YESU NI JIBU

Jumatano, 22 Januari 2014

ENDELEA NA FALSAFA MILIKISHA KWA MUJIBU WA BIBLIA KAMA UNAVYOLETEWA NA ASKOFU GAMANYWA SEHEMU PILI

Falsafa ya umikilishaji kwa mujibu wa Biblia

Katika toleo lililopita tulianza hoja hii kuhusu falsafa ya kumilikisha kwa mujibu wa Biblia. Aidha, tulipitia vipengele vya Mpango wa kwanza wa Mungu kwa binadamu na jinsi ulivyolenga kumfanya binadamu kutawala nchi na vitu vilivyomo. Kisha tukapitia anguko la binadamu wa kwanza na athari zake. Sasa katika toleo hili tunaendelea na sehemu ya pili kuhusu mpango wa pili wa Mungu wa ukombozi wa binadamu na matokeo yake:

Mpango wa pili wa Mungu ukombozi wa binadamu
Baada ay binadamu wa kwanza kupoteza haki, mamlaka na fursa za kumiliki, na kusababisha athari mbaya za mapigo ya magonjwa na umaskini wa kipato; Mungu aliamua kuonesha upendo wake kwa binadamu kwa kumtuma Mwanawe Pekee ulimwenguni kama tunavyosoma: “Kwa maana jinsi hii, Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na zima wa milele.” (Yh.3:16)
Ujio wa Yesu Kristo duniani ulibeba misheni yenye mambo mawili muhimu ambayo binadamu aliyapoteza ambayo ni: i) Kurejesha mahusiano yaliyovunjika kati ya binadamu na Mungu ii) Kurejesha mamlaka aliyonyanganywa binadamu na Ibilisi.
Kwa habari ya kurejesha mahusiano yaliyovunjika kati ya binadamu na Mungu, Yesu Kristo alikuja akiwa kufanyika dhabihu ya dhambi iliyomtenga binadamu na Mungu kama ilivyoanidkwa:“Siku ya pili yake akamwoma Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama Mwakandoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” (Yh.1:29)
Kupitia mateso na kifo cha Yesu Msalabani, Yesu aliupatanisha ulimwengu na Mungu kwa yeye kulipa fidia ya adhabau ya dhambi, tena ya kosa la binadamu wa kwanza. Lakini kwa Yesu kushuka kuzimu na kufufuka katika wafu kulisababisha kurejeshwa mamlaka zote zilizoporwa na Ibilisi pamoja na haki ya kumiliki.
Mtume Yohana aliyekuwa mwanafunzi aliyependwa sana na Yesu, anatusimulia katika Injili aliyoiandikwa akisema kwamba, ujio wa Yesu Kristo ulilenga kurejesha mamlaka ya kifalme kwa wote watakaomwamini Yesu Kristo:“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” (Yh.1:11)
Tendo la mtu kufanyika mtoto wa Mungu limebeba ahadi na mamlaka ya kumiliki mali za mfalme, ambaye ni Mungu Baba, kwa kupitia Mwanawe Pekee. Huwezi kufanyika mtoto wa mfalme ukaendelea kuishi maisha ya ufukara, labda kama unafanya igizo!
Majibu ya maswali nyeti kuhusu falsafa ya kumiliki
Ninafahamu kwamba yako maswali sugu tena ya miaka mingi ambayo huulizwa na kila mwenye mashaka na falsafa ya kumiliki. Maswali hayo ni kama haya yafuatayo: i) Hivi huu Ukombozi wa Yesu Kristo kwa binadamu ni maisha ya sasa au siku ya kiyama? ii) Kwanini wengi wanaodai kumfuata Yesu Kristo maisha yao ni yale yale ya mateso na umaskini wa kipato? Iii) Je Yesu mwenyewe si alishasema kuwa ulimwenguni tunayo dhiki, na mitume wake nao wakathibitisha kwamba tunaingia mbinguni kwa njia  ya dhiki nyingi? 
Majibu ya maswali haya ni muhimu sana kwa kila asomaye makala haya, na bila shaka atapata fursa ya kuzipima nadharia zilizopo na majibu yangu:
1. Majibu ya ukombozi wa Yesu ni maisha ya sasa au siku ya kiyama?
Ukombozi wa Yesu Kristo kwa binadamu ni maisha ya sasa na kilele chake ni kunyakuliwa kwa kanisa duniani. Ukifuatilia kwa makini katika Injili zote kuhusu maisha ya Yesu Kristo duniani, utakuta alihubiri Injili ya ufalme iliyoambatana na udhihisho wa mamlaka ya kifalme katika kutatua matatizo sugu matatu: kusamehe dhambi, kuponya ulemavu na magonjwa yote; na kushughulikia mahitaji ya chakula yalipojitokeza. 
Aidha, kanisa la kwanza lililoanzishwa na mitume jijini Yerusalemu nalo lilidhihirisha maisha ya kifalme kwa kuhakikisha watu wanatubu dhambi na kuzaliwa mara ya pili, kuponywa magonjwa yote, na kila aliyejiunga na kanisa hilo aliacchana na umaskini wa kipato. Kwa hiyo maisha ya ukombozi wa Yesu Kristo yanaanzia hapaa hapa duniani kama yalivyodhihirishwa na Yesu Kristo, mitume wake na wakristo wa kanisa la kwanza! 
Hata hivyo, bado mchakato wa kumiliki unaendelea na utafikia kilele chake wakati Yesu Kristo atakapolichukua kanisa lake na kwenda kukaa nalo pale mahali aliposema anakwenda kuliandalia makao.
Kwa kusema haya, sipuuzii uhalisia wa mambo jinsi yanavyoonekana kwa macho hapa duniani kwa hivi sasa. Uhaalisia unaonesha jinsi ambavyo maisha ya wengi waitwao wachaji Mungu, wafuasi waamini wa Yesu ni duni na kujaa changamoto nyingi za kiuchumi. Mimi pia nimepitia maisha haya haya tangu mwanzoni mwa uchanga wa imani yangu katika Kristo na mapokeo niliyofundishwa hapo awali.
Naomba nijibu sio kama majivuno bali kwa unyenyekevu mkubwa kwamba, changamoto zote zinazoonekana hivi sasa, hazitokani na wala sio sehemu ya Injili ya Yesu Kristo na Mitume wake. Haya ni matunda ya ukengeufu wa karne nyingi huko nyuma ambao ulizalisha “Ukristo bandia” katika ulimwengu huu! 
Nadhari ya kwamba, maisha ya dhambi na umaskini ndio dhiki za mkristo duniani mpaka Yesu atakaporudi mara ya pili ni matokeo ya ukengeufu ule ambayo Yesu Kristo mwenyewe aliutabiri kuwa utakuja na kuwakumba walio wengi! Kumbukeni mfano wa ngano na magugu ambao Yesu aliwaambia waanfunzi wake na tafsiri aliyoitoa. 
Ukristo bandia umeshika nafasi kubwa ulimwenguni kwa kuwaaminisha watu kuishi katika dhambi kisha kuungama na kuendelea maisha ya dhambi kanisani; badala ya kuzaliwa mara ya pili na kupokea uwezo wa kushinda dhambi (wanaona  ni fahari kuitwa wenyedhambi)
Hata kwa wale wanaopokea neema ya kuujua Ukristo wa kweli, na kuzaliwa mara ya pili, kwa sababu ya mapokeo ya ukristo bandia, bado huendelea kuaminishwa kwamba, maisha ya umaskini wa kipato ni njia mojawapo ya utakatifu, na kumiliki uchumi na tamaa za kiulimwengu. Kwa imani hii, huendelea kuishi maisha duni, ambayo matokeo yake walio wengi huiacha imani na kurudi duniani. Mungu atusaide sana!!!
Lakini tukumbuke kwamba KANISA LA KWANZA kwa muda wa miaka 40 mfululizo, likiwa na zaidi ya washirika 30,000 lilidhihirisha maisha ya ukombozi wa Kristo duniani; dhambi ilikemewa, wagonjwa wote waliponywa, na hapakuwepo na maskini wa kipato!
2. Majibu kuhusu dhiki iliyotajwa na Yesu na mitume wake
Neno hili “dhiki” limekuwa likitafsiriwa kinyume ili kuhalalisha maisha ya mikandamizo ya kipepo, nagonjwa na umaskini wa kipato kwa wachaji Mungu kanisani. Yametumika kama faraja lakini nyuma yake ni mbinu za adui za kufanya wahusika kuchukuliana na maisha haya kwa kudhani ni mapenzi ya Mungu wawe hivyo haoa duniani! 
Kwa kifupi Maneno ya Matoleo ya Biblia za Kiingereza yaliyotumika kutafsiri neno hili “dhiki” ni “hard times” “persecutions” na “tribulations”! Tafsiri ya maneno haya ni “Nyakati ngumu”, “mateso” na “mateso makali” au adha! Hapa hatusomi habari za dhiki kuitwa “magonjwa” wala “maskini uliokithiri”!
Baadhi ya maandiko ambayo yametumiwa sana ni kauli ya Yesu Kristo aliwapowambia kwmaba: “..Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” (YH.16:33)
Maana ya neno “dhiki” lililotajwa hapa ni upinzani mkali dhidi ya imani katika Kristo wenye kuambatana na vitisho, na mateso ya mapigo ya viboko, na vifungo  vya gerezani. Hii ndiyo dhiki aliyomaanisha Yesu. Isitoshe, Yesu aliwoanya pia wanafunzi wake kwamba sio kwamba watateswa kwa sababu ya imani yao kwake, bali hata kuuawa pia: “watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.” (Yh.13:2)
Baada ya Yesu kupaa, na mitume wake kuchukua nafasi ya kuhubiri Injili ambayo ilikuwa imepigwa marufuku na wakuu wa dini na dola, ndipo yalipotimia maneno ya Yesu Kristo ya kupatwa na “dhiki nyingi” ambazo zimetajwa na Luka alipoandika: “Wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.” (Mdo.14:22) 
Majumuisho ya majibu ya maswali
Kama nilivyokwisha kuanisha hapa juu, falsafa ya kumilikisha ni urithi wa Agano Jipya kwa wote wanaomjia Yesu Kristo. Ukombozi wa Yesu Kristo unajumuisha msamaha wa dhambi, unaosababisha kufutwa kwa adhabu ya maradhi na umaskini wa kipato. Jamii ya waaminio imeahidiwa kuishi maisha ya kifalme duniani na kilele chake ni mbinguni Yesu atakapolichukua kanisa lake. Dhiki inayotajwa duniani sio umaskini wa kipato bali chuki na upinzani dhidi ya imani unaoambatana na vitisho na mateso ya kimwili pamoja na kuuawa inapobidi.
Katika makala nyingine baada ya hii, nitaongelea changamoto za “Injili ya utajirisho” iliyojengwa kwenye “utoaji wa mali na fedha” kuwa ndiyo njia pekee ya kupata utajiri duniani. Aidha tutapitia maswali tata yanayohoji: Kwanini wanaotoa sadaka hawapokei matokeo ya utoaji wao kama wanavyoahidiwa? Je! Kwanini “utoaji wa siku hizi” unaonekana kuwanufaisha “wapokeaji” kuliko “watoaji”? Na utoaji ulio kamili wenye matokeo kama ilivyoandikwa katika Biblia ukoje? Nitaweka bayana tofauti kubwa iliyopo kati ya “Falsafa ya kumiliki” na “Injili ya utajirisho”!

Itaendelea toleo lijalo

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni