YESU NI JIBU

Jumatano, 15 Januari 2014

FALSAFA YA UMILIKISHAJI KWA MUJIBU WA BIBLIA



Kutana na askofu mkuu wa WAPO mission International uweze kufahamu kwa undani juu falsafa ya umilikishaji kwa mujibu wa biblia

Baada ya kutoa taarifa ya kongamano la vijana na tamko lao; leo naomba
nikutambulishe rasmi kuhusu kampeni mpya ambayo WAPO MISSION INTERNATIONAL imeitangaza mwaka huu inayoitwa OPERESHENI MILIKISHA. Hoja ya leo ni kuitambulisha kwako kampeni hii kuanzia sababu zake, malengo yake na matarajio yake nini:



Propaganda za kulinda amani

na kufuta umaskini wa kipato



Amini usiamini, humu duniani kuna mambo ya kustaajabisha ukiyagundua katika uhalisia wake.  Naomba nitumie mfano hai wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Sudani ya Kusini. Mpaka ninapoandika makala haya; wakati vita vinaendelea kwenye uwanja wa mapambano, na raia wasio na hatia wanauawa na wengine kukimbia na kuyaacha makazi yao; eti vikao vya kutafuta amani nchini humo vinaendelea jijini Adis Ababa Ethiopia, na pande mbili husika zinajadiliana jinsi ya kusitisha vita!!  Swali la msingi ambalo haliko kwenye mjadala wa AdisAbaba ni Nani anadhamini vita hivyo? Nani anayefanya biashara ya silaha zinazotumika kuuana nchini Sudani? Je naye yuko kwenye kikao cha kujadili ajenda ya kusitisha vita Sudani?

Ndivyo ilivyo na Vita dhidi ya Umaskini wa kipato katika jamii za nchi zenye majina rasmi ya nchi za ulimwengu wa tatu. Wakati rasirimali za asili (ambazo zina uwezo wa kufuta 100% umaskini wa kipato wan chi husika) zinaendelea kuchukiliwa bure, au kwa manunuzi yasiyo na tija kwa nchi husika; na kisha rasirimali hizo  hizo zinazalisha bidhaa ambazo hurejeshwa kwenye soko la nchi maskini  kwa bei za juu; na kutenegeza faida kubwa; eti matajiri wa ulimwengu wa kwanza wanasadikiwa kudhamini mipango ya kufuta umaskini wa kipato katika nchi hizo hizo zinazoporwa utajiri wake wa asili!

Hivi kweli kuna nia ya dhati (kutoka kwa matajiri wa ulimwengu wa kwanza), ya kufuta umaskini wa kipato kwa nchi maskini? Hivi kama kweli matajiri hao wangelitaka kuufuta kweli umaskini ingewachukua zaidi ya miaka ya 50 kukamilisha zoezi hilo?

Nadhani tumefika wakati muafaka wa kutokumung’unya maneno. Amani na utulivu, na kufutwa kwa umaskini wa kipato haviwezi kutoweka kwa juhudi za matajiri wa ulimwengu wa kwanza, wakati biashara zao zimejengwa katika misingi ya biashara ya kutengeneza na kuuza silaha, na kupora rasirimali za asili kwa nchi maskini. Mwenye kutaka kuamini kwamba kuna siku umaskini wa kipato utatoweka kutoka kwa matajiri atambue kwamba umaskini wake ndio unaowaneemesha matajiri hao.

Mwenye nia ya dhati ya kuleta amani

na kufuta umaskini ni Mungu peke yake.



Ni Mungu peke yake ndiye awezaye kutuliza ghasia na kurejesha amani na utulivu katika jamii; na kisha ndiye mwenye nia na uwezo kufuta umaskini wa kipato kwa maskini.

Kwanini nasema hivi?  Majibu ya swali hili ndiyo hoja maalum katika makala haya. Naomba nistafsiriwe kuwa naleta majibu mepesi kwa maswali magumu. Naomba nitumie fursa hii kuthibitisha ukweli, uzito na ushahidi ni kwanini nasema Mungu peke yake ndiye mwenye ufumbuzi wa changamoto nilizozitaja hapa juu.

Maono asilia ya Mungu kuhusu binadamu

Kwa wale tunaoamini kwamba binadamu ameumbwa na Mungu kama livyoandikwa katika Biblia, tunao ushahidi wa kimaandiko kwamba maono ya Mungu kuhusu binadamu hayakuwa na nia ya kumfanya binadamu kuwa fukara na maisha ya fujo na ghasia duniani.

Tukisoma maandiko kuhusu maono ya Mungu juu ya binadamu tusoma kwamba: “Mungu akasema na tumfanye mtu kwa mfano wetu; na kwa sura yetu; wakatawale…..” (Mw.1:26)

Andiko hili linadhihirisha bayana kusudi la Mungu kuhusu binadamu hata kabla hajamuumba. 1. Kuumbwa kiumbe anayeshabihiana na Mungu kwa fikra, hisia na utashi; 2. Kuumbwa kiumbe atakayemwakilisha Mungu katika utawala wa dunia na viumbe vyote vilivyomo.

Kutokana na Maono haya Mungu aliyatimiza kwa kuwaumba binadamu wa kwanza, Mwanamume na mwanamke, kama ilivyoandikwa: “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale…..” (Mw.1:27-28)

Kutokana na ushahidi wa kimaandiko tuliyosoma hapa juu, tunathibitisha kwamba binadamu wa kwanza waliumbwa katika hali ya utukufu wa Mungu, na wakamilikishwa kuitawala nchi na viumbe vyote vilivyomo. Kwa maelezo mengine ni kwamba, haki na mamlaka ya kumiliki ni ya kimaumbile. Hisia ya kumiliki ni sehemu ya maumbile ya  kila binadamu.

Pasipo kujali binadamu yuko katika mazingira ya aina gani hisia ya kumiliki imo ndani yake. Maswali mengi yanayojitokeza ni kama huu ndio ukweli tena wa kimaumbile kwa kila binadamu, kwanini basi hivi sasa kuna matabaka ya maskini na matajiri, watumwa na mabwana, waajiri na wajiriwa? Majibu ya maswali haya yanatupeleka kwenye sehemu ya pili ya falisafa ya umilikishaji.

Kuvunjika kwa mahusiano na kupoteza mamlaka

Baada ya binadamu wa kwanza kuumbwa, na kumilikishwa kama Mungu alivyowakusudia, binadamu hao hao walifanya maamuzi mabaya ambayo yaliwagharimu matokeo mabaya. Mungu alipowamilikisha aliwapa sheria ya kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, na akawaonya kwamba siku watakapokiuka sheria hiyo, watavunja mahusiano na yeye, na pia watapoteza sio mamlaka ya utwala peke yake, bali wasitisha na maisha ya umilele duniani.

Adamu na Eva walipokiuka sheria ya Mungu; ghafla wakajikuta wamefarakana na Mungu kama livyoandikwa: “…kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;..” (Rum.3:23)

Kwa bahati mbaya, uvunjwaji wa sheria ya Mungu ulifanywa na binadamu wa kwanza wale wale ambao ndio walitakiwa kubaki mfano wa vizazi vya binadamu vinavyofuatia. Biblia imeandikwa kwamba:“Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa             dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote             wamefanya dhambi.” (Rum.5:12)

Kutokana na maandiko tunaona kwamba kwa kosa la binadamu kuliathiri vizazi vyote vya binadamu waliofuata baada yao. Na athari hazikuishia katika kupoteza utukufu wa Mungu, bali ulisababisha kunywang’anywa ile mamlaka ya utawala. Lakini Mungu atukuzwe kwa sababu hakuridhika na athari zilizomsibu binadamu bali aliandaa mpango maalum wa kumkomboa na kumrejesha katika asili yake ya kwanza. Mpango huu tutaupitia katika makala yajayo.


Itaendelea wiki ijayo

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni