Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo
Mwanamke
mkazi wa Unga-Limited jijini Arusha , Lightness Kivuyo ameripotiwa kufa wakati
akifanyiwa maombi nyumbani kwa mchungaji aliyejulikana kama ‘Nabii Rajabu’ eneo
la Kwa-Mrombo pia jijini Arusha.
Kwa
mujibu wa dada wa marehemu, Juliana Kivuyo, Lightness alikuwa amesindikizwa
nyumbani kwa nabii huyo nyakati za usiku na mumewe aliyemtambulisha kama Shafii
Mohammed na kwamba wakati akifanyiwa ibada ya maombi, alianguka na kufariki
miguuni mwa ‘Mtume,’ huyo.
“Baadaye shemeji alikuja nyumbani akihema, huku
anadai kuwa dada alikuwa kwenye hali mbaya kule kwenye maombi,” alisema Juliana na
kuongeza kuwa alitoka mbio kwenda Kwa-Mrombo nyumbani kwa Nabii Rajab na
kumkuta dada yake amelazwa kwenye kochi, akiwa bila nguo isipokuwa tu khanga
alizofunikwa nazo.
Nabii
huyo pia anadaiwa kumnyoa nywele zote pamoja na nyusi za macho wakati
akimfanyia ‘huduma,’ hiyo.
Polisi
jijini hapa wamethibitisha tukio hilo wakiongeza kuwa tayari watu wawili
wamekamatwa kutokana na kifo hicho cha ‘maombi tatanishi.’
Aidha,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo ameongeza kuwa atatoa taarifa kamili
mara baada ya kikao chake na Mkuu wa Mkoa.
Mganga
Mkuu katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Jacqueline Uriwo amekiri
kupokea mwili wa marehemu, lakini akasema, “Kwanza walijaribu kutudanganya kuwa huyo mama alikuwa hai na kwamba
aliletwa kwa ajili ya matibabu, lakini tukagundua kuwa walichokileta ni mwili mfu,
hivyo tukampeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti!.”
Mkurugenzi
wa Huduma ya Mazishi katika hospitali hiyo ya mkoa, Dk Francis Coster alisema
mwili ulipelekwa hapo na mume wa marehemu ambaye alisisitiza kuwa mkewe hajafa,
bali kazimia tu na kwamba mara nyingi huzimia kwa saa nyingi.
Dk
Coster aliongeza kuwa ilibidi na wao wasiweke mwili kwenye jokofu na kuulaza
kwenye machela kwa saa sita na ndipo wakaamua kuuweka kwenye droo za maiti,
kwani ilikuwa wazi sasa kwamba asingeamka tena asilani.
Waganga
hospitalini hapo wamekiri kuwa mwili wa marehemu uliletwa hospitalini hapo
ukiwa umenyolewa upara, lakini ukiwa na mikwaruzo pamoja na uvimbe hususan
maeneo ya mikono na kifua.
Baba
mkubwa wa marehemu, Ally Kivuyo ambaye ndiye mlezi wa Lightness, alisema mume
wa marehemu alimtaarifu juu ya kifo hicho na kuongeza; “Lakini baadaye nikaletewa taarifa nyingine kuwa Lightness kumbe alikufa
wakati akifanyiwa maombi au vitu vingine, nyumbani kwa mtu anayeitwa ‘Nabii
Rajabu,’ hapo basi ikabidi niwataarifu polisi ambao walikuja kumkamata mumewe
pamoja na huyo anayejiita nabii au mtabiri.”
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni