Tafsiri mpya ya msamiati wa
“Imani potofu”
Siku
hizi jamii imeanza kuchanganyikiwa na kile kinachoitwa “kuongezeka kwa imani
potofu” zenye kudanganya na kuathiri imani za wengi kiitikadi.
Kutokana
na uchunguzi wangu binafsi, nimekuja kubaini kwamba, mahali tulipofikia kumbe
tafsiri yake ina utata mkubwa na maana nyingi tena tofauti hata kama matamshi ni yale yale. Ninachotaka kuelezea hapa ni
kwamba, kila inayoitwa “imani potofu” na wengine, kumbe nayo inaziona imani
nyingine nje yake ndizo zimepotoka! Kwa maelezo mengine, tumefikia mahali
ambapo “Usahihi” wa imani yako ni “upotofu” wa imani kwa mwingine aliye tofauti
na wewe kiitikadi.
Ni
kutokana na utata huu, Mamlaka za nchi mbali mbali duniani zilifikia hatua za
ama kupiga marufuku “imani zote” na kubakia dini moja au chache zinazokubalika.
Kisha baadaye ikaonekana huu ni udikteta usiotenda haki kwa binadamu na hivyo likaanzishwa “Tamko la Haki za
binadamu ulimwenguni” ambalo pamoja na mambo mengine limejumuisha “haki ya
kuabudu” na kujiunga au kubadili dini. Kwa mujibu wa tamko hili fursa imetolewa
kuwepo kwa imani nyingi, zilizopo hivi sasa, na kuanzishwa mpya, ili mradi mtu
havunji sheria za nchi
Kwa
kupitia haki ya uhuru wa kueneza imani, kila mtu anapata fursa ya kuchagua au
kuacha, kujitenga au kujiunga na imani ile ambayo anaiona ndiyo sahihi kwa
uelewa na utashi wake binafsi. Kwetu sisi Tanzania, uhuru wa kuabudu ni haki
ya kikatiba.
Baada
ya kutoa maelezo ya msingi kuhusu utata wa tafsiri ya “Imani potofu”; naomba
sasa nije kwenye kuwasilisha tafsiri mpya ya msamiati wa “Imani potofu”.
Tafsiri hii kwa hivi sasa ndiyo inayotumika na sehemu kubwa ya jamii. Tafsiri
yenyewe ni kama ifuatavyo:
“imani yoyote inayokera imani nyingine; na
inapata umaarufu mkubwa kiasi cha kuwa tishio la kuvutia wafuasi wa imani
nyingine kujiunga nayo”
Imani
hiyo inaweza kuwa ni sahihi au potofu kulingana na mtazamo wa kila mtu kwa
itikadi yake, lakini kigezo kinachozingatiwa katika kuibatiza jina la “Imani
potofu”; ni pale ambapo “wafuasi wengi wa imani za dini nyingine wanaondoka au
kuyahama madhehebu yao na kujiunga na imani hiyo” ! Katika harakati za kujaribu
kudhibiti matishio ya imani hiyo, na kuwakinga waumini wao wasijiunge nayo ni
kuitangaza rasmi kuwa ni “imani potofu”
Naomba
nijihami mapema msomaji kwa kusema kwamba, kwa kusema haya sina nia ya
kuhalalisha “Imani potofu” kupitia mada hii. Naomba nisieleweke kwamba sio kila
“imani inayoshawishi maelefu ya watu kujiunga nayo ni sahihi au ni potofu”.
Hoja
ninayotaka kuiweka bayana ni kuhoji uhalali wa matumizi ya kigezo cha
“ushawishi na umaarufu mkubwa” kutafsiriwa kuwa imani husika ni potofu kwa
sababu hiyo tu! Ingelikuwa kigezo hiki kina mantiki, basi tungeweza kutilia
mashaka imani zote zenye wafuasi wengi kuwa zimefanikiwa kwa sababu nazo ni
“imani potofu”!
Mtazamo
wangu, na uzoefu wangu binafsi, imani zote, ziwe potofu au sahihi, ziwe mpya au
za zamani, zote zikiweka bidii kikamilifu katika kujieneza kwa jamii zinaweza
kuwa na wafuasi wengine pasipo kujali sana
usahihi au upotofu wake kiitikadi. Lakini naweza kukubali kwa sehemu kwamba
usahihi au upotofu wa imani unaweza kuchangia kwa kiasi fulani kufuatwa na
wafuasi wengine kwa kutegemea ni mbinu gani ya kimawasiliano inayotumika.
Dhana ya imani potofu kuwa na
wafuasi wengi kuliko imani sahihi
Baada
ya kuelezea tafsiri ya msamiati wa imani potofu kwamba ni ushawishi na umaarufu
wa kupata wafuasi wengi kwa haraka; na baada ya kubainisha waziwazi kwamba nia
ni kujaribu kuwakinga waamini wasihame na kujiunga na imani inayovuma kwa
wakati husika; sasa nije kwenye chimbuko la tafsiri hii iliyoshika hatamu
katika jamii.
Kwa
karne nyingi imekuwepo dhana kwamba, imani potofu ina uwezo wa kuwa na wafuasi
wengi kwa sababu zimetokana na Shetani mwenyewe. Tena yapo na maandiko
yatumikayo katika kusimamia dhana hii ua kwamba hata Yesu mwenyewe alitabiri
juu ya manabii wa uongo ambayo watadanganya wengi. (Math…….) Maandiko mengine
ni ya mitume akina Petro na Paulo yaliyolitahadharisha kanisa kwamba watakuwepo
mitume na manabii wa uongo ambao watatengeneza wafuasi wengi kwa ushawishi na
udanganyifu wao.
Kwanza kabisa, naomba kuthibitisha kwamba ni
kweli imani potofu zinapata wafuasi wengi kwa sababu zimejaa udanganyifu wa
Shetani. Tena naweza kuongezea uzito katika hoja hii kwa kusema kwamba,
kinachofanya imani potofu kupata wafuasi wengi ni kwa sababu hazina masharti
yenye maadili ya kiungu, na zimejaa uwashiwi unaohamasisha tamaa binafsi au
wanaotafuta msaada binafsi.
Lakini,
ninapenda kuzungumuzia udhaifu wa dhana hii. Sio kweli hata kidogo kwamba,
imani sahihi haipati wafuasi wengi kwa sababu yenyewe ndiyo imetokana na Mungu
wa kweli. Ingelikuwa hii ndiyo maana sahihi, basi Yesu Kristo mwenyewe, enzi za
mwili wake duniani, asingefuatwa na makumi elfu ya wafuasi wengi! Maneno yake
na mafundisho yake yalikuwa magumu na mifano mingi ilikuwa na mafumbo lakini
bado umati mkubwa wa watu ulimfuata na kumsikiliza na kushuhudia kwamba huyu ni
Mwalimu kweli kweli!
Kana
kwamba hii haitoshi, baada ya kufufuka na kupaa kwake, mitume wake nao
walitengeneza maelfu ya wafuasi na wanafunzi wengi kama
ilivyokuwa nyakati za Yesu mwenyewe. Kanisa la kwanza lilianza kwa kishindo cha
wafuasi 3000 kwa siku moja na katika muda wa miaka 40 mfululizo lilikuwa na
wafuasi wasiopungua 30,000 wanaokusanyika kwa wiki jijini Yerusalemu!
Ni
nini ninachotaka kusema hapa? Napenda kuweka bayana ukweli huu, kwamba hata
“Imani sahihi katika Kristo”, kama kweli kweli ikihubiriwa kwa usahihi kama Yesu na mitume wake wa kwanza; kazi zile zile
zilizofanyika enzi za karne ya kwanza pia zitatendeka hata sasa. Kwa matokeo
hayo makumi elfu ya watu wataikimbilia imani hii kwa wingi kama
ilivyokuwa karne ya kwanza.
Pamoja na ukweli kwamba “Imani potofu” zina
ushawishi wa kupata wafuasi wengi; lakini sio kwamba hao wafuasi wenyewe hutoka
kwenye imani sahihi na kisha kuijunga na imani potofu! Wengi wao hawakuwahi
hata kuijua “imani sahihi” tangu kuzaliwa kwao na ndio maana ni rahisi kwao
kujiunga na imani nyingine potofu!
Kwanini imani potofu
zimeruhusiwa
kuwepo sambamba na imani sahihi?
Kitu
ambacho kinatatiza watu wengi na hasa wale ambao ni wapenzi wa imani sahihi, ni
kuona jinsi ambavyo imani potofu zinaendelea kufumuka na kuendelea kupoteza
wafuasi wengine wasioijua au kuwa na imani sahihi. Wengine wanafunga na kuomba
wakijaribu kudhibiti ongezeko la imani potofu. Hata hivyo, ukweli halisi bado
imani potofu zinaongezeka kila siku.
Ningependa
kujibu swali hili gumu kwanza kwa kutahadharisha athari zitokanazo na shinikizo
la kutumia nguvu za dola kudhibiti imani potofu. Kujaribu kudhibiti mfumuko wa
imani potofu kupitia nguvu za Dola, kwanza ni kinyume cha katiba na tamko la
haki za binadamu. Pili, kila itikadi katika dini inatafsriwa kuwa potofu na
itikadi nyingine zinazotofautiana kiitikadi. Tatu nitalieleza kwa mujibu wa
mafundisho ya Bwana Yesu Kristo. Kabla sijaanza kufafanua hebu tuyasome maneno
ya Yesu kwa mfano alioutoa:
“Akawatolea
mfano mwingine, akisema, ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu
njema katika konde lake; lakini watu walipolala akaja adui yake akapanda magugu
katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa,
yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana,
hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia
adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, basi wataka twende
tuyakusanye? Akasema la; msije mkakusanya magugu na kuzing’oa ngano pamoja
nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno
nitawaambia wavunao, yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome;
bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.” (Math.13:24-30)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni