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu. 

Mambo mawili muhimu hapa. Kwanza, ni tatizo la kujilimbikizia akiba isiyo na matumizi bali imekaa tu kwenye hifadhi yake. Pili, kukataa kutumia akiba ya mali katika vipaumbele vya Mwenyezi Mungu alivyoamuru kwa wale wanaomiliki mali nyingi!

Yesu aliposema “kujitajirisha kwa Mungu” maana yake halisi kwa tafsiri ya toleo la Biblia ya Kiingereza cha Amplified limesema: “So it is with the one who continues to lay up and hoard possessions for himself and is not rich his relation to God…..”  Haya maneno ya “…to lay up and hoard possessions…” yana maana ya kukusanya na kujilimbikizia..” Maana yake na ulimbikizaji ambao matumizi yake hayana mchango wa uhusiano na huduma za kimungu.

Katika uchambuzi huu kuhusu mfano wa Yesu tunajifunza mambo muhimu yafyatayo:

1.        Tishio la mali kuchukuliwa na wengine

Mtazamo wa kujilimbikizia mali nyingi ili hatimaye ndipo mkusanyaji apate kuzifaidi hapo baadaye si kitu kipya. Yupo mchaji Mungu aliyepata kuwa tajiri sana kuliko wengi duniani, ambaye alifanya utafiti kuhusu hatma ya utajiri ambapo alihitimisha kwa kusema hayo nayo ni ubatili:

"Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata.  Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonyesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili."(MHU. 2:18, 19)

Kuna maneno haya “……kazi yangu yote niliyojisughulisha nayo chini ya jua,…..” “……..sina budi kumwachia yeye atakayenifuata…….” “…… atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo…….” hayo nayo ni ubatili.”

Aliyeandika haya ni mfalme Sulemani ambaye alijikusanyia mali na utajiri mwingi kuliko matajiri wote wa ulimwengu waliowahi kuwepo kabla na baada yake. Ushahidi mwingine wa utafiti wa Mhubiri unapatikana katika maandiko yafuatayo:

“Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu.” (MHU. 2:21)

Katika maandiko haya tunakutana na maneno haya.. “….Mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na maarifa, na kwa ustadi….” “…….naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake…”

Hili jambo lilimchanganya sana Sulemani. Mtu anakusanya mali nyingi kwa muda mrefu na nguvu nyingi, akisha kufikia kilele cha ulimbikizaji kabla hajazifaidi anaondoka ghafla, na mtu mwingine anazichukua bila kuzitaabikia!!

2.        Kufananishwa na Mpumbavu

Yesu anamtaja tajiri Yule kuwa “Mpumbavu”! Ukifuatilia kwa makini Bibilia inamtafsiri “mpumbavu” ni mtu yeyote asiyetambua uwepo wa Mungu:

“Mpumbavu amesema moyoni, hakuna Mungu; wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, hakuna atendaye mema.” (Zab.14:1)

Hivi ndivyo Yule tajiri mkulima alivyoonnesha upumbavu wake ambapo Yesu aliutafsiri kwamba ni “dhana potofu ya uzima wa mtu kuwa katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo..”

3.        Jinsi ya kuweka akiba yenye tija ya milele

Haya basi, baada ya kuuthibitisha hasara ya kujilimbikizia mali na kisha kufa ukaziacha na kuondoka patupu, Yesu alipendekeza njia ya kunufaika na mali za duniani hata baada ya kuondoka duniani ni kuhakikisha matumizi ya mali hizo yanatoa kipaumbele kwa mambo ya ufalme wa Mbinguni:

“Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi hujunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.” (Mat.6:19-21)

Katika maandiko haya, ukiyatafsiri kwa mtazamo wa mfano wa tajiri aliyejilimbikizia mali kibinafsi, utagundua maana kama ifuatavyo: Kwanza, kukusanya mali na kuzitumia kwenye mambo ya ufalme wa Mungu ndiyo njia pekee ya kulimbikiza mali mahali salama kwa maana kwamba mali zinakutangulia uendako badala ya kuziacha nyuma yako uondokapo.

Majumuisho kuhusu kujikinai na kupoteza heshima

Watu wengi hutumia nguvu na muda mwingi katika kutafuta mafanikio kwa njia mbali mbali. Baada ya kufikia mafanikio na wahusika kupata kutambuliwa, na kupata umaarufu na heshima kutokana na mafanikio waliyoyapata, ghafla hubadilika kitabia na kupotesha heshima ile ile waliyokuwa wameipata kutokana na kazi kubwa waliyokwisha kuifanya.

Moja wapo ya tabia mbaya inayopoteza heshima ni kujikinai na kudhani kwamba, mafanikio hayo ni juhudi binafsi na Mungu hana sehemu wala jamii inayowazunguka. Kimsingi hakuna mtu afanikiwaye yeye peke yake kwa juhudu zake binafsi, pasipo ridhaa ya Mungu, na pasipo mikono ya watu wengine kuhusika kwa njia moja au nyingine. Hata kama maono, mipango na mikakati ya utekelezaji imebuniwa na mtu mmoja; bado ufanisi wake lazima hujumuisha wengi hata kama waliohusika walifanya hivyo kwa malipo.

Aidha, ni upumbavu wa hali ya juu, pale ambapo mtu afikiapo mafanikio ya kiuchumi, kufikiri kwamba ataishi milele duniani ili kunufaika kibinafsi na utajiri aliojilimbikizia hapa duniani. Tunao ushahidi wa maelfu ya watu wengi ambao kwa muda fulani walifanikiwa katika kumiliki uchumi na kupata umaarufu lakinii ghafla wahusika wakatoweka ghafla kwa maradhi yaliyooshindikana kutibika japokuwa walikuwa na mali nyingi. Mali zile hazikuwasaidia kudhibiti na kurefusha maisha yao, wakaondoka pasipo kutaka.
Kana kwamba hii haitoshi, watu wengi waliojilimbikizia mali nyingi, wanapoondoka ghafla haichukui muda mrefu hata na mali zile walizohifadhi huangukia mikononi mwa watumiaji wasio na uchungu nazo, na kisha kutoweka na kubaki historia tu.
Matokeo haya, ya kujikinai na kuishia kupoteza heshima ni changamoto kwa jamii ya kizazi cha wanaofanikiwa katika karne hii ya ishirini na moja. Katika toleo lijalo tutapitia kwa kina matumizi mabaya ya mali na utajiri na athari zake kwa wahusika pamoja na jamii kwa jumla.

Itaendelea toleo lijalo,

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni