YESU NI JIBU

Jumamosi, 5 Novemba 2016

MAHAKAMA KUU YAZUIA KUFUKUZWA MAKAMU ASKOFU WA EAGT

Mapanga yatumika kulinda Kanisa alipozikwa Ask.Kulola,
Miaka mitatu na siku 50 hivi, tangu Askofu Mkuu na Mwanzilishi wa kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) DK. Moses Kulola kumaliza kazi hapa duniani, (kufariki) hali si shwari ndani ya kansia aliloacha, baada ya Makamu Askofu Mkuu, John Maene kufukuzwa katika uongozi na uchungaji katika kanisa la Bungando, Mwanza, lilipo kaburi la mwanainjili huyo na kuzua kiza kinene katika mustakabali wa kiroho.
Habari za ndani toka ndani ya kanisa hilo zinaeleza kuwa tangu kutwaliwa kwa kiongozi huyo, ilizuka hali ya sintofahamu kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutoelewana baina ya wale wanaoelezwa kuwa ni “wa Kulola” yaani wafuasi wake  sugu na wale wa kizazi kipya kinachotaka kubadili mambo na kujenga himaya mpya.
Ni katika hali hiyo, hivi karibuni aliyekuwa Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, John Maene, alifukuzwa uongozi na uchungaji kwa kile kilichodaiwa kuwa alipatikana na tuhuma za ukiukaji wa kimaadili, lakini akapinga tuhuma mbele ya Halmashauri ya kanisa na kasha kufungua Kesi katika mahakama Kuu kanda ya Mwanza.

Taarifa zilizothibitishwa na mmoja wa wazee wa kanisa la Buganda (Jina linahifadhiwa kwa sasa) zinaeleza kuwa, kiongozi huyo alifungua shauri la Madai Mahakama kuu mwanzoni mwa wiki iliyopita, sambamba na kuomba amri ya mahakama ya kuzuia utekelezaji wa maamuzi ya Halmashauri ya kanisa wa kumfukuza hadi pale shauri ilililopo mahakamani litakapopata ufumbuzi.
“Tayari tumepata amri ya Mahakama, lakini pia vijana wameamua kulilinda kanisa kutokana na njiama zinazoendelea chini kwa chini kwani wachungaji wanaotaka kutekeleza amri “haramu” wamejifungia kwenye kanisa moja wakiendelea kujadiliana hatujua wanapanga nini,”alisema Mzee huyo ambaye alisema wazi kuwa wanasimama na kiongozi wao (Askofu Maene) hadi dakika za mwisho na kuwa Mungu atawatetea.
MTIRIRIKO WA MATUKIO
Mtiririko wa matukio yanayoashiria kuwa hali si shwari ndani ya kanisa la EAGT,  yalianza wiki iliyopita baada ya kikao cha Halmashauri kuu na Baraza la waangalizi wa kanisa hilo, vilivyofanyikia mjini Dodoma kuamua kuizinisha kutimuliwa kwa Makamu Askofu Mkuu kwa kile kilichodaiwa kuwa alituhumiwa kukiuka maadili.
Hata hivyo, Makamu huyo alipopewa nafasi ya kujitetea mbele ya Baraza la waangalizi alikanusha tuhuma hizo ambazo inadaiwa kuwa chanzo chake ni unabii uliotolewa na mmoja wa manabii wa kanisa hilo, na wajumbe wakaonekana kumuelewa, lakini uongozi wa kamati kuu ukatishia kujiudhulu na kuliacha kanisa ikiwa wajumbe wangekataa kuidhinisha mpango huo, ndipo maamuzi yakafikiwa.
Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni Mjane wa Marehemu Askofu Kulola Elizabeth Kulola, ambaye hakukubaliana na wenzake baada ya kumuuliza mtuhumiwa akakanusha tuhuma zake.
WAZEE WAFUKUZWA BUGANDO
Nyakati linafahamu kuwa baada ya mambo kwenda mrama, Makamu Askofu Maene, aliondoka mjini Dodoma na kurejea Mwanza ambapo Jumamosi baadhi ya wazee wa kanisa walimtaka aende kwenye kikao kujadili suala la kufukuzwa lakini, hakwenda aliwajibu kuwa wangekutana ibadani na Jumapili asubuhi alienda ibadani kama vile hakuna kilichotokea, lakini alipopanda madhabahuni baada ya nyimbo za sifa, kuabudu kumalizika alieleza mkasa wote na kueleza msimamo wake kuwa yeye bado ni Makamu Askofu Mkuu wa EAGT, mpaka suala la kile anachotuhumiwa litakapojadiliwa na Mkutano Mkuu.
Kasha aliwaeleza waumini kuwa yeye ni mchungaji kiongozi wa kanisa hilo kihalali na kasha akawatimu wazee wa kanisa ambao walituhumiwa kuwa wachochezi. Majina ya wazee tunayahifadhi mpaka tutakapowapa nafasi ya kujitetea) .
Baada ya msimamo huo kanisa lilirindima kwa shangwe na kuahidi kumuungamkono mchungaji wao hadi tone la mwisho la mapambano waliyoyaita ya kutetea haki yao,
WACHUNGAJI WATIMUA MBIO
Baada ya tukio la Jumapili mapambano yalihamia mahakamani ambapo jumatatu wanasheria walitinga Mahakama Kuu na kufungua shauri, lakini Jumatano mambo yalibadilika baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa barua ya kumtimua mhungaji wao ilikuwa mikononi mwa wajumbe wakiipeleka  na kuwa mchungaji mbadala kutoka shinyanga alikuwa tayari amefika mwanza mjini.
Waumini wakakumbushana kuwa huenda amri ya mahakama isingeheshimiwa kama ilivyotokea Jijini Dar es Salaam, ambapo mahakama ya Wilaya ya Temeke ilitoa amri ya kuzuia mkutano wa kanda uliokuwa umeitishwa kwa dharura na amri ya mahakama ikafikishwa kwa wadhamini, lakini wakaendelea na kasha wakatekeleza uamuzi waliokusudia kuufanya.
Ni katika hofu hiyo inaelezwa kuwa vijana shupavu wa kanisa la EAGT Bugando, wakayanoa mapanga na kujaa katika viwaja vya kanisa huku wakisisiza  kuwa wako tayari kwa lolote ili kumlindaz mchungaji wao.
Majira ya saa tatu asubuhi Mjane wa Askofu Kulola alifika kanisani hapo na kwenda moja kwa moja kwenye kaburi alipozikwa mumewe Akaka juu yake na kuwasema kuwa  yote yatokee lakini mtu asisogelee kaburi hilo.
Inaelezwa kuwa maneno hayo yalizidisha ghadhabu  ya walizni  na wakati ikisubiriwa nini kitatokea, baadhi ya wachungaji wanaominika kuungamkono maamuzi ya kanisa walifika kanisani hapo lakini wakakumbana na vitisho vya vijana hao ambapo walilazimika kutimua mbio, huku wengine wakiruka ukuta  kujiokoa. (majina ya wachungaji walionusurika tunayahifadhi kwa sasa).
Nyakati ilipompigia Katibu Mkuu wa EAGT, Mch.Leonald   Mwezarubi,  simu yake iliita tu bila kupokelewa kwa muda mrefu.
Askofu Mkuu wa EAGT, Dr.Brown Mwakipesile alipoulizwa kuhusu hali hiyo na mtakabali wa kanisa alisema kwa kifupi kuwa kanisa linaandaa tamko na kwa sasa wana lakusema.
Tangu alipofariki Askofu Mkuu  na mwanzilishi wa kanisa la EAGT Dr.Moses kulola, Agosti 29, mwaka 2013 katika hospitali ya AMI (African Medical Investments) iliyopo Slipway jijini Dar es Salaam, alipokuwa amelazwa baada ya kurejea kutoka katika matibabu  huko India kumekuwa na mfululizo wa matukio yanye utata yaliyoanza  hata kabla ya mwiliwake kurejeshwa mavumbini.

Tukio la kwanza lilikuwa lile la bodi ya wadhamini wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwenda mahakamani kuwasilisha pingamizi la kutoruhusu mwili wa Dkt. Moses Kulola kuzikwa katika viwanja vya kanisa hilo lililopo maeneo ya Bugando jijini Mwanza wakidai ni mali yao.
Lakini sasa wamerejea tena mahakama ile ile na safari hii ni makamu askofu anayelalamika kuonewa na kukiukwa kwa kanuni  kikatiba na utawala wa haki katika kumsimamisha uongozi na kumvua uchungaji.
NGUVU ZA ASKOFU MAHENE
Ingawa wengi wanautazama mgogoro huo kama unaomhusu mtu mmoja lakini ukweli ni kuwa nyuma ya Mchungaji Mahene ambaye ni mzee wa miaka 70 hivi kuna umati wa wachungaji kutoka kanda ya ziwa waliomuwezesha kuwa na upinzani mkali  katika uchaguzi wa viongozxi wa kanisa hilo mwaka jana.
Nyakati linafahamu kuwa katika uchaguzi huo, Mhane, Mwezarubi na mwakipesile walikuwa na ushindanbi katika nafasi ya Askofu Mkuu na kusababisha kura kurejewa mara tatu, hadi pale Mwezarubi alipoamua kujitoa na kusalia, Mwakipesile na Mahene.
Ni katika marudio hayo, Mwakipesile aliibuka mshindi na baadaye mshindani wake (Mahene) akatwaa nafasi ya makamu Askofu na Mwezarubi akawa katibu mkuu, hivyo watatu hawa wana nguvu zinbazokaribiana ndanbi ya kanisa hilo.
HOFU YA KUGAWANYIKA  KWA EAGT

Wakati sasa makabiliano yakihamia kortini kuna kila dalili za kanisa hilo ambalo mwanzo wake ni kugawanyika kutoka TAG, likagawanyika tena kufuatia kile kinachoelezwa kuwa ni hofu ya kuandamwa kwa wale wanaoitwa “wa-Kulola” yaani wanasalia kushika misingi aliyoacha mzee wa Injili Kulola na wanahofiwa kuwa tishio katika siasa za kanisa.

Mmoja wa wachungaji waliopo karibu na uongozi aliliambia nyakati kuwa kinachoendelea sasa ni kulisafisha kanisa kwa mambo mawili maombi  na kufuata kanuni kwa kuwaondoa wale wanaoonekana sio watii na waliotenda dhambi.
“Tuko kwenye maombi tunamuomba Mungu mtu akileta ujanja na uwezo wake atapambana na Mungu, mkuu amesema anasafisha kanisa hata wakibaki nane wanaoshika imani hao watatosha vinginevyo atajiondoa akafanye kazi zingine…”alisema mmoja wa wachungaji waliopo karibu na uongozi wa sasa.

Aidha imeelezwa kuwa kufuatia hali hiyo ya “Matengenezo” baadhi ya waqchungaji wamekuwa na hofu kwa kile kinachoelezwa kuwa “mwenzio akinyolewa tia kichwa maji” hali inayompa Askofu Mahene nguvu ya kusaidiwa.

TETESI ZA BUGANDO KUREJEA TAG
Wakati tukienda mitamboni kulienea madai kuwa mgogoro wa EAGT, Bugando unaweza kutimiza usemi kuwa “Vita vya panzi ni karabu ya mjusi” kwani kanisa hilo kwa muda mrefu lilikuwa na mvutano baina ya EAGT na TAG, na nyaraka yaani hati za ofa wanazo TAG, hivyo itakuwa vigumu kwa uongozi wa EAGT kulitetea ipasavyo kortini.


Ni hali hiyo inayoleta wasi wasi kuwa mambo yakienda vibaya linaweza kujikuta likirejea mikononi mwa TAG, lakini hakuna msemaji  yeyote baina ya makanisa hayo mawili aliyekuwa tayari kuzungumzia tetesi hizo.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni