YESU NI JIBU

Jumatano, 8 Juni 2016

KAULI YA MWANGALIZI MKUU WA WAPO MISSION INTERNATIONAL WAKATI WA KUKUMBUKA SIKU YAKE YA KUZALIWA:

Tarehe 6 mwezi wa sita mwaka huu 2016 ni siku ya kumbukumbu ya  kuzaliwa kwa Askofu wa huduma yaBCIC na mwangalizi wa WAPO mission Askofu Sylivester Gamanywa, ambaye ameandika ujumbe ufuatao kwenye akaunti yake ya facebook.
SIKU NA MWEZI KAMA LEO NILIZALIWA DUNIANI!

miaka 59 iliyopita nilifurahia sana birthday yangu nikiwa na raha ya kuongezeka umri! leo ninajishangaa sina tena furaha ya kuongezeka umri kama zamani!
hii ni baada ya kubaini kuwa kwa kadiri umri wangu tangu kuzaliwa unavyoongezeka kama siku ya leo; kumbe muda wangu wa kuendelea kuishi duniani unapungua!
sio kwamba naogopa kufa la hasha; naogopa kumaliza muda wa kuishi duniani kabla ya kumaliza kusudi la mungu lililonileta duniani!
nikitafakari muda wa kuishi uliobakia na maono ya kutimiza kusudi la mungu naona muda uliobaki ni mfupi kuliko majukumu yaliyoko mbele yangu!
hali hii imenilazimisha kujiwekea mpango mkakati wa matumizi ya muda uliobaki ili kutimiza hilo kusudi kabla muda haujaisha!
hivi sasa ratiba yangu imejaa majukumu ya lazima tu tena ni yanayohusiana na wito na maono peke yake!
kuanzia marafiki mpaka ndugu na jamaa zangu wote kama hatuna uhusiano unaonisaidia na kuchangia katika kutimiza wito na maono yangu, ninasikitika sina muda nao kama nilivyokuwa zamani!
nimejikuta naungana na bwana yesu alipowaambia mama yake na ndugu zake akisema, wale walioko pamoja naye na kumsikiliza na kutoa kipaumbele kwa mambo ya ufalme wa mungu baba yake hao ndio mama na ndugu zake!
hata humu humu kwenye mitandao ya kijamii simo kwa sababu ninatafuta kuburudika kwa michapo ya mitaani. nimo humu “kikazi” na “kimaono”!
hivi ndivyo ninavyoipokea kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu!
naona birthday yangu imekazana kunipunguzia muda wa kuishi katika kutimiza wito na maono ya kusudi lililonileta duniani!
lakini hata kama muda uliobakia unatishia kuisha upesi, kwa imani katika yeye aliyenileta duniani nimepania kwa dhati kutokuondoka kabla sijatimiza kusudi la kuzaliwa kwangu!
na katika hili ninahitaji dua, sala na maombezi kutoka kwa kila mmoja wenu ili nimalize vema na kwa ushindi wa kishindo kwa ajili ya utukufu wa Mungu Baba!

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni