YESU NI JIBU

Jumapili, 9 Desemba 2012

KANISA LACHOMWA MARA TATU MARA TATU LIKIKARABATIWA HUCHOMWA TENA WAHUSIKA WADAIWA NI WAUMINI WA DINI YA KIISLAMU




Wakati serikali ikijitahidi kukabiliana na vitendo vya uchomaji moto makanisa nchini vinavyofanywa na baadhi ya wanaharakati wa Kiislamu, imebainika kuwa Kanisa la Salvation Ministry for all Nations (SMAN) lililoko Mbezi Juu Jijini Dar es Salaam, limechomwa moto zaidi ya mara tatu.
Uongozi wa Kanisa hilo umelimbia Gazeti hili kuwa licha ya matukio hayo ya hujuma wanazofanyiwa na waumini wa Kiislamu kutoka katika msikiti wa Al Mubarak ulioko jirani na Kanisa hilo, usiku wa Jumapili iliyopita ya Desemba 2, 2012 , waumini hao walilibomoa Kanisa hilo na kufanya jaribio jingine tena la kulichoma moto.
Kwa mujibu wa Mchungaji kiongozi wa Kanisa hilo la SMAN Freddy Mwamtembe na Msaidizi wake Mch. Eliya Sudi, matukio matano ya hujuma mbaya dhidi yao yameripotiwa katika vituo vya polisi Mbezi Juu na Kawe na kufunguliwa majalada   yanayoeleza jinsi hujuma hizo zilivyofanyika kwa muda na nyakati tofauti.
Hujuma ya kwanza ya uharibifu mali na uchomaji moto wa Kanisa hilo iliripotiwa katika akituo cha polisi Kawe Februari 25, 2012  na kufunguliwa jalada nambari KW/RB/1743/2012 la kuchoma moto  choo cha kanisa hilo, ambapo jalada la pili la siku hiyo hiyo lilifunguliwa katika kituo cha Polisi Mbezi Juu likiwa na nambari MBJ/RB/586/2012 likitaarifu juu ya tukio la kuchomwa moto Kanisa hilo na kuharibu mali majira ya saa saba usiku.
Jalada jingine lilifunguliwa Machi 10, 2012 katika kituo cha Polisi  Mbezi juu na kupewa nambari MBJ/RB/714/2012, likitoa taarifa juu ya hujuma ya kuchomwa moto kwa Kanisa hilo la SMAN.
Hujuma nyingine lililofanyiwa kanisa hilo imo katika jalada la kituo cha Polisi Kawe lenye nambari KW/RB/7974/2012 kama taarifa ya  tukio lililofanywa Agosti 12, 2012 na waumini 28  wa msikiti wa Al Mubarak kwa kuvamia ibada, kujeruhi waumini na kuharibu mali za Kanisa hilo, ambapo Mchungaji Msaidizi Eliya Sudi alijeruhiwa akiwa madhabahuni.
Aidha uongozi wa Kanisa hilo ulilikabidha gazeti hili waraka unaoelezea jinsi waumini wa msikiti huo wanavyoshirikiana na mama mmoja kulifanyia fujo kwa kufukia msingi wa jengo lake na kisha mama huyo kuchimba msingi na kuanza ujenzi wa nyuma yake katika kiwanja cha Kanisa hilo.
Uongozi huo wa Kanisa la SMAN  ulisema ulilifikisha suala hilo katika ofisi ya Serikali ya Mtaa wa  Ndumbwi kupitia mjumbe wa nyumba kumi shina namba 40  Mbezi Juu Bwana Bonifasi Matiku  kwa ajili ya utatuzi, lakini hawakupatiwa msaada wowote, hadi ikabidi wamwandike barua Afisa Mtendaji wa kata ya Mbezi Juu, kumtaarifu juu ya kiwanja cha kanisa lao kuvamia na mama huyo ambaye kwa sasa jina lake limehifadhiwa.
Mjumbe huyo alidhibitisha juu ya kuwepo kwa hujuma dhidi ya Kanisa hilo na hatua alizochukua,ambapo liitaka serikali kutumia sheria ili kukabiliana nazo na kuzikomesha.
“Nakumbuka siku nilipofika  ofisini kwa Mtendaji wa Kata ya Mbezi Juu,  niliishia kutukanwa na wajumbe niliowakuta pale (majina tumeyahifadhi kwa sasa), wakinieleza mbele ya Mtendaji huyo kwamba ni lazima mama huyo  atajenga katika eneo la kiwanja chetu cha Kanisa. Nilimtahadharisha Mtendaji juu ya matusi niliyotukanwa lakini akanitaka niondoke akidai atashughulikia suala hilo. Mwandishi  hadi leo hakuna kilichofanyika”, alisema Mchungaji Mwamtembe.
Alisema tayari amelifikisha suala la  hujuma za Waislamu dhidi ya Kanisa lake katika ofisi za Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni alikoahidiwa kushughulikiwa haraka kwa mujibu wa sheria.
“Kwa kweli sisi Wakristo ni wavumilivu sana kwa vile tunapenda amani na utakatifu. Tunaiomba sana serikali iwashughulike watu hawa wachache wasiopenda amani na wanaochochea vurugu za kidini. Ugomvi wa kidini ni mbaya sana. Tunaomba serikali iwe makini katika hili”, alisema Mch. Mwamtembe.
Alisema waumini hao korofi wa Kiislamu wanaolihujumu Kanisa lake kwa kulichoma moto, kuharibu mali na kujeruhi  washirika ni watu wanaofahamika wazi na hufanya hujuma hizo wazi wazi, wakitamka wazi  kuwa hawataki Kanisa katika maeneo yao; jambo ambalo ni kinyume kabisa na Katiba ya nchi  inayoruhusu uhuru wa kuabudu kwa kila mtu
Mmoja wa Mashehe wa Msikiti  wa Al Mubarak Mbezi Juu aliyetajwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha waumini wake kulihujumu kanisa  la SMAN, hakuweza kupatikana kutokana na kutofika msikitini hapo kwa uwazi, akiogopa kukamatwa na Polisi wanaomsaka.  
Aidha juhudi za kumpata mama aliyetajwa kushirikiana na waumini wa msikiti wa Al Mubarak kulihujumu kanisa hilo hazikuzaa matunda,  kutokana na makazi yake kutojulikana.


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni