Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amewahimiza
wajasiriamali kuzingatia matumizi salama ya kemikali wanazotumia katika
uzalishaji wa bidhaa zao ili kulinda afya za binadamu na mazingira.
Dkt. Mafumiko ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam
alipotembelea maonesho ya wanawake wajasiriamali yaliyoandaliwa na Chama cha
Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ambayo yanafanyika kwenye viwanja vya
Mnazi Mmoja.
Aliwaeleza wajasiriamali hao kuwa Mamlaka ya Maabara
ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) katika utekelezaji wa majukumu yake imekuwa
ikitoa mafunzo kuhusu matumizi salama ya kemikali kwa wadau wake mbalimbali
wanaotumia kemikali wakiwemo wajasiriamali ili kuwapa elimu ya matumizi salama
ya kemikali pamoja na namna bora ya kuhifadhi bidhaa zao.
“Kwa nafasi yetu kama wasimamizi wa sheria ya kemikali
tuna jukumu la kuhakikisha watumiaji wa kemikali kama vile watengeneza batiki
na wanaosindika bidhaa za vyakula pamoja na dawa asili wanazingatia taratibu za
kiusalama, hivyo tunawaahidi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wadau hao,”
alisisitiza Dkt. Mafumiko.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TWCC, Mercy Sila alisema
kuwa katika zoezi la kuwafikia wajasiriamali, taasisi yake inapata ushirikiano
mzuri kutoka GCLA kwenye kuwaelimisha wajasiriamali hao namna bora na salama ya
kutumia kemikali katika uzalishaji wa bidhaa.
Aidha, baadhi ya wajasiriamali waliowahi kupata
mafunzo ya matumizi salama ya kemikali kutoka GCLA walieleza kuwa elimu waliyoipata
imewasaidia kuboresha bidhaa zao na kulinda afya zao bila kuchafua mazingira.
Naye mjasiriamali kutoka Zanzibar, Salma Othman ameiomba
GCLA iendelee kutoa elimu kwa wadau wengi zaidi kupitia njia mbalimbali ili
kuhakikisha jamii ya Watanzania inazingatia usalama wa afya za watu na
mazingira.
Maonesho hayo ya pili ya wajasiriamali wanawake yaliyoandaliwa
na TWCC yalianza Machi 3 mwaka huu na yanatarajiwa kukamilika Machi 8, 2022
ambayo ni Siku ya Wanawake Duniani.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni