Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue akifafanua moja ya swali lililoulizwa kutoka kwa mmoja
Waandishi wa habari (hayupo pichani) kuhusiana na suala zima la kusimamishwa
kwa Mkurugenzi wa NIDA,katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika Ikulu
jijini Dar es Salaam mapema leo, kuhusu uamuzi wa Rais Magufuli kutengua uteuzi
wa Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu.
Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue akizungmza katika mkutano na waandishi wa habari, Ikulu Dar
es Salaam leo, kuhusu uamuzi wa Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa
NIDA, Dickson Maimu
1.1 Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametengua
uteuzi wa Bwana Dickson E. MAIMU, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa kuanzia leo, tarehe 25 Januari, 2016.
1.2 Aidha, baada ya utenguzi huo, Bwana Dickson E. MAIMUamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, pamoja na wafuatao:
1.2.1 Bwana Joseph MAKANI, Mkurugenzi wa TEHAMA
1.2.2. Bi Rahel MAPANDE, Afisa Ugavi Mkuu
1.2.3 Bi Sabrina NYONI, Mkurugenzi wa Sheria
1.2.4 Bwana George NTALIMA, Afisa usafirishaji
1.3 Taarifa zilizomfikia
Rais zinaonesha kuwa NIDA hadi sasa imetumia Sh.179.6 bilioni. Kiasi hiki ni
kikubwa na Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizi
zilivyotumika, maana Rais amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na
kasi ndogo ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
1.4 Hivyo, Rais ameelekeza
Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa
manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA.
1.5 Rais pia ameelekeza
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu
za NIDA, ikiwemo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha
idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.
1.6 Rais vile vile
ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ifanye uchunguzi
kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.
2.0 Wizara
ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa
2.1 Aliyekuwa Naibu Waziri
wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Serikali ya Awamu ya
Nne, Mhe. Mahadhi Juma MAALIM ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania
nchini Kuwait, kufuatia uamuzi wa Serikali kufungua Ofisi ya Ubalozi katika nchi
hiyo rafiki.
2.2 Rais ameagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika
Mashariki na Ushirikiano wa Kianda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja
Mabalozi wawili ambao mikataba yao imeisha. Leo hii Mabalozi hao wanatakiwa
kukabidhi kazi kwa Afisa Mkuu au Mwandamizi aliye chini yao. Mabalozi hao ni:
2.2.1 Bi Batilda Salha BURIANI, aliyeko Tokyo, Japan
2. 2.2 Dkt. James Alex MSEKELA, aliyeko Rome, Italia.
2.3 Rais amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London,
Uingereza, Bwana
Peter Allan KALLAGHE. Anarejea Wizara ya
Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa
atakapopangiwa kazi nyingine.
2.4 Kwa maana hiyo, vituo vya Ubalozi vifuatavyo viko
wazi:
2.4.1 London, kufuatia kurejea nchini kwa Balozi Peter A. KALLAGHE
2.4.2 Brussels, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Deodorous KAMALAkuchaguliwa kuwa Mbunge.
2.4.3 Rome, Italia, kufuatia kuisha kwa
mkataba wa Dkt. James Alex
MSEKELA.
2.4.4 Tokyo, Japan, kufuatia kuisha kwa
mkataba wa Bibi
Batilda BURIANI
2.4.5 Kuala Lumpar, Malaysia, kufuatia
aliyekuwa Balozi, Dkt. Aziz Ponray MLIMA, kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa.
2.4.6 Brasilia, Brazil, kufuatia kustaafu kwa
aliyekuwa Balozi, Bwana Francis
MALAMBUGI.
3.0 Tawala za Mikoa
3.1 Rais ametengua uteuzi
wa Eng. Madeni Juma KIPANDE kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu
Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
4.0 Utumishi wa Umma
3.2 Nachukua nafasi hii
kuwahimiza viongozi wote katika Utumishi wa Umma, na watumishi wote wa umma,
kubadilika kwa dhati kwenye utendaji wao na uadilifu wao.
3.3 Napenda kusisitiza
kuwa Rais na sisi tunaomsaidia hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na
watumishi wengine. Tungependa kila mtu mwenyewe ajirekebishe na kutomfikisha
Rais mahali ambapo inabidi amchukulie hatua. Mambo yafuatayo ni muhimu:
4.2.1 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu isipate
kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi.
4.2.2 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu asipate
kigugumizi kuchukua hatua za nidhamu, lakini afanye hivyo kwa kuzingatia kwa
ukamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma.
4.2.3 Lazima uongozi na watumishi wa umma
wawahudumie wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima. Kwa sababu hiyo:
a) Kila ofisi ya Serikali iwe na dawati la kusikiliza
shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
b) Kwenye kila Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya
wajenge uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu na kwa wakati.
Kwa muundo wa Serikali yetu hakuna sababu kwa mwananchi kufunga safari mpaka
Ikulu Dar es Salaam kwa kuamini kuwa ni Rais tu anayeweza kumaliza matatizo
yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila pembe ya nchi yetu. Ikibidi wananchi
wafike Ikulu ina maana hao wawakilishi wa Rais hawakutimiza wajibu wao.
c) Kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae majina yao
ili iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi
wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati, na kumtolea taarifa
yule anayefanya mambo ya hovyo.
d) Kila ofisi ya Serikali iwe na utaratibu wa kupokea maoni ya
wananchi kuhusu huduma inayotolewa kwenye ofisi hizo, na kushughulikia haraka
maeneo yote ambayo wananchi wataonesha kutoridhika na huduma.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
25 Januari, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni